March 09, 2026

WANAWAKE WA TFS SAO HILL WAWAFARIJI WATOTO YATIMA MUFINDI

Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu akiwa anamfariji mtoto wa yatima wa kituo cha Caring from Childhood to Youth kilichopo katika kijiji cha Bumilayinga,wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu akiwa akikabidhi zawadi  katika kituo cha watoto yatima cha Caring from Childhood to Youth kilichopo katika kijiji cha Bumilayinga,wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake.
Na Fredy Mgunda, Mufindi
Wanawake wahifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoka Shamba la Miti Sao Hill wametembelea na kuwafariji watoto wanaolelewa katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Caring from Childhood to Youth kilichopo katika kijiji cha Bumilayinga, wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya shughuli za kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambapo wanawake hao walionyesha upendo na mshikamano kwa watoto hao kwa kutumia muda kuzungumza nao pamoja na walezi wao na kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake hao, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, alisema licha ya majukumu yao ya kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu, wanatambua pia umuhimu wa kushiriki katika shughuli za kijamii zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja.

Alisema vitendo hivyo vinasaidia kuimarisha upendo, mshikamano na ushirikiano ndani ya jamii, huku vikiwapa watoto walioko katika mazingira magumu matumaini na ari ya kuendelea kupambana ili kufikia malengo yao ya maisha.

Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha Caring from Childhood to Youth, Bw. Ponsiano Mfikwa, aliwashukuru wanawake hao kwa kuwatembelea na kuwakumbuka watoto hao, akisema ujio wao umeleta faraja kubwa kwa watoto pamoja na walezi wao.

Alisema msaada huo ni ishara ya moyo wa upendo na unatoa mfano mzuri kwa jamii kuendelea kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kukua katika malezi bora.

Naye Diwani wa Kata ya Sao Hill ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Mhe. Stephen Msigwa, aliwapongeza wanawake wahifadhi kwa juhudi zao katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu pamoja na kushiriki katika shughuli za kijamii.

No comments:

Post a Comment