Nafasi Ya Matangazo

June 20, 2012

MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

Miaka 48 iliyopita, Raisi wa Tanganyika wakati huo, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Raisi wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume; walisaini mkataba ulioitwa Mkataba wa Muungano (Articles of Union) kwa ajili ya kuunganisha nchi zao (Zanzibar & Tanganyika) kuwa nchi moja yenye dola moja.

Mkataba huo ulikuwa mkataba wa Kimataifa (International Treaty) na kila nchi ilipaswa kuridhia mkataba huo katika sheria za nchi husika. Kazi ya kuridhia ni kazi ya Bunge la kila nchi.

Kwa upande wa Tanganyika, tarehe 25 April, 1964, Bunge la Tanganyika liliridhia Mkataba wa Muungano na Bunge la Tanganyika likatunga sheria iliyoitwa Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Namba 22 ya mwaka 1964. Hii ina maanisha kuwa mkataba wa Muungano ni sehemu ya sheria za nchi (Tanganyika) kuanzia tarehe 26 Aprili 1964.

Kwa upande wa Zanzibar, wao hawakuwa na Bunge wala Baraza lolote la Wawakilishi. Baraza la Mapinduzi la Zanzibar ndio lilikuwa likifanya kazi kama Bunge la Zanzibar na Baraza la Mawaziri. Hivyo Mkataba wa Muungano uliridhiwa na kupitishwa na Baraza la Mapinduzi. Isipokuwa kutokana na uzembe au kutokuwa makini kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, tangazo la kuridhia Mkataba wa Muungano haukutolewa katika Gazeti la Serikali (Government Gazette) la Zanzibar. Hivyo Mkataba wa Muungano ulipitishwa na kuthibitishwa na Baraza la Mapinduzi.

Wapo wasomi ambao wamekuwa wakikosoa kuhusu jambo hili, lakini inabidi tukubali kuwa masuala yote ya sheria; Raisi husaidiwa na Mwanasheria Mkuu. Mwanasheria Mkuu ndio mshauri mkuu wa masuala ya sheria kwa serikali, yeye ndiye mwenye jukumu la kubariki kazi zote za Raisi au serikali kabla ya serikali haijafanya hiyo kazi husika. Mfano ni Mwanasheria Mkuu wa serikali na Katibu wa Baraza la Mawaziri ndio wenye jukumu la kuhakikisha kuwa wanapeleka Muswada/Mkataba kuridhiwa na Bunge na kutoa matangazo katika gazeti la serikali (Government Gazette).

Miswada yote inayotoka serikalini kwenda Bungeni husainiwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri.

Muswada ukiwa sheria baada ya Bunge kuupitisha ni Katibu wa Bunge ndiye  wa kwanza kuuthibitisha kuwa Bunge limepitisha muswada husika kuwa sheria.  Na baada ya Katibu wa Bunge (Clerk of the National Assembly) kuusaini inabaki kazi ya Raisi kuusaini (assent) ili sheria ianze kutumika.

Kwa hiyo Zanzibar waliridhia na kuthibitisha Mkataba wa Muungano isipokuwa  kulikuwa na matatizo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kutoa Tangazo katika Gazeti la Serikali baada ya Baraza la Mapinduzi kupitisha Mkataba wa Muungano kuwa sehemu ya sheria za Zanzibar.

Tarehe 27 April, 1964 majira ya saa kumi na moja jioni kulifanyika sherehe kubadilishana nyaraka za Muungano. Muda huo Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume walibadilishana Nyaraka za Muungano mbele ya Bunge la Tanganyika. Na vile vile siku hiyo wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi kutoka Zanzibar waliapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Muungano. Wajumbe hao wa Zanzibar ni Abeid Karume, Kassim Abdallah Hanga, Abdulrahman Babu, Hassan Nassor Moyo , Aboud Jumbe Mwinyi, Hasnu Makame  na Idris Abdul Wakil.

Kwa upande wa Zanzibar, Baraza la Mapinduzi pia lilipitisha na kuikubali sheria ya Muungano (Sheria ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika)) kulingana na taratibu za Zanzibar za wakati huo.

Kifungu cha 4 cha Sheria ya Muungano kinasomeka hivi:-

Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar katika siku ya Muungano (Union day); zitaungana kuwa dola moja na Jamhuri moja na kuitwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa hiyo, siku ambayo Mwl. Nyerere alichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo ilikuwa siku ya Muungano. Siku hiyo waliobeba vibuyu na vyungu ni Mama Sifaeli Shuma ambaye alibeba kibuyu kilichokuwa na udongo wa Tanganyika, Khadija Rajabu Abbas alibeba chungu chenye udongo wa Zanzibar, Omari Hassan Mzee alibeba chungu kilichokuwa na udongo wa Tanganyika na Zanzibar baada ya kuchanganywa.
Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar liliendelea kutumika kwa muda mfupi kwani wengi waliliona kuwa ni refu. Mwezi Desemba 1964; Bunge la Muungano lilitunga Sheria ya kutumia jina Tanzania. Sheria hiyo iliitwa Sheria ya Jamhuri ya Muungano (kutangazwa kwa Jina la Nchi), Namba 61 ya mwaka 1964. Kuanzia Desemba 1964, jina TAN (TANganyika) & ZA (ZAnzibar) NIA (ya kuungana) lilianza kutumika.

Nyaraka za Serikali ya Muungano kabla ya Decemba 1964 zilionyesha jina la nchi kama Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Miradi ambayo Mwalimu Nyerere aliizindua mfano jiwe la Msingi la Jengo la Ushirika lililopo Mtaa wa Lumumba, Ilala, Dar es Salaam linasomeka hivi hadi leo:-

“Jiwe la Msingi limewekwa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mwl. J.K. Nyerere leo tarehe ………….. 1964.


JE, MUUNGANO WA ZANZIBAR NA TANGANYIKA NI WA KIPEKEE HAPA DUNIANI?

Kuna wanasiasa na wasomi wamekuwa wakieleza maneno kuwa dunia hii hakuna Muungano kama huu wa Tanzania yaani  Muungano na serikali mbili; kwamba kuna Muungano wa kubaki na serikali moja au tatu! Jambo hili si la kweli. Wanasiasa na wasomi wanaosema hivyo ni watu wanaohubiri siasa rahisi (cheap politics) na kufundisha wanafunzi wetu taaluma ya kichochezi kabisa.

Ukweli ni kuwa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika unafanana kwa kila hali na Muungano wa Uingereza (England) na Scotland. Muungano wa England na Scotland ulizaa United Kingdom of Great Britain siku ya Mei Mosi 1707 baada ya nchi hizo kusaini Mkataba wa Muungano. (Treaty of the Union between Kingdoms of Scotland and Britain). Mkataba huu unafanana (pari material) na Mkataba wa Muungano (Articles of the Union wa Zanzibar na Tanganyika.

Mambo yanayofanana katika mikataba hiyo miwili ni kuwepo kwa Serikali ya Muungano ambayo pia inashughulikia masuala ya upande mmoja wa Muungano (Tanganyika/Uingereza). Pili nchi ndogo (Zanzibar/Scotland) kuruhusiwa kuwa na serikali yao kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano.

Mkataba wa Muungano wa Scotland na England ulithibitishwa na mabunge yote yaani la Scotland na la England. Mpaka leo hii, huu Muungano upo licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi zinazoukabili.

Changamoto zinazoukabili Muungano wa Scotland na England zinafanana na changamoto za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Ni rai yangu kuwa wasomi na wanasiasa wa Tanzania wanapaswa wajifunze na wafanye utafiti makini kuhusu faida za Muungano kabla hata ya kutoa maoni kuhusu kulazimisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uvunjwe.

Muungano wa Uingereza haukuishia kuunganisha Scotland pekee ila baadae waliungana na Ireland ya Kaskazini (Northern Ireland), na Wales pia. Kwa hiyo hivi leo Uingereza tunayoijua ni Muungano wanchi ambazo ni England, Northern Ireland, Scotland na Wales.

Zile nchi ndogondogo yaani Scotland, Northern Ireland na Wales zina serikali zao hadi leo kwa ajili ya Masuala yasiyokuwa ya Muungano (non- union matters) kama ilivyo kwa Zanzibar. Isipokuwa England yenyewe kama ilivyo Tanzania Bara haina serikali kwa masuala yake yasiyokuwa ya Muungano (non – union matters). Mambo yasiyokuwa ya Muungano ya England yanashughulikiwa na serikali ya Muungano yaani Government of United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland. Pia ikumbukwe kuwa nchi ya Ireland ambayo iko jirani na Uingereza ni tofauti na Northern Ireland.

Northern Ireland mji mkuu wake ni Belfast, Scotland ni Edinburg, Wales mji mkuu wake ni Cardifff. Wakati London ni mji mkuu wa Muungano wa Uingereza yote.

Uingereza ndio taifa la kwanza duniani kuwa na viwanda vikubwa. Pia ni taifa kubwa lenye nguvu za kiuchumi, kijeshi, kisayansi, kiutamaduni na ushawishi wa kisiasa. Sasa jiulize kwa nini lilihitaji Muungano – tunaona maskini hatutaki Muungano – tunaona hauna maana. Tumepoa, tumepotoka!.

Licha ya Muungano huo; Uingereza ni Mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Madola, Halmashauri ya Ulaya (Council of Europe), G7, G8, G20, NATO, OECD, World Trade Organization na Mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).

Kwa hiyo Scotland, Wales na Northern Ireland hazina dola ingawa ni nchi. Nchi yenye dola ni ule Muungano wao yaani United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland. Wasomi wengine huita nchi hii ‘nchi nne ndani ya nchi moja’ yaani four countries within a country.

Mara nyingi watu wanaifahamu nchi hii kwa jina moja tu United Kingdom (UK) au Britain au England lakini hawajui kama nchi hii imeundwa na nchi zilizoungana kama ilivyo Tanzania Bara na Zanzibar. Raia wa Uingereza huwa wengine wanajitambulisha kama Wabritish, Wainglish, Wascottish, Wawelsh au Wanorthern Irish. Kama ilivyo kwa raia wa Tanzania; wengine hujiita Wazanzibar, wapo wanaojiita Watanganyika kama Mch. Christopher Mtikila. Lakini jambo la msingi ni kuwa Pasi yake ya kusafiria inasema Mch. Mtikila ni raia wa Tanzania na siyo raia wa Tanganyika.

Vile vile licha ya Uingereza kuwa ni Muungano wa nchi nne zilizokuwa na dola bali pia Uingereza ni nchi yenye utawala wa kifalme. Uingereza si Jamhuri (Republic) bali ya kifalme (Monarchy).

Ufalme (Monarchy) wa  Uingereza una haki ya kuombwa ushauri na serikali, hali ya kushawishi serikali na wananchi. Pia ufalme una haki ya kuionya serikali/wananchi. Mfalme au Malkia ni Mkuu wa Nchi pia na ndiye anaye (assent) saini sheria ikiishapitishwa na Bunge ili ianze kutumika. Waziri Mkuu wa Uingereza ni mkuu wa serikali. Waziri Mkuu wa Uingereza hapigiwi kura na nchi nzima isipokuwa hutoka kwenye chama chenye wabunge wengi katika Bunge la Makabwela (House of Commons). Uingereza kila kiongozi wa juu wa chama cha siasa huwa anagombea Ubunge na ikatokea chama chake kinapata viti vingi katika Bunge, Kiongozi huyo wa chama chenye wabunge wengi huwa Waziri Mkuu. Waziri Mkuu wa Uingereza na Baraza lote la Mawaziri huteuliwa kiutawala na Ufalme (Monarchy) kuunda serikali ingawaje kiuhalisia ni Waziri Mkuu ndiye anayewachagua mawaziri. Kwa taratibu za Uingereza, ufalme huheshimu wote ambao huteuliwa na Waziri Mkuu.

Mawaziri wote wa Uingereza kutoka katika Bunge la Makabwela ambalo lina wabunge 650 kutoka katika majimbo 650. Uingereza pia ina vyama vikubwa vya siasa vitatu yaani Conservative Party (Chama rafiki na CHADEMA), Labour Party (Chama rafiki na CCM) na Liberal Democrats. Vyama vingine ni vidogo na huwa havishindi viti vya ubunge au wakati mwingine hupata kiti kimoja hivi au viwili kwa bahati. Hata Tanzania vyama vya Siasa vikubwa ni vitatu kwa sasa na vingine huwa wasindikizaji.  Uingereza hakuna viti maalum. Kila anayetaka Ubunge huwa anaenda jimboni kugombea ubunge.

Wales, Northern Ireland na Scotland huwa zina serikali na mabunge yao. Waziri Mkuu wa hizi nchi (Wales, Northern Ireland na Scotland) huitwa First Minister kama ilivyo kwa Zanzibar, Chief Minister na sasa Makamu wa Pili wa Raisi.

Jambo lingine la kuvutia kwa Uingereza ni kuwa, nchi hii ina katiba ambayo haijaandikwa (uncodified constitution) tofauti na Tanzania. Katiba ya Uingereza ambayo haijaandikwa huwa inarekebishwa na Bunge la Uingereza kwa kipengele/taswira ya Katiba ambayo haijaandikwa au imeandikwa.

MUUNGANO WA UINGEREZA UNAVYOFANANA NA MUUNGANO WA TANZANIA

Wales, Northern Ireland na Scotland huwa zina Serikali na mabunge yao. Waziri Mkuu wa hizi nchi (Wales, Northern Ireland na Scotland) huitwa first Minister kama ilivyo kwa Zanzibar Chief Minister na sasa Makamu wa Pili wa Raisi wa Zanzibar.

Ile nchi kubwa ya Uingereza (largest country of United Kingdom) haina serikali yake kama nilivyokwisha fafanua awali bali hutegemea serikali ya Muungano kwa masuala yote ya ndani ya Uingereza kwenyewe.

Pia Bunge la Uingereza lina Baraza la juu zaidi ambalo huitwa Baraza la Mabwanyenye (House of Lords) wajumbe wa Baraza hili huteuliwa kutoka katika viongozi wa dini wa kanisa la Uingereza na wengine huteuliwa na Ufalme kutoka miongoni mwa Waingereza wenye sifa na heshima kwa taifa ambao si wabunge wa Bunge la Makabwela. House of Lords ni wataalamu wa maarifa mbalimbali ambao huchambua sheria zilizopitishwa na House of Commons. Wabunge wa House of Lords hawachaguliwi kwa kupigiwa kura na wananchi lakini hulinda maadili ya Taifa pia na walinzi wa katiba kwani wana uwezo au nguvu (Parliamentary Soreignity) ya kufuta maamuzi ya mahakama na hata masuala ya katiba. Mawaziri wachache sana huteuliwa kutoka katika House of Lords. Kwa sasa House of Lords ina wajumbe 189.

Kuna haja ya Katiba mpya ya Tanzania kuwa na Bunge la Ushauri (Senate) vilevile likiwa na wajumbe ambao ni watu mashuhuri au viongozi wastaafu.
JE, ZANZIBAR ILIBURUZWA KATIKA MUUNGANO?

Si sahihi kabisa kusema katika Muungano Zanzibar iliburuzwa. Viongozi wa Zanzibar, Sheikh Abeid Karume, Mzee Thabit Kombo, Hassan Nassor Moyo, Idris Abdul Wakili, Abdul Jumbe na wengineo hawakuwa viongozi wa kuburuzwa hata kidogo.

Hata uamuzi wa nani awe Raisi wa Muungano ni uamuzi wa Sheikh Karume kwani ndiye aliyemwambia Mwl. Nyerere awe Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukisikiliza hotuba za Sheikh Karume za kati mwaka 1964 na 1969 amerudia sana haya maneno. Naomba ninukuu kama ifuatavyo:-

“Nimemwambia Mwalimu tuungane yeye awe Raisi na Mimi niwe Makamu wake”

Hakuna jambo hata moja ambalo Tanganyika iliiburuza Zanzibar. Kila jambo la Muungano liliamuriwa kwa muafaka wa pande zote mbili. Utaratibu huu unaendelea hadi leo hii. Licha ya elimu ya darasani ndogo aliyokuwa nayo Sheikh Karume lakini alikuwa na busara na mapenzi kwa watu wake kuliko hata wasomi wa leo hii ambao hawana mapenzi kwa taifa lao.

Mfano, Sheikh Karume aliweza kujenga nyumba za makazi kwa wazanzibar ambazo zimetoa malazi kwa zaidi ya familia mia tisa. Nyumba hizi zinatumika mpaka leo.

KWA NINI RAISI WA ZANZIBAR SIYO MAKAMU WA RAISI WA TANZANIA TENA!

Baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa ilionekana hakuna haja ya Raisi wa Zanzibar kuwa Makamu wa Raisi wa Muungano. Kwani iwapo Raisi wa Zanzibar akitoka chama tofauti na Raisi wa Muungano: ingekuwa ngumu kuongoza nchi na hata vikao vya Baraza la Mawaziri. Kwani huyo Makamu wa Raisi (Raisi wa Zanzibar) angeweza kuwa na msimamo tofauti na Raisi wa Tanzania kuhusiana na ilani ya uchaguzi, sera na mtazamo wa kisiasa.

Sababu nyingine ambayo ilipelekea Raisi wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Raisi wa Muungano ni kuzuia madaraka makuu ya nchi (Raisi wa Muungano na Makamu wa Raisi wa Muungano) kwenda kwa upande mmoja wa Muungano iwapo Raisi wa Muungano atakuwa Mzanzibar. Raisi wa Tanzania akiwa Mzanzibar na ikumbukwe kuwa Raisi wa Zanzibar kwa nafasi yake alikuwa anakuwa ni Makamu wa Raisi wa Muungano; basi nafasi za juu za uongozi zingekuwa chini ya upande mmoja wa Muungano.

Ili kuleta usawa katika kugawana madaraka makuu ya nchi katiba ya Muungano ilirekebishwa na Makamu wa Raisi ni mgombea mwenza wa Raisi wa Tanzania na wanatokana na Chama alichotoka mgombea wa uraisi. Iwapo mgombea wa uraisi atatoka upande wa kwanza wa Muungano basi mgombea wa Makamu wa Raisi wa Muungano anapaswa atoke upande wa Pili wa Muungano!

Ikumbukwe pia Raisi wa Muungano (kama anatoka Bara) anapotaka ushauri kuhusu masuala ya Zanzibar; ushauri huu anaupata kwa Raisi wa Zanzibar na siyo kwa Makamu wa Raisi (hata kama makamu wa Raisi anatoka Zanzibar).

KATIBA YA ZANZIBAR.

Tangu mwaka 1963; Zanzibar iliongozwa kwa amri ya Raisi (Presidential Decrees) na Baraza la Mapinduzi. Baraza la Mapinduzi lilikuwa ni Serikali na Bunge kwa wakati huo huo.

Ni mpaka mwaka 1984 ndio Zanzibar ilipata katiba iliyoandikwa katika nyaraka moja na Baraza la Wawakilishi liliundwa na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi/Mawaziri walianza kuteuliwa na Raisi kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

MABADILIKO YA KATIBA YA ZANZIBAR MWAKA 2010 YA KUWEKA NAFASI YA MAKAMU WA PILI WA KWANZA WA RAISI WA ZANZIBAR KUNATAMBULIWA NA KATIBA YA MUUNGANO?

Ibara ya 102 hadi ya 107 (Sura ya Nne) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Katiba ya Zanzibar. Hivyo kisheria inamaanisha kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua Katiba ya Zanzibar na marekebisho yeyote yale yatakayofanyika Katiba ya Zanzibar.



KWANINI HAIRUHUSIWI KUTOA MAONI KATIKA TUME YA KUREJEA KATIBA YA MUUNGANO KWA MASUALA YA MIPAKA YA MUUNGANO?

Ni sahihi kabisa kwa wananchi wa pande zote za Muungano kuzuiwa kujadili mipaka ya kijiografia ya Muungano na kujadili au kupiga kura ya maoni kama Muungano uwepo au usiwepo!

Ni viongozi wendawazimu tu ndio wanaoweza kuwauliza watanzania kama wanataka, Muungano au hawataki! Kiongozi mbaguzi ndiye anayeweza kuhoji mipaka ya kijiografia ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Ni sababu nzuri kuzuia watanzania wasijadili mipaka ya Tanzania bali Muungano uboreshwe.

Ukiruhusu watanzania wajadili na hata kupiga kura ya kuukataa Muungano kwa kisingizio kuwa hawakuulizwa kabla ya kujiunga na Muungano ni uendawazimu na ufinyu wa fikra. Kwani kila mkataba wa kimataifa ambao Tanzania iliusaini/inaousaini ni mwananchi yupi aliulizwa? Mikataba ya kimataifa husainiwa na Raisi wa nchi kwa niaba ya wananchi na nchi bila kupata ruhusa ya moja kwa moja ya wananchi. Hakuna mwananchi ambaye amewahi kupiga kura ya maoni ili kutoa ruhusa kwa serikali kusaini mkataba wa kimataifa. Isipokuwa mikataba hiyo baada ya kusainiwa na Raisi, hujadiliwa na kuridhiwa na Bunge kabla ya kuanza kutumika Tanzania.

Si haki ya Mzanzibar wala ya Mtanzania Bara kuwa alipaswa aulizwe kabla ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume kusaini mkabata wa Muungano ambao ni mkataba wa kimataifa. Hakuna haja ya kuwauliza watanzania kama wanapenda Muungano au la! Iwapo watanzania wataukataa Muungano; kwangu huo utakuwa ni uwazimu. Kwani hata Zanzibar nje ya Muungano; wapemba au waunguja watasema hawakuulizwa kabla ya Pemba na Unguja kuwa Taifa la Wazanzibar.

Hivyo nje ya Muungano; Pemba na Unguja pia lazima zitajitenga: kama Pemba itapiga kura isiwe sehemu ya Zanzibar na Unguja nayo ipige kura ya maoni isiwe sehemu ya Zanzibar; je kutakuwa na hiyo Zanzibar ambayo Uamsho wanaidai!

Kwa Tanzania Bara, vilevile iwapo raia wa Tanzania Bara watapiga kura ya Maoni kujitoa katika Muungano basi tujue madhara na hasara yatakayo patikana baada ya kurudi kwa taifa la Tanganyika ni makubwa kuliko hata changamoto za Muungano. Nje ya Muungano; wasukuma, wagogo, au wanyakyusa watahoji kuwa hawakuulizwa ili wakubali wawe sehemu ya Tanganyika. Na makabila mengine pia yatasema hivyo hivyo na hata watanganyika katika mikoa au kanda watasema wapige kura kwani mkumbuke watanganyika hawajawahi kupiga kura ya maoni kukubali kuwa watanganyika.

Mfano wasukuma au watu wa kanda ya ziwa au hata kabila dogo kama wakerewe wapige kura ya maoni kujitoa katika Tanganyika; Je, kutakuwa na Tanganyika hapo?

VYOMBO VYA HABARI VINAVYOHARIBU MUUNGANO

Televisheni ya Taifa (TBC) inayoendeshwa kwa kodi za Watanzania mwezi Aprili ilirusha kipindi cha This Week Perspective. Mmoja wa wageni waliyoalikwa ni wakili maarufu Harold Sungusia yeye hujitambulisha kama mwanaharakati wa haki za binadamu ila mimi huwa namuona ni shabiki wa Chadema na si mtetezi wa haki za binadamu. Ndg. Sungusia huwa hasifiii mazuri ya CCM, yeye husema mabaya ya CCM tu na mabaya ya Chadema huwa hayasemi kabisa hata kwa bahati mbaya. Ndiyo maana mimi humwona yeye kama shabiki wa Chadema na si mwanaharakati wa haki za binadamu. Mgeni mwingine katika kipindi hicho alikuwa ni Ndg. Hans Kitine. Huyu amewahi kuwa Waziri, Mbunge na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. Baada ya kushindwa ubunge, Ndg. Kitine amekuwa na mawazo hasi kabisa juu ya CCM na serikali yake. Mwendesha kipindi hicho ni mwandishi mkongwe Adam Simbeye. Kipindi cha siku hiyo kilikuwa kinajadili kuhusu miaka 48 ya Muungano wa Tanzania.
Kwanza nilimshangaa Mzee Kitine anayesema Muungano ni mzuri ila wananchi hawakuulizwa kama wanataka Muungano. Alipokuwa serikali mbona hakuuliza hivyo? Yeye kama Mbunge na Waziri alifanya lipi jema kwa Muungano? Baada ya kushindwa ubunge amekuwa akiulaumu CCM na kusema itakufa! Mimi naamini hata yeye Kitine amechangia matatizo ya CCM. Ndg. Kitine amesahau alivyofuja hela za umma kwa matibabu hewa ya mkewe huko Kanada. Kama aliweza kuwa Mkurugenzi wa Idara nyeti kama Usalama wa Taifa na bado hana uwezo hata wa kiintelejensia wa kujua kuwa Zanzibar ikiwa nje ya Muungano itagawanyika katika Upemba na Uunguja! Na Tanganyika ikiwa nje ya Muungano itakawanyika vilevile katika makabila au ukanda!

Hivi Mzee Kitine, Usalama wa Taifa aliongozaje kama hajui kuwa nje ya Muungano; Tanzania Bara nayo itataka ipige kura ya maoni ili Watanganyika wakubali kuwa sehemu ya Tanganyika.

Wewe mzee Kitine unasema Watanganyika hawakuulizwa kuwa watanzania! Je, ni lini basi Wazanzibar waliulizwa kwa kura ya maoni ili wawe wazanzibar? Na ni lini Watanganyika waliulizwa kwa kura ya maoni ili wawe watanganyika?

Mwaka 1964, Mzee Kitine ulikuwepo na upo hadi leo! Mbona hukuomba kura ya maoni? Mawazo ya Mzee Kitine yaliungwa mkono na wageni wengine akiwepo na Ndg. Harold Sungusia na mwendeshaji wa kipindi Ndg. Adam Simbeye.

Namshangaa Harold Sungusia ambaye ni mwanasheria na ninaamini anajua Sheria ya kuondoa utawala wa Machifu, namba 53 ya 1963 (Chiefs Abolition of Office: Consequent) Act. Sheria hii iliondoa utawala wa machifu na kulipa fidia kwa machifu. Na baada ya hapo machifu walitumiwa katika nafasi mbalimbali za uongozi wa nchi kama Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, mabalozi na watumishi katika serikali ya Tanganyika. Je, Sungusia unataka kila kabila la Tanganyika hivi leo tupige kura ya maoni ya kukubali, au kukataa uchifu kwani hakuna kabila lililoulizwa kabla ya machifu kuondolewa!

Mimi napendekeza TBC itafakari sana uwezo wa Simbeye katika kuongoza kipindi hicho. Kama tunataka kulinda maadili ya Taifa basi TBC mjue ni nani anayepaswa aalikwe katika vipindi vyenu ili kuepuka upotoshaji kwa umma.
Hivi Sungusia hujui kuwa mikataba yote ya kimataifa kama ilivyokuwa kwa mkataba wa Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika wananchi huwa hawaulizwi. Isipokuwa Bunge tu kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya Tanzania ndiyo lenye mamlaka ya kuudhibitisha mkataba wa kimataifa ili uanze kutumika katika nchi kama sehemu ya sheria za Tanzania.

Ni lini wewe Sungusia, Simbeye na Kitine mlipiga kura ya maoni kukubali Tanzania ijiunge na Umoja wa Mataifa, SADC, EAC, Comesa, South Commission, AU, WTO, World Bank, IFM, Nchi zisofungamana na upande wowote (Non-Alignment Movement), Jumuiya ya Madola, na nyinginezo?

Hebu acheni ubaguzi. Ukiona mtu anataka watanzania wapige kura ya maoni kuukubali au kuupinga Muungano wetu ujue kuwa huyo mtu ni mbaguzi mkubwa. Tafadhali usimjali na usimsikilize kabisa, mtu huyo ni wa kuogopwa sana.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tarehe 13 Machi 1995 alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika hoteli ya Kilimanjaro alitoa moja kati ya hotuba zake kali alizozitoa mwishoni kabisa ya maisha yake na mimi huichukulia hotuba hii kama wosia. Mwalimu alisema hivi na hapa namnukuu:-

“Kwangu Muungano (Tanzania) ni muhimu kuliko jambo lolote….. nje ya Muungano wazanzibar mtajikuta kuna wazanzibar na wazanzibara … nje ya Muungano wa Tanganyika mtaongelea ukabila….Hamwezi mkakaa salama baada ya kutenda dhambi ya kuwabagua watu wa nchi yenu ile ile moja mkawaita wale ‘wao’ na hao ‘sisi’. Dhambi ile ya ubaguzi haiishii hapo. …….Huwezi kufanya ubaguzi wa namna hiyo halafu dhambi ile ikuache hapo hapo…….hiyo dhambi itakuandama tu…..Mkipate Boris Yelstin wenu hapa atawetenganisha.”

Licha ya hotuba hii nzuri ya Mwalimu bado wazee wangu Simbeye na Kitine, hawaelewi Muungano. Nguli Sungusia naye vilevile. Nawashangaa watu hawa wanakuwa na mawazo kama ya kikundi cha kibaguzi cha Uamsho.

Hata gazeti la Mwananchi limekuwa likichochea Muungano uvunjwe. Gazeti hili linamilikiwa na wanahisa kutoka nchi jirani ya Kenya. Hivi nyinyi watu wa Mwananchi mbona hamjaenda Kenya kusema kilomita 25–50/maili 16–31 ya pwani ya Kenya (Mombasa na Lamu) zijitenge na Kenya na ziwe sehemu ya Zanzibar. Kwani wakati wa utawala wa Sultani wa Zanzibar zilikuwa sehemu ya Zanzibar.

Nawaonya wanaharakati na waandishi wa Tanzania. Jiangalieni yasije yakawapata kama yaliyompata Arap Sang. Arap Sang alishangaa sana jina lake lilipotajwa kuwa mmoja wa watuhumiwa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Wakati mwandishi wa habari anavunja sheria anaweza asijue kama anavunja sheria lakini kutokujua sheria si utetezi.

Ni lazima watanzania tujifunze kuheshimu mipaka iliyowekwa na wakoloni na mipaka iliyowekwa na Muungano. Historia lazima isonge mbele, tupende tusipende. Haya ndio mabadiliko ambayo watanzania tunapaswa tuyafuate. Asiyekubali mabadiliko haya, mabadiliko yatambadili mpaka atakapokubali kubadilika.

WANASHERIA WAACHE KUCHOCHEA KUUA MUUNGANO.

Wanasheria wenzangu tusiwadanganye watu kwa kutaka umaarufu. Si kweli kuwa kila jambo muhimu la nchi lazima kura ya maoni ipigwe ili kuamua nini kifanyike. Ikiwa kura ya maoni ni yakupigwa kila mara, basi kila mwezi na kila wiki tunaweza tukawa na kura ya maoni kwa vile yako mambo mengi ya nchi yakuyapigia kura.

