Wanawake wa Tume ya Madini wamefanya tukio la kibinadamu lililogusa mioyo ya watu wengi kwa kulipia gharama za matibabu kwa wagonjwa wenye uhitaji maalum katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Kitengo cha Usafishaji Damu (Dialysis) iliyopo jijini Dodoma.
Msaada huo umetolewa kupitia ziara waliyoifanya hospitalini hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo kilele chake ni tarehe 08 Machi, mwaka huu. Wanawake hao wamejumuika na kuwatia moyo wagonjwa waliokumbwa na changamoto za kifedha, wakiwemo waliokuwa wakipatiwa matibabu ya figo.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Tume ya Madini, Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, amesema:
“Tunatambua kila mtu ana mahitaji mbalimbali, lakini nashukuru kwa michango iliyotolewa na Tume ya Madini kufanikisha kulipia baadhi ya gharama kwa wagonjwa kumi na wanne (14) waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za kifedha katika kupata matibabu ya figo. Huu ni wakati wa kuwatia moyo na kuonyesha upendo wetu kwa wenzetu.” amesema.
Mhandisi Mwasha amesisitiza kuwa wanawake wana wajibu wa kuwa walezi na kuendeleza msaada kwa wananchi wenye mahitaji zaidi.
“Kutoa ni akiba ya baadaye, sio kwa familia zetu tu, bali kwa jamii kwa ujumla,” ameongeza.
Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, amesema msaada huu ni njia ya kugusa maisha ya wananchi na kurudisha tabasamu miongoni mwa wagonjwa, huku akibainisha gharama kubwa ya matibabu ya figo nchini.
Wakati huohuo akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Mwanaidi Makao ameshukuru kwa msaada huo, akisema:
“Sio rahisi kusafisha damu kila mara kwa wagonjwa wetu kwa sababu gharama ni kubwa. Tunashukuru kwa kutuunga mkono na kuwasaidia wenye uhitaji.”
Naye Daktari bingwa wa hospitali hiyo, Dkt. Sabina Mmbali, amefafanua kuwa asilimia 60 ya wagonjwa wa figo wanatumia bima za afya, huku asilimia 40 ya wengine wakilipia matibabu kwa uwezo wao wenyewe. Matibabu ya figo hutakiwa kufanywa mara tatu kwa wiki.
“Msaada huu ni faraja kubwa kwa wagonjwa wetu, na tumefurahi sana,” amesema Dkt. Mmbali.
Wananchi wengi wameshuhudia tukio hilo na kupongeza jitihada za wanawake wa Tume ya Madini, wakisema kwamba ni ishara ya utu na mshikamano kwa kijamii.













0 comments:
Post a Comment