Nafasi Ya Matangazo

January 27, 2026


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipanda mti wa Muembe (Mangifera indica) katika eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 27 Januari, 2026, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Rais Mhe. Dkt. Samia alizaliwa tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
  
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikata Keki mara baada ya kuongoza Zoezi la kupanda miti kwenye eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 27 Januari, 2026, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Rais Mhe. Dkt. Samia alizaliwa tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi mara baada ya kuongoza Zoezi la kupanda miti kwenye eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 27 Januari, 2026, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Rais Mhe. Dkt. Samia alizaliwa tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

**********

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza zoezi la kupanda miti katika maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi, Zanzibar,kama sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa na utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji miti ya “27 ya Kijani” 

Rais Dkt. Samia alisema ameichagua siku yake ya kuzaliwa kuwa siku ya kupanda miti kama ishara ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu na kutimiza wajibu wake wa kulinda mazingira na kuacha urithi kwa vizazi vijavyo, na kuongeza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kupanda miti ili kurejesha uoto wa asili uliopotea kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aliongeza kuwa Tanzania inakaribia kuwa na takribani watu milioni 70, idadi ambayo itaisogeza nchi kufikia ulinzi na mustakabali endelevu wa mazingira kitaifa, ikiwa katika Watanzania milioni 30 kila mmoja atachukua hatua ya kupanda na kutunza angalau mti mmoja kila mwaka.

Alieleza kuwa, mabadiliko ya tabianchi ni uhalisia unaoathiri maisha ya wananchi kupitia ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko, ongezeko la joto na kuongezeka kwa kina cha bahari, akiongeza kuwa upandaji na utunzaji wa miti ni miongoni mwa njia mahsusi za kukabiliana na athari hizo kwa kuhifadhi vyanzo vya maji, kuimarisha uzalishaji wa chakula, kuboresha afya ya binadamu na kulinda bioanuwai.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia alieleza umuhimu wa kuhusisha watoto katika juhudi za utunzaji wa mazingira, akisisitiza kuwa malezi ya mapema hujenga kizazi chenye uelewa na uwajibikaji wa kulinda maliasili za Taifa.

“Mtoto akipanda mti na akausimamia akiwa mdogo, anakua akiwa na upendo wa mazingira na fikra za kulinda maliasili za nchi yetu,” alisema Rais Samia.

Akieleza malengo ya zoezi hilo, Rais Dkt. Samia alieleza kuwa kupanda miti ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya kitaifa ya kukuza sekta ya kilimo na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa, sambamba na fursa za kiuchumi zitokanazo na biashara ya hewa ukaa kupitia misitu inayolindwa na kurejeshwa.

Kimataifa, alieleza Tanzania inaunga mkono kwa vitendo Ajenda ya Maendeleo Endelevu 2030, hususan malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda uhai katika ardhi, kuhakikisha usalama wa chakula, afya ya jamii na upatikanaji wa maji safi.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia aliwashukuru Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kuanzisha na kuendeleza kampeni ya “27 ya Kijani”, pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFSA) na wadau wengine kwa kusimamia, kuhamasisha na kuwezesha upandaji wa miti nchini hususan katika kampeni hiyo.
Matukio mbalimbali wakati wa Zoezi la kupanda miti kwenye eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 27 Januari, 2026, katika kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 27 Januari, 1960. 

  
Posted by MROKI On Tuesday, January 27, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo