JKCI YAWAFIKIA VIONGOZI, YAWAFANYIA UCHUNGUZI WA AFYA WAKATI WA MKUTANO WA CEO FORUM 2026
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moris Budotela akimsomea majibu Meneja Uhusiano kwa Umma Hifadhi ya Ngorongoro Hamisi Dambaya wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya inayofanyika katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali (CEO Forum 2026) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha.
Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Glory Mtui akichukua sampuli ya damu wakati wa kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali (CEO Forum 2026) kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa wa Mikutano (AICC) jijini Arusha. **********
Na. Mwandishi Maalum - Arusha
Viongozi na watendaji wakuu wa
taasisi za umma nchini wanufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa
yasiyoambukiza zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi, mashirika
ya umma na wakala wa serikali (CEO Forum 2026).
Huduma hizo zinatolewa katika
kambi maalumu inaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) ambapo
washiriki wa kikao kazi hicho wanafanyiwa uchunguzi wa utendaji kazi wa moyo,
vipimo vya figo, wingi wa mafuta kwenye damu na wingi wa sukari kwenye damu
sambamba na kupewa elimu ya kujua namba zao.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hii Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI-ALMC) Farida
Abdallah alisema kambi huduma za uchunguzi wa afya kwa viongozi hao ni za
muhimu kwani wakiwa na afya bora wataweza kutekeleza majukumu yao kwa weledi na
kuleta maendeleo ya nchi.
“Tumepata fursa ya kuwahudumia
wenyeviti wa bodi, wakurugenzi wa taasisi, mashirika ya umma na mashirika ya
kiserikali nchini, viongozi hao wameendelea kufika katika kitengo cha uchunguzi
wa magonjwa ya moyo kwaajili ya kujua namba zao”, alisema Dkt. Farida.
Dkt. Farida alisema sambamba
na uchunguzi wa afya ya moyo wataalamu wa JKCI wameendelea kutoa elimu ya lishe
bora kwa viongozi hao ili waweze kufahamu viashiria vya magonjwa ya moyo na
namna ya kukabiliana na magonjwa hayo.
Kwa upande wake Meneja
Uhusiano kwa Umma wa Hifadhi ya Ngorongoro Hamisi Dambaya alisema amefurahishwa
na huduma aliyoipata kutoka kwa wataalamu wa JKCI kwani uchunguzi aliofanyiwa
umemsaidia kupata taarifa sahihi kuhusu afya yake.
“Nimefanyiwa uchunguzi wa afya
na kuhudumiwa vizuri, kikubwa nimefanyiwa vipimo vya moyo na kupata elimu ya
kutosha kuhusu magonjwa hayo. Watanzania
wana kila sababu ya kufika katika Taasisi hii na kuchunguza afya zao”, alisema
Dambaya.
Kambi hiyo inaendelea kutoa
huduma za uchunguzi na elimu ya afya kwa washiriki wa mkutano wa CEO Forum 2026
ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kinga na
utambuzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza.
No comments:
Post a Comment