Nafasi Ya Matangazo

September 29, 2014

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Meza Kuu-Katikati), akizungumza na wawakilishi wa Kampuni mbalimbali zinazohusika kusambaza umeme vijijini kutoka India, China na Sri Lanka zinazofanya kazi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuhusu utekelezaji wa miradi husika
Na Veronica Simba

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amezitaka Kampuni zilizopewa tenda kusambaza umeme vijijini kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa vinginevyo watanyang’anywa tenda hizo.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma katika Mkutano baina yake na wawakilishi wa Kampuni husika kutoka India, China na Sri Lanka zinazofanya kazi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi pamoja na Mameneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) wa mikoa hiyo na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Profesa Muhongo aliitisha Mkutano huo kwa lengo la kupokea taarifa kutoka kwa Watendaji wa Kampuni hizo kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kabla ya kutembelea miradi hiyo kwa mara nyingine kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara kujiridhisha na maendeleo yake.

Akizungumza katika Mkutano huo mara baada ya kupokea taarifa za utekelezaji kutoka pande zote, Waziri Muhongo alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa REA, Dk. Lutengano Mwakahesya kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unafuatiliwa kwa ukaribu na kusitisha tenda mara moja kwa kampuni zitakazobainika kutotimiza makubaliano ya mkataba walioingia.

“Fuateni utaratibu wa kisheria kwa kutumia vifungu vilivyomo kwenye mkataba vinavyoelekeza kuchukua hatua stahiki kwa kampuni isiyotekeleza wajibu wake ipasavyo,” alisisitiza Muhongo.

Aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha inatimiza ahadi yake ya kuwapatia Watanzania umeme ili wajikwamue katika lindi la umaskini kwa kukuza kipato chao na cha Taifa kwa ujumla hali itakayofanya Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

“Yeyote atakayetukwamisha au kuturudisha nyuma katika kufikia malengo yetu ya kuwaondolea Watanzania umaskini, tutapambana naye na kamwe hatutampa nafasi,” alisema Muhongo.

Vilevile, aliwataka Mameneja na watendaji wengine wa Tanesco kuachana na utamaduni wa kukaa ofisini na kusubiri ripoti za utekelezaji wa miradi badala yake watembelee miradi wanayosimamia na kuhakikisha kazi inafanyika kama inavyotakiwa.

Aidha, Waziri Muhongo aliwataka wakandarasi waliopewa tenda husika kuwa wakweli na waaminifu na kuachana na tamaa hususan wanapopewa kazi ambayo wanajua hawana uwezo wa kuitekeleza ipasavyo ili kuwapa nafasi wengine wenye uwezo huo.

Alisema ni bora kwa Mkandarasi kukubali kazi anayoimudu ili aifanye kwa ubora unaotakiwa na hivyo kujiongezea sifa za kupewa kazi nyingine kuliko kuomba kazi kubwa asiyoweza kuitekeleza kikamilifu na matokeo yake anaharibu na kupoteza sifa ya kufikiriwa kupewa kazi nyingine.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga aliwataka wote wanaohusika na utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo ya kusambaza umeme vijijini kutimiza wajibu wao kwa vitendo.

“Achaneni na maneno maneno, mimi nataka kuona vitendo, nataka kuona matokeo,” alisisitiza na kuongeza kwamba hakuna sababu ya Wakandarasi kusuasua katika utekelezaji wa miradi hiyo kwani walioomba wenyewe wakijinadi kuwa wanaweza.

Naye Kamishna Msaidizi wa Nishati Sehemu ya Umeme, Mhandisi Innocent Luoga aliwataka Wakandarasi hao kujituma na kufanya kazi inavyostahili pasipo kusubiri kufuatwa-fuatwa na kuhimizwa kwa suala ambalo ni wajibu wao.

Wakichangia mawazo katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Edmund Mkwawa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala huo, Dk. Mwakahesya waliahidi kufanya kazi bega kwa bega na wadau mbalimbali wa sekta hiyo ili kuhakikisha Watanzania hususan walioko vijijini wanapatiwa nishati ya umeme kama Serikali ilivyodhamiria na kuahidi.
Posted by MROKI On Monday, September 29, 2014 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo