Nafasi Ya Matangazo

March 09, 2026

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali itachukua hatua kali ikiwemo kufilisiwa kwa yeyote anatakayebainika kuhujumu wakulima kwa kuwauzia pembejeo zisizokuwa na ubora zikiwemo mbegu.
 
Ameyasema hayo leo Jumapili, Machi 08, 2026 alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Laela A wilayani Sumbawanga, Rukwa. Amesisitiza kuwa watu hawatovumiliwa kwa kuwa wana lengo la kuliingiza Taifa katika njaa.
 
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Sylvia Sigula kuishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku ya pembejeo ila ameiomba Serikali kuwatatulia changamoto ya kuuziwa mbegu zisizokuwa na ubora jambo linalosababisha wakulima kupata hasara kwani kilimo ndio uchumi wa Rukwa.

ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Rukwa kufuatia taarifa za kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi hiyo.

Ametoa agizo hilo leo Jumapili (Machi 8, 2026) wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa Laela mkoani Rukwa baada ya kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali haitavumilia kuona miradi ya maendeleo ikicheleweshwa wakati fedha zake tayari zimetolewa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

 “Kamanda wa TAKUKURU nifanyie uchunguzi wa kina, senti mpaka senti, yeyote aliyehusika kwenye hii fedha hapa nipe taarifa hiyo ili niweze kufanya maamuzi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameonesha kutoridhishwa na kuchelewa kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari, madarasa pamoja na miundombinu mingine ya elimu katika eneo hilo.
 
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema wizara amekuwa ikifanya uchunguzi na kuchukua hatua pale inapobaini kuwepo kwa pembejeo zisizokuwa na ubora na tayari kuna mtu mmoja amekamatwa mkoani humo.
Posted by MROKI On Monday, March 09, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo