Wananchi, wanafunzi na walimu wa Kata ya Busonzo, Kijiji cha Idoselo wilayani Bukombe, wamepanda miche 200 ya miti ya matunda katika Shule Shikizi ya Mererani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani mwaka 2026.
Zoezi hilo lililofanyika Machi 19, limehusisha ushiriki mkubwa wa wananchi waliojitokeza kwa wingi kuonesha dhamira ya kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza katika tukio hilo, Diwani wa Kata ya Busonzo, Mhe. John Malikioli, aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanaitunza miti hiyo ili iweze kukua na kuleta manufaa ya kiuchumi na kimazingira.
“Kupanda miti ni hatua ya kwanza, lakini kuitunza ni wajibu wa kila mmoja wetu,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Emilian Fabian, aliwataka wananchi kubadili mtazamo hasi dhidi ya wahifadhi na badala yake kushirikiana nao katika kulinda rasilimali za misitu.
Alisema wahifadhi wapo kwa ajili ya kuhakikisha mazingira yanatunzwa na siyo kuwa kikwazo kwa wananchi.
Naye Afisa Misitu, Bi. Bahati Kamwana, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, alitoa wito kwa wananchi kuendeleza juhudi za utunzaji wa misitu ili kuhakikisha Wilaya ya Bukombe inakuwa ya kijani na yenye mazingira rafiki kwa maendeleo endelevu.
Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa Wilaya ya Bukombe imeendelea kufanya vizuri katika kampeni ya upandaji miti, ambapo zaidi ya miche 500,000 imepandwa katika msimu huu, hatua inayochangia uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani hutoa fursa kwa jamii kukumbushwa umuhimu wa misitu katika kukuza uchumi, kulinda mazingira na kuboresha maisha ya binadamu, huku wananchi wakihimizwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti.





.jpeg)
No comments:
Post a Comment