Nafasi Ya Matangazo

March 05, 2026



Na John Mapepele
Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema kuwa ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na Washirika wa Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund) umeendelea kuwa chachu ya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma za afya nchini.
 
Akizungumza katika mkutano wa nchi washirika wa Mfuko huo Machi 2, 2026 jijini Dar es Salaam Mhe. Mchengerwa alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuiwezesha Tanzania kufikia hatua ya kufanya majadiliano muhimu kuhusu mustakabali wa sekta ya afya. Alisisitiza kuwa pale washirika wa sekta ya afya wanapoungana kwa uwazi, dhamira na malengo ya pamoja, maisha ya wananchi huboreshwa kwa haraka zaidi.
 
“Mkutano huu si wa kawaida. Ni wakati wa kimkakati wa kuimarisha ushirikiano na kuthibitisha upya wajibu wetu wa pamoja wa kutoa huduma bora za afya kwa Watanzania,” alifafanua.
 
Mfuko wa Pamoja wa Afya Waimarisha Huduma za Msingi nchini
 
Waziri Mchengerwa alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Pamoja wa Afya mwaka 1999, zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.3 zimechangishwa kusaidia utekelezaji wa mipango ya kimkakati ya sekta ya afya. Asilimia 90 ya fedha hizo zimeelekezwa katika huduma za Afya ya Msingi zinazosimamiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
 
Alibainisha kuwa kuanzia mwaka 2017, fedha za Mfuko zilianza kupelekwa moja kwa moja katika zaidi ya vituo 7,345 vya afya kupitia utaratibu wa ufadhili wa moja kwa moja kwa Vituo vya Afya, hatua iliyoongeza uwazi na ufanisi katika matumizi ya rasilimali.
 
“Kwa pamoja tumeimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu, tumepunguza vifo, na kuongeza uzazi salama katika Vituo vya Afya. Mageuzi haya yameweka msingi imara wa mfumo wa afya wenye ustahimilivu,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa alisema Tanzania ipo katika kipindi cha mageuzi makubwa, huku lengo kuu likiwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Alifafanua kuwa wakati bima hiyo ikipanua ulinzi wa kifedha kwa wananchi, Mfuko wa Pamoja wa Afya unabaki kuwa mhimili wa kuhakikisha huduma bora na zenye usawa zinapatikana kwa wote.
 
Aidha, Waziri huyo alitoa wito kwa washirika kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Afya Kidijitali uliounganishwa, akisisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo mmoja wa kitaifa unaounganisha taarifa zote za afya.
 
“Huwezi kusimamia usichokiona, na huwezi kuboresha usichokipima. Mfumo wa kidijitali uliounganishwa ni mageuzi ya utawala, ufanisi na uaminifu,” alisema.
 
Akizungumzia dira ya muda mrefu, Mhe. Mchengerwa alisema Tanzania inalenga kupunguza utegemezi mkubwa wa bidhaa za afya kutoka nje kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa tiba na teknolojia za afya.
 
“Hili si suala la uchumi pekee, bali ni suala la usalama wa afya ya taifa. Mfumo imara wa afya lazima uunganishe ustahimilivu wa kifedha, kidijitali, rasilimali watu pamoja na uzalishaji na ugavi,” alifafanua.
 
Waziri huyo alieleza kuwa mandhari ya maendeleo duniani yanabadilika, huku nchi zikielekea kwenye ushirikiano wa thamani ya pande zote na uendelevu wa muda mrefu.
 
“Tunaamini mustakabali wa ushirikiano haujengwi juu ya utegemezi, bali ubunifu wa pamoja na uwekezaji. Ushirikiano wenye busara haufiche changamoto; hujifunza kutoka kwake na hubuni mifumo bora zaidi,” alisema.
 
Alikiri kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wakati, akieleza kuwa Serikali inafanya kazi kwa karibu na Wizara nyingine ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI  na Wizara ya Fedha ili kuondoa vikwazo vya kiutendaji na kuimarisha uwazi katika usimamizi wa fedha.

Akizungumza  kwa niaba ya timu ya mabalozi walioshiriki katika kikao hicho, Mheshimiwa Elke Wisch, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Mratibu wa Wadau wa Mfuko wa Pamoja wa Afya alimshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa katika kuokoa vifo vya mama wajawazito na mtoto wakati wa kujifungua.
 
Mhe. Wisch aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuendelea kuchangia katika sekta ya afya.
 
Aidha, walisifu juhudi zilizofikiwa  katika kuimarisha huduma bora za afya katika kipindi kifupi cha Serikali chini ya Rais Samia.
Posted by MROKI On Thursday, March 05, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo