Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi na wananchi
mbalimbali wakati akihitimisha ziara yake mkoani Iringa kwa kukagua maendeleo
ya ujenzi wa Jengo la abiria na Maegesho ya magari katika Uwanja wa Ndege wa
Iringa, leo tarehe 18 Oktoba 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi na wananchi mbalimbali wakati akihitimisha ziara yake mkoani Iringa kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la abiria na Maegesho ya magari katika Uwanja wa Ndege wa Iringa, leo tarehe 18 Oktoba 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi akisikiliza maelezo kutoka kwa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta
kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Jengo la abiria na Maegesho ya magari katika
Uwanja wa Ndege wa Iringa akihitimisha ziara yake mkoani humo, leo tarehe 18
Oktoba 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi akiagana na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika Uwanja wa Ndege wa Iringa, mara baada ya kuhitimisha Ziara ya kikazi mkoani humo, leo tarehe 18 Oktoba 2026.
Muonekano wa Uwanja wa Ndege wa Iringa ukiwa
katika hatua mbalimbali za ujenzi wa Jengo la abiria na Maegesho ya Magari
unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 41.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amewataka Watanzania kuthamini juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, huku akisisitiza uzalendo, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa Taifa.
Makamu wa Rais ametoa wito huo mkoani Iringa
wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa
jengo la abiria na maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa,
mradi unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 41.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha
usafiri wa anga, kufungua fursa za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa sekta ya
utalii, hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Aidha, amezitaka Wizara ya Uchukuzi, Shirika la
Ndege Tanzania (ATCL) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutathmini
uwezekano wa kuboresha miundombinu ya kiwanja hicho, ikiwemo uwekaji wa taa
zitakazowezesha ndege kutua na kuruka wakati wa usiku.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewataka
Watanzania kuunganisha nguvu katika ujenzi wa Taifa kwa kutambua wajibu wao
badala ya kujiuliza Serikali imewafanyia nini, akisisitiza kuwa kila mmoja
anapaswa kujiuliza amelifanyia nini Taifa lake.
Amesema uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii
kutaongeza tija, mapato ya Serikali na kuimarisha huduma za kijamii pamoja na
miundombinu ya maendeleo.
Akizungumzia usimamizi wa fedha za umma, amewataka
mawaziri, viongozi wa taasisi, wabunge, wakuu wa wilaya, madiwani na watendaji
wa Serikali katika ngazi zote kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo na
kupambana na vitendo vya ubadhirifu na rushwa.
Ameonya watu wanaodai asilimia ya fedha za miradi
bila kufanya kazi yoyote, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitawavumilia wabadhirifu na
itahakikisha fedha za walipakodi zinatumika ipasavyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe.
David Mwakiposa Kihenzile amesema Serikali imetenga takribani shilingi trilioni
moja kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya viwanja vya ndege katika mikoa ya
Iringa, Njombe, Songea, Sumbawanga, Mwanza, Shinyanga, Manyara, Tanga, Mtwara,
Lindi na Dodoma.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo upo katika
hatua mbalimbali, huku baadhi ikiwa imekamilika, mingine ikiendelea na mingine
ikiwa katika hatua za maandalizi ya ujenzi na zabuni.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa,
akizungumzia kuchelewa mwa mradi wa barabara ya mchepuo wa Iringa, amesema
mkandarasi aliyelipwa fedha za awali kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 3.3
aliondoka eneo la mradi na kusababisha kazi kusimama.
Amesema tayari ameitisha kikao na mkandarasi
huyo ili kuhakikisha anarejea kazini, huku akiwaonya wakandarasi wanaoshindwa
kutimiza wajibu wao kuwa wanaweza kuchukuliwa hatua, ikiwemo kufutiwa usajili
na kuzuiwa kufanya kazi nchini.
Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya
mradi, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa
jengo la abiria na maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa
unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 41 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Mei
2027.
Amesema mradi huo ulioanza Julai 17, 2025,
unatekelezwa na kampuni ya China Harbour Engineering Company Limited, huku kazi
za ujenzi wa jengo la abiria na barabara za ndani zikiendelea.
Besta amesema jengo hilo litakuwa na uwezo wa
kuhudumia abiria 140 kwa wakati mmoja, sawa na abiria 250,000 kwa mwaka, pamoja
na maegesho ya magari 80, hatua itakayochochea shughuli za biashara, uwekezaji
na utalii katika Mkoa wa Iringa na maeneo jirani.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesema amemtaka
Waziri wa Ujenzi kuhakikisha anafanya mazungumzo na wakandarasi wanaojenga barabara
ya mchepuko (bypass) ya kuingia na kutoka Iringa Mjini ili kupata mwafaka wa
kukamilisha ujenzi huo ambao tayari serikali imetoa fedha.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
18 Oktoba 2026
Iringa.
0 comments:
Post a Comment