Siyo kila jambo ni lazima kwa watanzania au wananchi watoe maoni yao. Yako masuala hayaitaji maoni ya wananchi labda tu kama maoni hayo ni ya kuyaboresha.

WANAHARAKATI WA KUDAI UZANZIBAR.

Ninyi mnaojiita wanaharakati wa kudai Uzanzibar nje ya Muungano na utanganyika nje ya Muungano. Mbona hamuwaulizi wazazi wenu kwanini hawakuwauliza KAMA MNATAKA kuzaliwa kabla ya kuwaleta duniani?

Ni kwa nini hamjahoji kwanini umezaliwa mzanzibar, mchaga au mrangi? Muungano ndio asili yetu anayeukashifu sidhani kama akili zake ziko sawa. Msomi Harold Sungusia anasema …… ‘miaka 48 ya Muungano haina kitu’. Na kuongeza kuwa …. ‘Muungano ni kama binadamu mwenye magonjwa mengi’. Sungusia alikejeli pia na kusema Muungano ni kama mwanamke aliyejichubua na dawa haramu za kutoa weusi katika ngozi (mkorogo). Sikubaliani na mifano mfu anayoitumia “mwanaharakati” huyu.

Mimi hupenda kuufananisha Muungano na ndoa. Ingawaji wanasiasa wengi hawapendi mfano huu ila mimi lazima niutumie ili masikio yenu yasikie na akili zenu zielewe maana ya Muungano.

Ndoa ni Muungano wa hiari wa mwanamke na mwanaume ambao wanategemea kuishi kwa maisha yao yote kwa mujibu wa Kifungu cha 9 Cha Sheria ya Ndoa ya Tanzania, Namba 5 ya 1971.

Kwa hiyo Muungano lazima uwe wa maisha yote; ikitokea unafunga ndoa ni lazima iwe kwa maisha yote. Talaka ni bahati mbaya katika ndoa kwani saa ya kuungana hakuna anayepaswa kuwaza talaka. Muungano pia ni hiari – hiari ya nchi na si hiari ya wananchi. Maslahi ya kila mwananchi ni tofauti na maslahi ya nchi. Nchi kwanza mwananchi baadaye. Hata ndoa ni Muungano wa hiari-hiari ya mwanamke na mwanaume, siyo hiari ya wazazi, ndugu, marafiki, majirani, miiko, mila au hata dini.

Muungano kama ilivyo ndoa, hakuna ndoa hata moja isiyokuwa na matatizo au changamoto. Jambo la msingi katika ndoa ni kukabiliana na changamoto za ndoa bila kuumiza upande wowote ule.

Tusidanganyike Watanzania kuwa upo Muungano duniani ambao hauna matatizo. Na hata nje Muungano, matatizo ya Zanzibar au Tanganiyika yatakuwa mengi kuliko hata kero za Muungano. Kero za Muungano zinaweza kutatuliwa hata kero hizo zikiisha nyingine mpya zitafuata.

KWANINI UPANDE FULANI WA MUUNGANO UNANUFAIKA NA MWINGINE HAUNUFAIKI?

Ukiwauliza baadhi ya Wazanzibar watakuambia Zanzibar inanyonywa na Tanzania Bara. Watasema Zanzibar ilipoteza kiti chake UNO! Zanzibar haina ubalozi nje ya nchi! Zanzibar haina dola, Zanzibar inapewa mapato kidogo ya Muungano, Zanzibar haipewi nafasi za kutosha katika serikali ya Muungano, Wazanzibar wananyanyaswa, wazanzibar hawakushirikishwa katika kujiunga na Afrika Mashariki, Zanzibar imezuiwa kujiunga na OIC. Vilevile wazanzibar hao husema Zanzibar inazuiwa isiwe na wimbo wake wa Taifa na mengine mengi ni madai ya kibaguzi ya kudai Zanzibar ijitoe katika Muungano.
Kama nilivyoeleza katika ndoa. Si kila mwanandoa atanufaika kwa kiwango sawa sawa na mwenzie. Hebu firikiria ndoa ambayo mwenzi mmoja anatoka katika familia tajiri na mwenzi mwingine anatoka katika familia fukara. Ni dhahiri mwenzi anayetoka katika familia fukara atafaidi zaidi kiuchumi kwa kuwa na mwenzi anayetoka katika familia tajiri. Na mwenzi anayetoka katika familia tajiri hawezi kunufaika kiuchumi kutoka kwa mwenzi wake anayetoka katika familia duni. Hata mwenzi mwenye kipato kidogo atafaidi zaidi iwapo mwenzi wake atakuwa na kipato kikubwa.

Kwenye ndoa kuna mwingine lazima abebe mimba na mwingine habebi mimba. Kuna anayenyonyesha na mwingine hanyonyeshi. Sasa katika Muungano au ndoa kila upande ukitaka uwe sawasawa kimajukumu na kimaslahi itawezekana kweli; haiwezekani kabisa.
IDADI YA MAJIMBO YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR

Hadi leo hii, Wazanzibar wapo Milioni Moja (1,000,000) lakini wana majimbo hamsini ya ubunge wa Muungano wakati wilaya ya Kinondoni ina wakazi Milioni Moja na Laki Tisa (1,900,000) lakini ina majimbo matatu ya uchaguzi! Je ni nani anayefaidi kutokana na Muungano hapa!? Nashangaa wazanzibar kusema wananyonywa na Muungano.

MGAWANYO WA MAPATO YA MUUNGANO KWA IDADI YA WATU

Tunaweza kuchukua uwiano wa idadi ya watu katika kugawana mapato ya Muungano. Katika mapato ya Muungano, Zanzibar inapewa 4% ya mapato ya Muungano na Tanzania Bara inachukua 96% ila ikumbukwe kuwa Wazinzibar ni asilimia 2.5% ya Watanzania. Lakini bado Zanzinar inasema kuwa 4% ya mapato ya Muungano haiwatoshi!

MAMBO AMBAYO ZANZIBAR IMENUFAIKA NAYO KATIKA MUUNGANO

Ulinzi na amani umeimarika Zanzibar kwani baada ya mapinduzi ya Zanzibar, wengi waliamini Zanzibar ingepinduliwa kama nchi nyingi za Afrika ambazo zilikuwa na Mapinduzi kwa wakati huo.

Zanzibar inashiriki vizuri katika masuala ya Muungano. Zanzibar ina wabunge hamsini wa majimbo katika Bunge la Muungano licha ya Zanzibar kuwa na wananchi karibu 1,000,000. Wilaya ya Kinondoni ina wakazi 1,900,000 lakini ina wabunge watatu katika Bunge la Muungano.

Wafanyabiashara wengi wa Zanzibar wamejenga nyumba za makazi, nyumba za biashara na kuwekeza biashara zao katika ardhi ya Tanzania. Fursa hii wasingeipata kwa Zanzibar kwani Zanzibar ina soko dogo yaani watu milioni moja tu!

Zaidi ya Wazanzibar laki tatu huishi na kufanyakazi katika ardhi ya Tanzania Bara. Biashara nyingi na kubwa za Zanzibar zimewekezwa Tanzania bara na faida ya biashara hizo hurejeshwa nyumbani Zanzibar.

Ikumbukwe kuwa Mzanzibar anaruhusiwa kumiliki ardhi bara, kugombea ubunge/udiwani wa jimbo la Tanzania Bara. Lakini Mtanzania wa Tanzania Bara haruhusiwi kumiliki ardhi Zanzibar na haruhusiwi kugombea ubunge/ udiwani huko Zanzibar. Hii ni faida ya aina yake ambayo Zanzibar inaipata katika Muungano.

Zanzibar imeweza kupata mapato kutokana na mapato ya Muungano ambayo husaidia kuendesha serikali na kuleta maendeleo ya Zanzibar.

Zanzibar pia imekuwa inachangia pato la Muungano mfano makusanyo ya kodi kwa mwaka 2009/10 Zanzibar ilikusanya kodi ya mapato Shilingi Bilioni 1 na Tanzania Bara kwa kipindi hicho ilikusanya Shilingi Bilioni 1,498 sawa na asilimia 99.93% ya makusanyo yote ya kodi za Muungano. Lakini katika kugawana, licha ya Zanzibar kukusanya chini ya 1% ila hupewa 4%.

Yapo maendeleo mengi ya kiuchumi kisiasa na kiutamaduni ambayo Zanzibar inanufaika na Muungano.

KWA NINI TANGANYIKA NA ZANZIBAR ZILICHUKUA MFUMO WA SERIKALI MBILI BAADA YA MFUMO WA SERIKALI TATU AU MOJA?

Ili kulinda utamaduni na mapokeo ya Zanzibar ilionekana ni busara sana kwa serikali ya Zanzibar ibaki ikiwa na nguvu ya kuendesha mambo machache kwa ajili ya Wazanzibar.

Hivyo basi busara ilionesha serikali ya Tanganyika iondoke na Tanganyika na Tanzania zitatumia serikali ya Muungano kwa masuala yote.

Hakuna shaka kuwa hata mifano ya Uingereza ilizingatiwa katika Muungano huu wa Tanzania.

Mfumo wa serikali tatu ulionekana utaleta gharama kubwa katika uendeshaji. Mfano serikali tatu zingeleta mabunge matatu, serikali tatu na Taasisi tatu hata kwa masuala machache tu. Muungano wa serikali tatu pia si Muungano moja kwa moja.

Kwa kawaida sheria zote za Tanzania hutungwa si tu kwa kuzingatia katiba ya nchi bali hata kwa kuzingatia mila, desturi na maadili ya Tanzania. Inajulikana kuwa Zanzibar ni nchi tangu Sultan wa Omani alipoingia Zanzibar mwaka 1698 hivyo isingekuwa busara serikali ya Zanzibar kuondoka kama ya Tanganyika.
Utaifa wa Zanzibar tayari ulikuwa umeenea na kukuza biashara na watu wengi wa nje. Kwa sababu za kuvutia utalii ilikuwa bora kwa serikali hiyo kubaki.

Kihistoria ilionekana ni vema serikali ya Zanzibar ibaki ili kuweka sawa historia kwa kuihifadhi na kuifundisha kwa vizazi hadi vizazi na kuwafundisha wageni na watalii pia.

Ilionekana ni vema kwa Zanzibar iwe na serikali yake kwa ajili ya masuala machache yasiyokuwa ya Muungano hadi leo hii Zanzibar ni nchi isiyokuwa na dola na isiyokuwa na mamlaka kamili. Zanzibar ina mamlaka yote isipokuwa masuala 22 ambayo yametajwa katika jedwali la kwanza la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

KWA NINI ZANZIBAR NA TANGANYIKA ZILIUNGANA?

Zanzibar na Tanganyika ziliungana na kuwa dola moja na Taifa moja. Historia ya mataifa haya zinafanana. Karibu 40% ya Wazanzibar asili yao ni Tanganyika. Watanganyika walioenda kuuzwa katika soko la watumwa pale Zanzibar na kwa bahati hawakununuliwa kutokana na kutokuwa na nguvu au kwa sababu yeyote ile walibaki Zanzibar na hawakurudishwa Tanzania Bara. Watumwa walipotoka Bara na kufikishiwa soko la watumwa Zanzibar walionunuliwa ni wale wenye nguvu na afya na ambao hawakununuliwa walibaki Zanzibar kama watu huru na hawakurudishwa makwao huko Bara. Historia ndio ambayo hufanya watu kuwatania Wazanzibar kuwa ni wavivu! Ndio maana kazi au mzigo ukiwa mzito; wazanzibar husema mzigo mzito mbebeshe mnyamwezi (kwa Kiswahili cha Zanzibar: mnyamwezi ni jina linalotumika kumaanisha mtu wa kutoka Bara). Hata hivyo mimi siamini kuwa wazanzibar ni wavivu. Kila kabila lina watu wavivu. Pia naona biashara za Wazanzibar hata zilizoko hapa Bara zimeendelea kukua siku hadi siku. Sasa kama ni wavivu wangeendelezaje biashara zao kwa kasi kubwa namna hii!

Jamii ya watu weusi karibu wote wa Zanzibar walitoka Tanzania Bara. Ndio maana ya kuwa na Wazanzibar wenye majina ya Kisukuma, Kinyamwezi, Kinyakyusa na majina ya makabila mengine ya Bara. Mfano ni Marehemu Adam Mwakanjuki, Jaji Othman Makungu, majina kama Bundala, Shija na mengineyo.

Ilionekana ili kuweza kulinda mipaka ya baharini ya Zanzibar na Tanganyika ni vema kwa nchi nizi kuungana na kuwa na jeshi imara la umoja la kulinda mipaka ya nchi hizi. Kutokana na machafuko yaliyofanywa na USA katika kisiwa cha Cuba kati ya mwaka 1955 hadi 1958 baada ya Fidel Castrol kuipindua Cuba. Zanzibar ilionekana ni kisiwa ambacho kingeweza wavamiwa na mabeberu wa magharibi na kwa namna yeyote ile wangeathiri uhuru si tu wa Zanzibar bali hata Tanganyika na Afrika yote. Hata watu wa magharibi walidhani Zanzibar itakuwa kama Cuba hivyo nao walitaka kuiangalia na kuidhibiti.

Mawazo ya kizalendo ya kiafrika yaliwasukuma waasisi wa Muungano na kuona ni vizuri kuunganisha Zanzibar na Tanganyika. Busara hiyo ilitegemea kuwa nchi nyingine za Afrika nazo sitaungana kikanda (regional cooperation) na baadaye kuwa na taifa moja la Afrika. Zanzibar na Tanganyika ndio zitakuwa mfano wa kuigwa. Na kwa kweli mpaka leo hii Muungano huu ni wa mfano kwa bara zima la Afrika.

MGAWANYO WA MADARAKA NA NAFASI KATIKA MUUNGANO

Baada ya Muungano nafasi zote za Muungano ziligawanywa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Sheria ya Muungano ilimfanya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Kwanza wa Raisi wa Muungano na Raisi wa Zanzibar alikuwa anakuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Muungano.

Bunge la Muungano lilipokea wabunge kutoka Zanzibar na nafasi zote za Muungano ziligawanywa kwa usawa kutoka pande zote za Muungano.

KIKUNDI CHA UAMSHO NA KUPINGA MUUNGANO

Matukio ya mwishoni mwa Mei 2012 Jijini Zanzibar, mkoani Mjini Magharibi, Unguja.  Kama tujuavyo sote kulitokea ghasia zilizochochewa na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu maarufu kwa jina la Uamsho.  Taasisi hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi sasa viongozi wake wameamua kuyaacha madhumuni hayo na kubeba ajenda za siasa. Matukio haya pia hayajaanza mwaka huu, yapo muda mrefu ila chini chini na yanaendeshwa na watu pia wanafundishwa jinsi ya kupigana na vyombo vya dola na wale wote wenye mapenzi mema na Tanzania.

Siku za nyuma, hawa viongozi wa kundi hili, wakitumia muda mwingi kuilaumu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki.  Lakini, mara tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na kuwakashifu viongozi waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa.  Isitoshe wamekuwa wakipandikiza chuki dhidi ya ndugu zao wa kutoka Tanzania Bara na wale wafuasi wa dini ya Kikristo.

Baya zaidi, katika uchochezi huo majengo na mali za Makanisa mawili  zilichomwa moto, maduka ya watu kuvunjwa na mali zao kuibiwa.  Kwa kweli vitendo hivi ni uhalifu ambao haukubaliki na wala hauvumiliki.  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kauli yake alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari ya kukemea vikali na kulaani uhalifu huo. 


Ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwamba, wenzetu hawa wamefanya uhalifu huo kwa hoja ya kupinga Muungano.  Haiwezekani mtu anayepinga Muungano, akaitetea hoja yake kwa kuchoma moto makanisa au kuvunja maduka ya watu na kupora mali zao.   Ukristo haukuingizwa Zanzibar na Muungano, bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya Muungano na wala haukutokea Tanzania Bara. Na kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais Ali Mohamed Shein jana, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar.  Kanisa kuu la Anglikan Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia 1893 ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa upande wa Afrika Mashariki si Zanzibar na Tanzania Bara tu. 

Katika hotuba yake ya kuwalaumu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Ali Mohamed Shein, pamoja na kueleza kwa ufasaha ukweli huu, pia alisisitiza suala la haki na uhuru wa Kikatiba wa mtu kuchagua au kubadilisha dini au imani yake (Ibara ya 19 ya Katiba ya Zanzibar na Ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano). Katika kutumia uhuru huo, mtu hastahili kuingiliwa au kulazimishwa na mtu yo yote. Hayo pia ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Kwa kweli yanayofanywa na ndugu zetu wa Uamsho ya kuchoma moto makanisa siyo sawa hata kidogo.  Na, wanapoyafanya kwa kisingizio cha Muungano ni jambo lisiloeleweka kabisa na wala halina mantiki.  Labda wenzetu wana lao jambo ambalo ni kuleta chuki za kidini. Wapo baadhi ya viongozi wa kundi hilo wamekuwa wakisafiri nchi nzima, bara na visiwani kuhamasisha waumini wa uislamu kudai taifa hili liwe la kiislamu. Katika mafundisho yao ambayo nimepata kuiona nakala ya mafundisho yao katika CD; Mkufunzi huyo amesema kuwa wako tayari kufa au kuuwa ili mradi tu nchi hii iwe ya kiislamu. Mkufunzi huyo amesema kuwa; kufa kutawapeleka mbinguni na kuuwa kutawapeleka mbinguni. 

Jambo lingine la kushangaza zaidi ni kule kutokea vurugu na ghasia hizi dhidi ya Muungano wakati ambapo Serikali imetoa fursa sasa kwa watu kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.  Kama tujuavyo sote, Tume ya Katiba imekwishaundwa na inajiandaa kupita kote nchini kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya waitakayo.  Kama mtu ana maoni yake kuhusu Muungano, hiyo si ndiyo fursa ya kufanya hivyo.  Utaratibu mzuri umewekwa kwa ajili yetu sote, vurugu za nini? Ubaguzi wa kidini wa nini?

Mimi sioni sababu ya msingi ya kusababisha kuvurugika kwa  amani kwa jambo ambalo limewekewa utaratibu muafaka wa kulishughulikia. Nawaomba tutumie utaratibu mzuri uliowekwa badala ya kufanya mambo yanayoleta mifarakano katika jamii na yanayosababisha uvunjifu wa amani na kuharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania.   

Serikali lazima ifanye na isisite kuchukua hatua kali dhidi ya watu hawa wahuni wa uamsho.  Watanzania wajiepushe na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha mifarakano baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina ya Wakristo na Waislamu.

Uamsho wamesema Zanzibar inanyonywa katika Muungano. Labda niulize!? Zanzibar ina wananchi Milioni Moja tu lakini ina majimbo 50 katika Bunge la Muungano wakati wilaya yangu ya kinondoni ina wakazi Milioni Moja na laki tisa ila ina majimbo matatu tu katika bunge la Muungano. Je ni nani anaemnyonya mwenzie?

Nauliza tena, Wazanzibar wanaruhusiwa kugombea ubunge jimbo lolote Tanzania Bara na pia wanaruhusiwa kumiliki ardhi Tanzania Bara lakini mtanzania bara haruhusiwi kugombea ubunge wala kumiliki ardhi Zanzibar. Je ni nani anaemnyonya mwenzie?

Ikumbukwe kuwa watanzania ni ndugu na wamekuwa wakiishi pamoja kwa upendo na furaha licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini na maeneo watokako. Kimeharibika kipi hata leo yatokee haya? Naamini kuwa wapo baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa ambao wamechochea harakati za Uamsho. Uamsho kama yalivyo makundi haramu kote duniani yana mkono wa wanasiasa. Siwezi amini tofauti na hivyo. Kama kundi haramu la Mungiki pale Kenya na Uamsho ni hivyo hivyo.

Wenye maoni kuhusu Muungano wetu, muundo wake na uendeshaji wake watumie fursa ya mjadala wa Katiba kutoa maoni yao.  Hatuhitaji kufanya ghasia kutoa maoni kuhusu Katiba.


Hali kadhaliak nawapongeza vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwa juhudi kubwa waliyoifanya ya kudhibiti hali ambayo mwelekeo wake haukuwa mwema.  Nawaomba waendelee kuwa macho ili watu wasioitakia mema nchi yetu na watu wake wasipate nafasi ya kutuvurugia amani na utulivu wetu.  Naamini tukidumisha utamaduni wetu wa kuheshimiana, kuvumiliana, kuzungumza pale tunapotofautiana na hata kukubali kutokukubaliana hakuna litakaloharibika. Haya shime tufanye hayo.

MAPENDEKEZO YANGU KUHUSU UAMSHO

Ninapendekeza kuwa Kikundi hiki cha Uamsho kifutiwe usajili na kifungwe, kwani kama walisajiliwa kufanya shughuli za kidini, imekuaje wakaanza kufanya mihadhara ya masuala ya siasa?

Kundi lolote lile au mtu yeyote yule anaye kashfu viongozi waasisi wa taifa letu na viongozi waliopo madarakani washtakiwe mara moja.

Wananchi waelimishwe kuhusu faida za Muungano na vikundi vinavyochochea udini vifungwe na Serikali.

Uamsho wametoa CD zenye matusi ya kukashifu wakristu, Serikali iwashitaki kwa kosa la kuingilia uhuru wa dini nyingine.

Serikali ihakikishe usalama wa mali na maisha ya wananchi. Waandishi wa habari waache kuandika habari za Uamsho. Viongozi wa Uamsho wakiitisha mikutano na waandishi wa habari, ndugu wana habari msiende. Tafadhari sana. Nyinyi waandishi wa habari mnapoenda kuwasikiliza wale wendawazimu na wabaguzi wakubwa mnakuwa mnawapa nguvu ya kuendelea kubagua na kuleta fujo. Ndugu wanahabari, jiangalieni msije mkawa kama Arap Sang wa Kenya. Arap Sang alikuwa akitangaza tu habari za kibaguzi kama alivyozipokea kutoka kwa wabaguzi na wafanya fujo. Kitendo hicho kimempeleka the Hague.

Nanyi wanahabari wa Tanzania hakika nawaambieni, ipo siku mtapelekwa the Hague wakati Uamsho watakapopelekwa pia. Mtabaki mnazubaa kama Arap Sang mkiulizana. Mbona mimi ni mwanahabari na sikushika silaha kuuwa? Bali niliandika yaliyokuwa yakitokea tu?

Katika kuandika habari, mwana habari hauruhusiwi kuandika habari za uchochezi au za kibaguzi. Hotuba zote za Uamsho ni za kibaguzi. Inakuwaje sasa wanahabari mnaziandika. Mimi naomba niwalaumu na nyinyi pia kwa kutumia muda mrefu kuwahoji viongozi wa Uamsho na wafuasi wake bila kupata hata dakika moja tu ya kutuhoji sisi waumini wa Muungano au kuhoji watu wenye dhamana ya kuulinda Muungano.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ubariki Muungano.

 
MGOMO WA MADAKTARI TANZANIA

MADA
Januari 24, 2012 madaktari zaidi ya 1,000 waligoma karibu nchi nzima. Mgomo huo uliendelea hadi 09 Februari 2012 mara baada ya Waziri Mkuu kukutana na madaktari na wahudumu wa sekta ya afya.

Hata hivyo, 28 Januari 2012, TUCTA (Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania) walitangaza kuwa mgomo wa madaktari ni batili, kinyume na sheria na hauna maslahi kwa taifa.

29 Januari 2012, Waziri Mkuu aliomba kukutana na madaktari katika ukumbi wa Karimjee lakini madaktari waligoma kuja katika kikao wakasema wanawasubiri wenzao watoke mikoani.

Vilevile siku ya tarehe 09 Februari 2012, Waziri Mkuu alitangaza kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Blandina Nyoni, na Mganga Mkuu wa Serikali, Dr. Deo Mtasiwa.

Waziri Mkuu pia aliunda kamati ya pamoja ya watu tisa ikiwa na wahudumu wa sekta ya afya na wawakilishi wa serikali ili kupitia madai ya madaktari na kuishauri serikali nini kifanyike kwa ajili ya madai hayo.

Machi 07, 2012 kulitokea mgomo mwingine ambao madaktari walitoa masaa sabini na mbili (72) kwa serikali iwe imewafuta kazi Waziri wa Afya na Naibu wake.

Migomo yoye hii iliathiri sekta ya afya kwa kiwango kikubwa sana.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipeleka kesi katika Mahakama ya Kazi na kuwashitaki madaktari kwa kuitisha mgomo haramu. Madaktari walikataa kwenda mahakamani wala kupeleka wakili wao. Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi ili tamka kuwa mgomo wa madaktari ni haramu; madaktari waliamrishwa kurudi kazini na vilevile kukaa katika meza ya majadiliano na serikali kuhusu maslahi yao.

Baada ya madaktari kuongea na Mhe. Raisi mgomo ulisitishwa na madaktari walirudi kazini.

Madakatari na wafanyakazi wote wa sekta ya afya walikuwa katika meza ya pamoja na serikali ambapo masuala ya masalahi ya madakatari yalikuwa yakishughulikiwa.

Juni 9, 2012 madaktari walikutana tena na kuazimia kugoma nchi nzima katika mgomo ambao wao wenyewe wamesema utaleta madhara makubwa sana kwa taifa. Ina maana lengo lao ni kuleta madhara kwa taifa, na madhara hayo si ukosefu wa huduma za afya tu bali hata vifo vya watu wasiokuwa na hatia.

Ibara ya 14 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 inasema hivi:-
‘Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria’

Hivyo daktari akigoma, na mgonjwa akifariki dunia; maana yake ni kuwa mgonjwa amenyimwa haki ya kuishi na daktari.

Ibara ya 22 hadi ya 24 ya katiba yetu inatoa haki kwa kila mtu (daktari) kufanya kazi na kulipwa ujira unaostahili kulingana na kazi anazozifanya au kulipwa malipo ya haki kwa kazi alizozifanya.

Lakini bado haki ya kuishi ndio haki kuu kuliko haki zote kwani atakaye kufa kutokana na daktari kugoma ni mhasibu, daktari, mwalimu, wazazi wa daktari, nduguze daktari, marafiki wa madaktari, na wengineo. Mgomo wa madaktari unawathiri madaktari wenyewe pia na unashusha hadhi ya daktari katika jamii. Jamii itamuona daktari ni mtu anayejari maslahi yake binafsi bila kujali wajibu wake kwa wagonjwa na jamii kwa ujumla. Afya ya mtu si jambo la mjadala.

Ukosefu wa mazingira mazuri ya kufanyia kazi siyo sababu ya kuhalalisha mgomo. Naomba niwape mfano wa mawakili wa serikali. Utakuta wakili wa serikali anaendesha kesi inayohusu uingizaji wa madawa ya kulevya yenye dhamani ya zaidi ya mabilion lakini anapanda daladala na anaishi uswahilini, nyumba ya kupanga. Zipo kesi nzito sana za ujambazi wa kutumia silaha za kivita ambapo watuhumiwa wameiba zaidi ya mabilioni lakini wakili wa serikali anayeendesha kesi hiyo hadai alipwe zaidi ya kile kilichopo.
Mimi mwenyewe niliishawahi kupewa kazi na serikali ya kuwatetea watuhimiwa wa kesi za mauaji kwa malipo ya shilingi elfu sitini tu. Ukihesabu siku ambazo nilikwenda Gerezani kuongea na mtuhumiwa, gharama za usafiri za kwenda gerezani, gharama zangu za kiofisi, gharama za kwenda mahakamani tangu kesi ilipoanza hadi ilipoisha. Utagundua kuwa elfu sitini haikuwa hela iliyonistahili hata kwa kufuata Ibara ya 22 na 23 ya Katiba kama nilivyotaja hapo juu.

Na hela yenyewe serikali walinilipa baada ya miezi 5 baada ya kesi kuisha. Kwa hiyo tangia mwanzo mwa kesi hadi mwisho nilikuwa natumia pesa yangu ya mfukoni. Ukumbuke mimi ni wakili wa kujitegemea. Kesi hiyo ilikuwa kesi ya mauaji namba 11 ya mwaka 2006: Jamhuri dhidi ya Thomas Anthony Mahiringa (mbele ya Jaji Madam Beatrice Mutungi).

Ni utaratibu wa serikali kuteua wakili wa kujitegea ili amtetea mtuhumiwa wa kesi ya mauaji pale ambapo mtuhumiwa wa kesi ya mauaji hana uwezo wa kuweka wakili wa kumtetea. Katika kesi hii ambayo, mtuhimiwa huyo nilimtetea vizuri, bila kunung’unika, bila kinyongo na nilikuwa simfahamu hata yeye alikuwa haamini, nilimtetea hadi akashinda. Alikutwa na hatia ya kuuuwa bila kukusudia na akapewa kifungo cha miezi sita nje ya gereza na alionywa asitende kosa lolote la jinai ndani ya ile miezi sita.

Hivyo mteja wangu huyu ambaye alikuwa amekaa jela pale Ukonga kwa zaidi ya miaka saba, siku hiyo aliachiwa huru. Hata ukiwa daktari utatibu wagonjwa usiowajua ila watibu hadi wao washangae jinsi unavyowajali.

Ipo kesi nyingine ya mauaji nayo nilishinda. Jamhuri dhidi ya GM (hataki jina lake lijulikane) kesi ya mauaji namba 30 ya mwaka 2007 (mbele ya Jaji Emilian Mushi). Nayo niliipata kwa utaratibu huo huo na nikashinda pia. Mtuhumiwa hakuwa ndugu yangu wala rafiki yangu. Ila kwangu mimi WATANZANIA KWANZA, MASLAHI YANGU BAADAE.

Mimi kama wakili nina haki ya kugoma ili serikali iongeze malipo ambayo sisi mawakili wa kujitegemea tunalipwa na serikali tunapowatetea watuhumiwa wa mauaji. Lakini siwezi fanya hivyo sababu hoja yangu haina maslahi kwa taifa. Wakili anapogoma anayeumia ni mtuhumiwa na si serikali. MADAKTARI WANAPOGOMA ANAYEUMIA SI SERIKALI BALI NI WAGONJWA.

 NA WAGONJWA NI NDUGU ZETU WOTE NA NDUGU ZA MADAKTARI. Ukitaka kuigomea serikali acha kazi za serikalini kaajiriwe kwingine unakoona kuna maslahi mazuri. Hivi kweli hao madaktari wanaotaka kugoma, wakigoma halafu wazazi wao au wake zao au waume zao wakiugua hawataenda kuwatibu? Au wanagoma ili wafe watu wengine wasiokuwa ndugu zao?

Ukweli unauma ila lazima niwaambie ndugu zangu madaktari. Mimi nimebahatika sana kwani familia yetu ina madaktari wengi sana.  Baba yangu, Baba zangu wakubwa na baba zangu wadogo, madada, kaka zangu na hata mke wangu naye ni daktari pia. Dada yangu mmoja ambaye ni daktari aliwahi kutania siku moja tulikuwa na sherehe ya familia nakusema yafuatayo:-

‘Ukoo huu unanishangaza, yani hata wale waliosoma kozi za zisizokuwa za sayansi, huwa wanafaulu somo la biolojia. Nadhani kila mtu katika nyumba hii, alipaswa awe daktari’
Nakumbuka baba yangu kabla hajastaafu alikuwa akitibu wagonjwa muda wote. Nyumba tuliyokuwa tukiishi ilikuwa jirani na hospitali. Kila mara usiku, walinzi wa hospital walikuwa wakija kumuamsha pale ambapo walikuwa wanapata wagonjwa waliyoitaji ujuzi wake. Na hata siku moja sikuwai msikia akikataa kwenda kutibu wagonjwa. Na wakati huo, mishahara ndiyo ilikuwa mibaya kuliko leo hii. Nilijifunza uzalendo kutoka kwake.

 Nilijifunza kuwa kama kijana, kama mtanzania; ni lazima nipende kuwahudumia watanzania kwanza bila kujali maslahi binasfi. Mpaka leo hii, baba anaheshimika sana kila mahali alipofanya kazi. Na mie huwa nafurahi kwani kila mahali ninapoenda; huwa waniambia kuwa baba yangu alikuwa mtu mwema, alijali sana kutibu wagonjwa wake kwa moyo wa upendo.

Mimi sipingi madaktari kudai haki zao; haki zao wadai ila kwa kufuata sheria na bila ya kugoma na bila kuleta madhara katika utoaji huduma za afya.

Kuna wakati hata huwa nashindwa kuelewa mikutano ya madaktari huwa wanaongelea nini! Kuna siku niliona kwenye vyombo vya habari walikuwa wanasema yafuatayo:-


waliongea na kulalamika kuwa mishahara ya wabunge ni mikubwa wakati wao madaktari wanaowapokea watu duniani wakati wa kuzaliwa na watu wanawafia wao mikononi: wanalipwa kidogo!
Pia walisema kuwa kwanini Mwanasheria Mkuu wa Serikali analipwa mshahara mkubwa kuliko Mganga Mkuu wa Serikali (CMO) wakati wote wana nyadhifa sawa!

Napenda niwaelimishe madaktrai kuwa sijawai kuona sheria ya ajira ambayo inasema mshahara wa mfanyakazi unapaswa upunguzwe (ukiacha adhabu za kinidhamu) kama wao wanavyotaka wabunge wapunguziwe mishahara. Mshahara siku zote huwa unaongezeka. Ukiona mwenzio (wabunge) kaongezewa na wewe nenda ukadai uongezewe ila usiseme kuwa fulani apunguziwe ili mimi niongezewe…..sema hivi…..naomba niongezewe, kama mlivyomuongeza fulani.
Pia tambuemni mbunge si mfanyakazi, bali ni mwakilishi wa wananchi na sisi wananchi tumewabidili wabunge wetu kuwa mashine za kutolea hela.

Badala ya kumueleza mbunge akatutetea bungeni, tunataka atugaie hela ili tukatatulie matatizo yetu binafsi! Mbunge akiwanjima hela wananchi, wananchi husema subiri uchaguzi, lazima atatukoma.  Ukitokea msiba, au jambo la kheri au harambee yeyote; watu humsubiria mbunge achangie! Hata katika mgomo wa madaktari wapo wabunge wanaowachangia ili wazunguke katika kila hospitali kufanya vikao haramu vya kuhamasisha mgomo haramu!

Madaktari mnapswa mjue kuna wafanyakazi wa serikalini, hasa wakuu wa idara ambao si wabunge ila wana mishahara mikubwa kuliko wabunge na hata kumliko hata waziri mkuu. Mbona hamkusema kuhusu hao wakuu wa idara za mashirika ya umma na idara za serikali? Mkabaki kuwasakama wabunge peke yao? Pia mimi najiuliza kama daktari anaona ubunge una maslahi mazuri, sasa kwanini hajaenda kugombea mbunge! Au madkatari mnapiga kampeni Dr Ulimboka na viongozi wenzake wawe wabunge kwa kupitia mgomo?

Wapendwa madaktari mnapaswa mjue kuwa CMO (MMS) hana madaraka/majukumu sawa na Mwanasheria Mkuu (AG/MM) kama mnavyodhania. AG ni mshauri mkuu wa masuala ya sheria wa serikali na anaingia katika vikao vikuu vya maamuzi kama vile Baraza la Mawaziri, Bunge na nyinginezo!

Je CMO naye mliisha sikia anaingia katika vyombo hivyo! AG kwa hiyo ndio mshauri mkuu wa sheria wa kila wizara na serikali nzima. Ana majukumu mengi sana kuliko CMO. Licha ya kuwa maslahi ya CMO au AG yanategemea elimu, ujuzi, maarifa na uzoefu wake lakini watu hawa wana majukumu tofauti kabisa si kwa Tanzania bali hata nchi nyingine. CMO hana cha kujibu Bungeni, liwe jema au baya kuhusu huduma za afya, mzigo huo unabebeshwa waziri wa afya kulijibu bunge. 

Serikali ikashambuliwa bungeni kuhusu sekta ya afya; mwenye jukumu la kujibu siyo CMO ni waziri wa afya. Wakati hoja ikiwa ya kisheria mwenye kujibu au kulishauri bunge ni AG.

MADAI YA MADAKTARI
Madai ya madaktari yalikuwa kama ifuatavyo:-
Kuongeza Mshahara wa Mwezi kutoka Tshs. 700,000/= hadi  Tshs. 3.5 Mil
10% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho ya Kuitwa Kazini (Call Allowance)
30% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho ya Kazi za Hatari ( Risk Allowance)
30% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho ya Maladhi/Nyumba (Accommodation/Housing Allowance)

40% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho ya Kufanya kazi katika mazingira magumu (Hardship Allowance) 10% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho Usafiri (Transport Allowance)  Kukopeshwa magari na kupatiwa Bima ya Afya Daraja la Kwanza (First class/Green card).

Pamoja na madai mengine ya kimaslahi

MAONI
Masharti ya kugoma au kutokugoma yapo katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba ya 6 ya 2004 katika kifungu cha 75 hadi 85. Sheria hii ni moja ya sheria zenye kulinda maslahi ya mfanyakazi na mwajiri ambayo bunge liitunga baada ya maridhiano baina ya wafanyakazi, waajiri, serikali na Shirika la Kazi la Kimataifa/la Umoja wa Mataifa (ILO).

Kwa sheria zote za Tanzania, sijawai kuona sheria ambayo wadau walishirikishwa kwa hatua zote na kwa maamuzi yote. Tena nikiwamegea siri, Bunge ni kama halikutunga sheria hii, kwani kila kitu kilifanywa nje ya Bunge na wafanyakazi na waajiri; Bunge ni kama lilipiga muhuri tu. Nashangaa kuona madaktari wanaotaka kugoma kwa kutokufuata sheria za nchi.

Madaktari wakumbuke kuwa Mwajiri anayo haki ya kuwafukuza kazi na kuajiri wafanyakazi wengine, hili sio jambo la mchezo hata kidogo. Hawa viongozi wa madaktari wanatumiwa na wamerubuniwa na watu wasioipenda Tanzania. Wamerubuniwa na watu wanaopenda kufurahia watanzania wafe sasa sijui wanataka kula njama za wataokufa.

Mgomo wa madaktari haukuwa halali na hautakuwa halali kwani Sheria za Kazi za Tanzania haziruhusu migomo isipokuwa kwa masharti yafuatayo:-

Mgomo unapaswa uwe ni kuhusu suala la haki ambalo halipo katika sheria za kazi na wala halipo katika Mkataba wa Ajira wa Mfanyakazi husika. Kwa mfano, kama posho ya mazingira magumu haipo katika mkataba wa ajira na sheria haijaizungumzia, mfanyakazi ataruhusiwa kugoma.

Wafanyazi walioko katika huduma ya maji, huduma za usafi/huduma za kuondoa uchafu/taka (sanitation), umeme, huduma za afya & maabara, zima moto & uokoaji, huduma za udhibiti, uongozaji safari za anga & mawasiliano ya ndenge na usafiri katika huduma hizo hapo juu hawaruhusiwi kugoma.

Wafanyakazi wanaopaswa kutoa huduma wakati wa mgomo hawaruhusiwi kugoma. (kuna kipindi wafanyakazi baadhi wanaruhusiwa kugoma kwa sharti kuwa baadhi yao wafanye kazi wakati wa mgomo ili kazi zifanyike na huduma zitolewe)
Wafanyakazi ambao wamekatazwa na mkataba wa hiari na mwajiri kutokugoma.
Pia mahakimu, waendesha mashitaka na maafisa wa mahakama hawaruhusiwi kugoma. Vile vile wafanyakazi wote walioko katika sekta ya huduma muhimu kama za nilivyoeleza hapo awali:
matibabu/hospital/afya,
waongoza ndege,
huduma za umeme,
huduma za usambazaji/uzalishaji maji,
huduma za sanitation,
huduma za zima moto na ukoaji,
huduma za uongozaji wa ndege,
huduma za masiliano katika huduma za anga na
huduma zote za usafiri katika sekta tajwa hapo juu
hawaruhusiwi kugoma ila sheria ina wapa kipaumbele cha kupeleka malalamiko yako katika Kamati ya Huduma Muhimu (Essential Services Committee) badala ya kugoma. (Kifungu cha 76 na 77, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba ya 6 ya 2004)
Hii ndiyo sheria na sheria lazima ifuatwe, nchi haiongozwi kwa jazba na hamaki za watu. Ingekuwa hivyo basi kila mtu angafanya analolitaka basi hata amani, utulivu na ustarabu usingekuwepo.

Licha ya a-e hapo juu; Pia kabla ya kugoma kwa wafanyakazi wanaoruhusiwa kugoma (ambao siyo madaktari na siyo wafanyakazi wanaotoka katika huduma muhimu kama nilivyoanesha hapo juu i-ix)

inabidi suala la mgomo liwe limepelekwa katika Tume ya Maridhiano na Usuluhishi wa Masuala ya Kazi, pia Tume iwe imeshindwa kusuluhisha, mgomo unapaswa uitishwe na chama cha wafanyakazi, kura ya siri ipigwe kulingana na katiba ya chama na wafanyakazi kwa wingi wao wakukubali kugoma, mwajiri anapaswa apewe notisi ya masaa 48 kabla ya kugoma.
(Kifungu cha 75, 76 na 80, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba ya 6 ya 2004)

MAONI NA HITIMISHO
Mgomo wa madaktari ni haramu. Si kuwa ni kinyume cha sheria bali hata kinyume na maadili na kinyume na mafundisho ya dini zote ambazo watanzania wanaziamini. Yafuatayo yanapendekezwa yafanyike ili tatizo kama hili lisitokee:-

Madaktari wasiruhusiwe kufanya tena vikao vya mgomo kwani sheria hairuhusu. Wao wana viongozi wao, hao viongozi ndio wakae na serikali ili kutatua hilo tatizo. Haiwezekeni madaktari wote wakae katika kikao kimoja. Je nani atabaki hospitali kutibu wagonjwa? Uliona wapi waandishi wa habari au walimu nchi nzima wamekaa kikao kimoja? Hakuna kikao cha wanataaluma wote kwa pamoja kwa siku moja!

Madaktari waelimishwe kuhusu sheria za kazi na sheria za nchi na haki zao.
Madaktari waelezewe kuwa licha ya kuwa mishahara ya madaktari haikidhi gharama za maisha kwa sasa; lakini kwa wanataaluma wote wanaoajiriwa na serikali kama wahandisi, walimu, wanasheria, nk…..ni madakatari ndio wenye mishahara mikubwa. Kama ni kuwa maslahi ya udaktari si mazuri hata kwa wanataaluma wengine pia. Kila mfanyakazi wa serikali ukimuuliza atakueleza mshahara haumtoshi! Maisha huwa yanapande gharama na sijawai kuona yakishuka. Madaktari waeleimishwe jinsi ya kupambana na maisha na kuacha kujipendelea kwani wafanyakazi wote wa sekta ya afya na sekta nyingine pia wanaitaji kuongezewa mishahara na posho zao.
Serikali ijipange kuwabana wanaharakati ambao ndio walikuwa wanawashawishi madaktari ili wagome. Inasemekana vikao vya viongozi wa madaktari vilikuwa vinafanyika katika baadhi ya ofisi za wanaharakati tena mbaya zaidi wanaharakati wa haki za binadamu. Sasa hawa wanaharakati wa haki za binadamu ambao hawajali haki ya uhai wa mgonjwa ila wanajali haki ya maslahi ya daktari. Serikali izifute hizi taasisi. Kuna haja ya kuwabana sana wanaharakati hawa waliokuwa wanawashawishi madaktari na kuwaletea waandishi wa habari wa kuandika habari zenye kuwapendelea madaktari na kuliangamiza taifa. Hata hao watu wanaojiita wanadai haki za binadamu na kutoa ushauri wa kisheria kwa madaktari sijawai kuwaona mahakamani wakishinda kesi hata moja! Sijawai kuwaona wakipewa leseni ya uwakili! Sheria ya uwakili wa kujitegemea inasema kuwa ni wakili aliyesajiriwa baada ya kufanya mitihani ya kitaaluma na kufaulu ndiye anayepaswa kutoa ushauri wa kisheria. Sasa hawa hawajafaulu mitihani ya kuwa mawakili wanatoaje ushauri wa kisheria kwa madaktari? Ndiyo maana wanaishia kuwadanganya madaktari kama wanavyowadanganya wajane, walemavu na watu wote kutoka makundi maalumu wanaohitaji ushauri na huduma za kisheria bure. Ina maana watu hawa wanojiita wataalamu wa haki za binadamu hawajui kuwa haki ya kwanza ni kuishi! Sasa kwa nini watu wa haki za binadamu wanaunga mkono mgomo wa madaktari hawajui kuwa wagonjwa watafariki?.  Au wametumwa! Au wanataka wapewe misaada na nchi za nje kwa ajili ya kujilipa posho wanaharakati wakati mgomo ukitokea!
Madaktari walionekana kufurahia pale walipokuwa wakiona vyombo vya habari vikilaumu serikali na kuandika habari zao. Kuna haja ya kudhibiti vyombo vya habari katika masuala ya mgomo pia serikali itoe taarifa sahihi na muhimu.  Madaktari wakigoma hata waandishi wa habari watakufa kwa kukosa huduma. Naomba sana ndugu zangu waandishi wa habari, siku madaktari wakigoma, na nyinyi gomeni msiandike habari zao!
Madaktari watakaogoma na wakatwe mshahara wa siku watakazogoma, na madaktari watakaokuwa kazini wakati wa mgomo inapaswa wapewe posho ya kufanya kazi za ziada wakati wenzao wamegoma.
Madaktari ambao wako tayari kuendelea na kazi, walindwe na wasaidiwe waweze kutibu wagonjwa kwani wao ndiyo mashujaa wetu na wazelendo.
Madakatri waelimishwe kuwa si wao ndio wafanyakazi wa serikali pekee bali serikali ina wafanyakazi wengi na wote wana umuhimu sana na wote wanahitaji waongezewe posho na mishahara licha ya kuwa mishahara ya madaktari ni mikubwa kuliko mishahara ya wanataaluma nyingine. Unapohitimu chuo kikuu, ukiajiriwa na serikali kama wewe si daktari basi ujue haulipwi mshahara anaoupata dakatari. Suala hili naona hata vyombo vya habari hawaliandiki kabisa. Mishahara ya taaluma nyingine inafuata baada ya mishahara ya madaktari. Sasa mbona wanataaluma wengine hawajagoma na wanadai maslahi yao kwa kufuata taratibu za sheria! Iweje kwa madaktari?
Madaktari waelimishwe wajue wakigoma wagonjwa wanakufa na jukumu la kwanza la daktari ni kuokoa maisha (save life), jukumu ambalo hawataki kulifanya na kuamua kugoma.  Kama ndugu zetu wakifa kutokana na mgomo wa madaktari; sote tutasema….baba yangu, ndugu yangu, rafiki yangu alifiariki si kwa ugonjwa ila kwa mgomo wa madakari! Ndugu yangu alikufa kipindi kile madaktari walipogoma!...
Daktari anayegoma siwezi mtofautisha na Dr. Harold Fredrick Shipman wa Uingereza ambaye aliwaua wagonjwa wake zaidi ya wagonjwa 250 kwa makusudi kabisa . Wagonjwa hao 80% walikuwa wanawake na aliwaua kati ya mwaka 1995 hadi 2000. Nataka niwaambie watanzania wenzangu akina Dr. Shipman wameishaingia Tanzania pia. Sisi wagonjwa tujue hatma yetu imefika kabla ya mwenyezi mungu hajaamuru tufe.
Pia Daktari bingwa wa upasuaji na mashuhuri sana, Dr. Francis E. Sweeney aliwahi kuuwa zaidi ya wagonjwa wake 13 kwa makusudi kabisa!
Yupo pia Dr. Morris Bolber wa Philadelphia, Marekani katika miaka ya 1930 aliuwa zaidi ya wagonjwa wake 50 ili aweze kunufaika na bima (death benefits) ambazo ndugu/warithi wa wagonjwa walikuwa wakilipwa.
Dr. Thomas Neil Cream alinyongwa mwaka 1892 huko Uingereza baada ya kuwauwa wagonjwa wake zaidi ya 10 kwa makusudi kwa kuwapa sumu ya kuua badala ya matibabu.
Dr. Henry H. Holmes aliuwa zaidi ya watu 230 huko Chigaco, Marekani katika miaka ya 1870 hadi 1896.
Dr. John Bodkin Adams aliyekamatwa mwaka 1957 kwa kuwaua wagonjwa wake zaidi ya 10 huko Uingereza.
Serikali iajiri madaktari wengi katika majeshi yote ili kusaidia kutoa huduma katika hali ya migomo kama hii. Kuna haja ya kuwa na madaktari wengi katika majeshi yetu.
Vilevile hospitali za majeshi ziongezewe vifaa na wataalamu. Hosptali za binafsi na hospitali za mashirika ya dini zisaidiwe ili kupunguza gharama za matibabu katika hospitali binafsi.
Madaktari wasainishwe kiapo cha utii na kiapo cha kutogoma kabla ya kuanza kazi kama vile sheria inavyotaka.
Madaktari ambao hawaungi mkono mgomo, serikali iwasaidie ili waweze kufanya kazi bila ya kusumbuliwa na waliogoma.
Madakatri waelimishwe kuhusu vyama vyao kwani hawaelewi ndio maana hata Dr. Steven Ulimboka anayeongoza mgomo si daktari aliyeajiriwa na serikali, jambo ambalo si sahihi kwa mtu asiye mfanyakazi wa serikali kuigomea serikali.
Serikali ifuatilie hasa katika mifumo ya hela ya kibenki, nk kwani inasemekana kuwa watanzania wanaoishi nje ya nchi wakisaidiana na watu wasio wapenda maendeleao wanafadhiri mgomo kwa kutuma hela katika akaunti za benki za viongozi wa mgomo wa madaktari.
Serikali ijitaidi kujenga nyumba za madaktari kwa wingi jirani na hospitali ili kuboresha huduma za afya kwani madakatri wakiishi jirani na hospitali inakuwa rahisi kuhudumia wagonjwa. Mfano serikali ijitaidi kujenga nyumba za madaktari na wafanyakazi wa sekta ya afya jirani na hospital ili iwe rahisi kwao kutoa huduma. Daktari anayekaa Mbagala na anakuja kutibu wagonjwa katika hospital ya Mwanayamala anasafiri umbali mrefu kiasi kuwa anachoka akiwa njiani kuja kazini.
Mahusiano kati ya viongozi wa wizara ya afya na wahudumu wa afya yaendelee kuboreshwa ili kuwa na mahusiano mazuri katika sekata yote ya afya.
Madaktari wapunguze kuwe na misimamo ya kihafidhina kama Uamsho na Al Shabab. Madaktari watambue kuwa haki zao za maslahi mazuri ya kazi zinapoishia ndio haki ya mgonjwa ya kusihi inapoanzia.
Madakatari wajifunze kutoka kwa wanataaluma wengine jinsi ambavyo wanataaluma wengine wanavyoendesha umoja/vyama vya taaluma zao. Wajifunze kutoka kwa wahasibu, wahandisi, nk



[1] Imeandikwa na Ndugu Emmanuel Makene, wakili wa kujitegemea na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni.
Posted by MROKI On Wednesday, June 20, 2012 1 comment

1 comment:

  1. AnonymousJune 21, 2012

    walewale kasolo majina, pole wakili

    ReplyDelete

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo