Nafasi Ya Matangazo

April 22, 2026







Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Ramadhani Lwamo, amesisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi katika uthaminishaji wa madini ya vito kupitia ushirikiano wa karibu kati ya Tume na wadau wa sekta ya madini, hususan katika upangaji na uhuishaji wa bei elekezi za madini hayo.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwazi, kuongeza tija pamoja na kuboresha mazingira ya biashara ya madini nchini.

Akizungumza katika kikao  kazi cha Wajimolojia na Wathaminishaji wa Madini kilichofanyika leo Aprili 22, 2026, Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma, Eng. Lwamo amesema kuwa ushirikiano huo tayari umeanza kuleta matokeo chanya.

Amesema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuboreshwa kwa mifumo ya uthaminishaji wa madini ya vito na kuongezeka kwa mapato ya Serikali yatokanayo na biashara ya madini ya vito na almasi.

Eng. Lwamo ameeleza kuwa juhudi hizo zinaendana na lengo la Tume ya Madini la kukusanya shilingi trilioni 1.2 katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku taasisi ikiendelea kuimarisha upatikanaji wa wataalam wa uthaminishaji pamoja na vitendea kazi muhimu ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu hayo.

Aidha, amewapongeza watumishi wa Tume ya Madini kwa juhudi wanazoendelea kuzionesha na kusisitiza umuhimu wa kuongeza bidii ili kufikia na kuvuka malengo yaliyowekwa.

Kikao hicho kinatarajia kufuatiwa na vikao maalum vya kupitia na kuhuisha bei elekezi za madini ya vito kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, wakiwemo FEMATA, TAMIDA, TAWOMA na CHAMATA.
Posted by MROKI On Wednesday, April 22, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo