Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe. Zephania Sumaye, jana Machi 19, 2026 wameongoza zoezi la upandaji miti katika kijiji cha Kileti, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani pamoja na kuimarisha uhifadhi shirikishi wa misitu.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Wilaya alimpongeza Kamisna wa Uhifadhi TFS, Pro. Dos Santos Silayo kwa kuendeleza ushirikiano na jamii zinazozunguka misitu, akieleza kuwa hatua hiyo inachangia kurejesha manufaa kwa wananchi na kuongeza ulinzi wa rasilimali hizo muhimu.
“Ni jambo la kujivunia kuona wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali za misitu. Ushirikiano huu utasaidia kuhakikisha misitu inalindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” alisema.
Alisisitiza umuhimu wa kuweka mipaka ya wazi ya mashamba na maeneo ya misitu kwa kupanda miti, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti uharibifu wa misitu na kuboresha matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya milimani ya Lushoto.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la miti Shume, Christopher Yakuti, alifananisha umuhimu wa misitu na maisha ya binadamu, akieleza kuwa uwepo wa misitu ni sawa na uhusiano wa samaki na maji.
“Misitu inapotea, maisha pia yanakuwa hatarini. Ni wajibu wetu sote kushirikiana kulinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi,” alisema.
Naye Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba, Mhifadhi Mwandamizi Grace Kabuche, alisema maadhimisho hayo yameambatana na hatua mbili muhimu; kusaidia jamii zinazozunguka hifadhi pamoja na kuhamasisha upandaji miti kwa lengo la uhifadhi endelevu.
Alieleza kuwa zaidi ya miti 2,000 imepandwa katika kijiji cha Kileti, huku TFS ikikabidhi mifuko 280 ya saruji kwa vijiji na taasisi za elimu ili kusaidia miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa zahanati na vyoo vya shule.
Kabuche aliongeza kuwa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo vimeunda kamati maalum za uhifadhi zinazoshiriki katika doria na ulinzi wa misitu, hatua inayosaidia kuimarisha usimamizi shirikishi wa rasilimali hizo.
Zoezi hilo linaendelea kuwa sehemu ya juhudi za kitaifa za kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa misitu na kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu kupitia matumizi bora ya rasilimali za asili.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment