Nafasi Ya Matangazo

September 08, 2026

Na Mwandishi Wetu, 
ADDIS ABABA.
Ethiopia“Afrika inapaswa kutumia utajiri wake wa madini muhimu kujenga viwanda, kuongeza uzalishaji wa umeme na kuunda ajira ndani ya bara, badala ya kuendelea kusafirisha malighafi bila kuongeza thamani,” amesema Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard S. Muyungi.

Dkt. Muyungi ametoa kauli hiyo wakati akitoa mchango wa Tanzania katika Mkutano wa CCDA-XIV unaofanyika Addis Ababa, Ethiopia, akisisitiza kuwa mpito wa haki kuelekea uchumi usiotegemea nishati za kisukuku haupaswi kuishia katika kubadili vyanzo vya nishati pekee, bali unapaswa pia kubadilisha mifumo ya kiuchumi inayohusika na mchakato huo.

Amesema swali la msingi kwa Afrika ni iwapo bara hilo litaendelea kuwa msambazaji wa madini yanayohitajika katika uchumi wa kijani duniani au litatumia rasilimali hizo kujenga viwanda, kuongeza uzalishaji wa umeme, kuendeleza teknolojia na kuunda ajira ndani ya Afrika.

Kwa mujibu wa Dkt. Muyungi, Afrika ina sehemu kubwa ya rasilimali za madini muhimu duniani, lakini bado ina uwezo mdogo wa kuchakata na kuongeza thamani. Ameeleza kuwa bara hilo linamiliki takribani asilimia 29 ya akiba ya bauxite duniani lakini lina chini ya asilimia moja ya uwezo wa kusafisha alumina, huku likiwa na asilimia saba ya akiba ya nickel lakini uwezo wa kusafisha ukiwa chini ya asilimia mbili. Hali hiyo inaenda sambamba na changamoto ya nishati, ambapo takribani Waafrika milioni 600 bado hawana umeme.

Akizungumzia nafasi ya Tanzania, Dkt. Muyungi amesema nchi ina fursa kubwa kutokana na rasilimali za graphite, nickel, cobalt, copper na rare earths, ambazo ni muhimu katika teknolojia za nishati safi na uzalishaji wa bidhaa za kisasa.

Ameutaja Mradi wa Kabanga kuwa miongoni mwa fursa kubwa za Tanzania katika mnyororo wa thamani wa madini muhimu, ukiwa na akiba ya madini inayofikia tani milioni 52.2 yenye kiwango cha takribani asilimia 1.98 cha nickel, pamoja na copper na cobalt. Tanzania pia ina rasilimali kubwa za graphite pamoja na Mradi wa Ngualla wa rare earths.

Hata hivyo, amesema Tanzania haipaswi kujikita katika uchimbaji pekee, bali inapaswa kutumia rasilimali hizo kujenga mnyororo wa thamani wa ndani na kikanda, ambapo graphite inaweza kutumika katika uzalishaji wa vifaa vya anodi za betri, huku nickel, cobalt na copper zikichochea mnyororo wa uzalishaji wa betri na miundombinu ya umeme.

Dkt. Muyungi amesema madini muhimu hayawezi kuchochea mpito wa haki bila kushughulikia pia changamoto ya upatikanaji wa nishati, akisisitiza umuhimu wa Mission 300, unaolenga kuwaunganisha Waafrika milioni 300 na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030, pamoja na utekelezaji wa Tamko la Nishati la Dar es Salaam lililoidhinishwa na nchi 48 za Afrika Januari 2025.

Amesema hadi Juni 2026, zaidi ya watu milioni 50 katika nchi 40 za Afrika walikuwa wameunganishwa na umeme kupitia Mission 300. Aidha, amesisitiza umuhimu wa nishati safi ya kupikia katika mpito wa haki kwa sababu inagusa afya, mazingira na ustawi wa wananchi, hususan wanawake.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, amesema nchi za Afrika zinapaswa kutumia AfCFTA kujenga vituo vya kikanda vya uchakataji na uzalishaji, kuendeleza miundombinu ya pamoja, kukuza wazalishaji wa Kiafrika na kuongeza ushiriki wa wazawa katika mnyororo wa thamani. Amebainisha kuwa graphite na nickel za Tanzania zinaweza kukamilishana na cobalt ya DRC, copper ya Zambia na manganese pamoja na Platinum Group Metals kutoka Kusini mwa Afrika.

Dkt. Muyungi pia amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika ujuzi, utafiti na ubunifu ili kuhakikisha Afrika haibaki kuwa msambazaji wa malighafi. Amesema African Green Minerals Strategy inapendekeza wawekezaji kutenga angalau asilimia tano ya mishahara kwa ajili ya kujenga ujuzi wa STEM wa wenyeji na asilimia moja ya mauzo kwa ajili ya utafiti, maendeleo na ubunifu.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa wakati mataifa makubwa duniani yakiongeza ushindani wa kupata madini muhimu kwa ajili ya teknolojia za nishati safi, Afrika inapaswa kutumia fursa hiyo kuhakikisha rasilimali zake zinaleta ongezeko la thamani, uhamishaji wa teknolojia, miundombinu, ujuzi, ulinzi wa mazingira na manufaa kwa jamii, ili madini muhimu yawe kichocheo cha ujenzi wa viwanda na maendeleo endelevu barani Afrika
Posted by MROKI On Tuesday, September 08, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo