Nafasi Ya Matangazo

July 23, 2015

Vijana skauti  4 pamoja na kiongozi mmoja ni miongoni mwa washiriki wa Jamboree ya  maskauti ya dunia itakayofanyika Nchini Japan katika mji wa Yamaguchi – Kihara hama  kuanzia tarehe 28 Julai hadi 8 Agosti 2015.

Jamboree ya  Skauti ya Dunia ni mkusanyiko wa  Skauti kutoka nchi zote wanachama na kawaida hufanyika kila baada ya miaka minne kama iliv yo kwa mashindano ya mpira ya kombe la dunia.

Mwanzilishi wa Chama cha Skauti duniani Hayati Lord Baden Powell alianzisha mfumo wa Jamboree ya  Skauti ya dunia kwa madhumuni ya kuwakutanisha vijana skauti kubadilishana mawazo na kujifunza mambo mbalimbali kutoka nchi tofauti tofauti.

Jamboree ya kwanza ya maskauti ya dunia ilifanyika London Uingereza mwaka 1920 na kuanzia mwaka huo imekuwa ikifanyika kila mwaka katika nchi tofauti tofauti.

Shirikisho la Vyama vya Skauti Dunia (WSB) World Scouts Bureau, ndio hupanga na kuchagua  nchi itakayo andaa Kambi hili la kimataifa katika kipindi kijacho.

Chama cha Skauti Tanzania inapeleka idadi ndogo ya washiriki kutokana na gharama kubwa za ushiriki wa kambi hii. Jumla ya dola za kimarekani 4000 sawa na milioni 8 za Kitanzania ndio gharama za ushiriki kwa mshiriki mmoja.

Gharama hizo ni pamoja na usafiri, chakula malazi na ada ya ushiriki wa kambi hiyo ambayo huchukua karibu siku 10.

Shughuli zinazofanyika wakati wa Jamboree hiyo ni pamoja na mafunzo mbalimbali ya stadi za kiskauti, kazi za Jamii, Moto wa Kambi, na siku moja maalum ya Kimataifa ambapo kila nchi wanachama huandaa maonyesho maalum kuonyesha bidhaa mbalimbali walizonazo ikiwa ni pamoja na kuonyesha utamaduni wao.

Kikosi cha skauti kutoka Tanzania kinawakilishwa na:-
Eline Kitali – Kamishna Mtendaji na Mkuu wa Msafara.
Michael Malima kutoka mkoa wa D’salaam
James Mzoma Chinula kutoka mkoa wa Kilimanajaro
Malkia Ulimboka Mwakilili kutoka mkoa wa Mbeya
Martha Albert Bennie. Kutoka mkoa wa Mwanza.


Skauti hao wanatarajia kuondoka nchini Jumamosi tarehe 25 Julai 2015 na shirika la ndege la Emirates  muda wa saa 10.45 alasiri  na wanatarajia kurejea nchini 10 Agosti 2015.

HIDAN .O. RICCO.
KAMISHNA MKUU MSAIDIZI
HABARI NA MAWASILIANO.

Posted by MROKI On Thursday, July 23, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo