Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni
akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule wakati wa ziara ya
kutembelea na kukagua shughuli za usafi na hatua zinazochukuliwa kutunza
mazingira katika Mto Ng’ombe, uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, jijini
Dar es Salaam, Oktoba 11, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akikagua shughuli za usafi na hatua zinazochukuliwa kutunza mazingira katika Mto Ng’ombe, uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Oktoba 11, 2026.Na Mwandishi wetu, Dar Es
Salaam
WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad
Yussuf Masauni, amewataka viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuweka mifumo
endelevu ya ukusanyaji na utunzaji wa taka, kudhibiti uchafuzi wa mazingira na
kuchukua hatua za kupunguza athari za mvua za El NiƱo.
Waziri Masauni amesema usafi
wa jiji haupaswi kutegemea maagizo kutoka kwa viongozi wa juu, bali unapaswa
kuwa sehemu ya utendaji wa kila siku wa taasisi na mamlaka zinazohusika na
usimamizi wa mazingira.
Amesema Dar es Salaam ni sura
ya nchi, hivyo viongozi katika ngazi zote wana wajibu wa kuhakikisha jiji
linakuwa safi na mazingira yanatunzwa wakati wote.
Waziri
huyo ametoa kauli hiyo Oktoba 11, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea na
kukagua shughuli za usafi na hatua zinazochukuliwa kutunza mazingira katika Mto
Ng’ombe, uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa licha ya
changamoto za upangaji wa makazi katika baadhi ya maeneo ya jiji, ni muhimu
kuimarisha udhibiti wa utupaji holela wa taka na kuweka mifumo madhubuti ya
ukusanyaji wake ili kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.
Mhe. Masauni amesema Ofisi ya
Makamu wa Rais haitakubali kuona utekelezaji wa shughuli za usafi na utunzaji
wa mazingira ukisuasua, akizitaka taasisi, halmashauri pamoja na viongozi wa
wilaya na mkoa kusimamia jukumu hilo kwa umakini na uwajibikaji.
Ameeleza kuwa taka hazipaswi
kuonekana kama uchafu pekee, bali zinaweza kuwa chanzo cha uchumi na fursa za
ajira kwa wananchi endapo zitakusanywa, kutunzwa na kuchakatwa kwa utaratibu
unaofaa.
Kutokana na hali hiyo,
amezitaka mamlaka husika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa taka ili kuwezesha
matumizi yake yenye tija na kuongeza thamani badala ya kutupwa ovyo na
kuhatarisha afya za wananchi pamoja na mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema wilaya hiyo inaendelea kutekeleza
kampeni za kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za usafi na utunzaji
wa mazingira.
Mtambule amesema wananchi
wanaoishi karibu na Mto Ng’ombe wameelekezwa kuondoka katika maeneo hayo ili
kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua, huku zoezi la kubomoa
nyumba katika maeneo husika likiwa limeanza kutekelezwa.
Ameongeza kuwa shughuli za
ukusanyaji na utunzaji wa taka zinaendelea, sambamba na juhudi za mamlaka za
wilaya kuhamasisha jamii kushiriki katika kulinda mazingira.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano
kati ya viongozi na wananchi katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na
salama, huku hatua za kudhibiti uchafuzi na kupunguza athari za mvua
zikiendelea kusimamiwa.
No comments:
Post a Comment