Ikiwa ni mkakati wa kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kimitaji, Wizara ya Madini imeingia makubaliano na Benki ya CRDB kupitia programu maalum kwa ajili ya kuwasadia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mikopo kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya uchenjuaji (CIP), vifaa na gharama za uendeshaji.
Akizungumza kwenye kikao cha kujadili mapendekezo ya ushirikiano kati ya Benki ya CRDB na Tume ya Madini katika utoaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini, Waziri Mavunde amesema kupitia makubaliano haya, wachimbaji wadogo wenye leseni za madini wataweza kuomba na kupatiwa mikopo na benki hiyo na kuwezesha uzalishaji wao kuwa wenye tija na mchango wao kuendelea kukua kwenye makusanyo ya maduhuli ya Serikali.
Akielezea moja ya wanufaika wa programu hiyo Waziri Mavunde amesema kuwa ni pamoja na kikundi cha SAZA GOLD FAMILY ambapo Benki ya CRDB ipo mbioni kutoa mkopo wa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kuchenjua madini ya dhahabu na vifaa vya uchimbaji kwa kikundi hicho kinachoendesha shughuli zake katika eneo la Saza mkoani Songwe.
Ameendelea kusema kuwa awali, kupitia ziara ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu katika eneo la Saza, kikundi cha wachimbaji wadogo kupitia Mbunge wa Songwe, Mhe. Philipo Mulugo waliomba kupatiwa leseni ya uchimbaji wa madini, ambapo Rais Samia alielekeza kikundi hicho kupatiwa leseni ya uchimbaji iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni ya BAFEX.
Amesema ikiwa ni mkakati wa kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kikundi cha SAZA GOLD FAMILY kilipewa leseni na kuanza kuchimba madini na kuomba mkopo kwa ajili ya mtambo wa uchenjuaji wa madini na vifaa ambapo mchakato wake ulianza mara moja kupitia Benki ya CRDB.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameitaka Tume ya Madini na Benki ya CRDB kukamilisha Makubaliano ya Awali (MoU) ifikapo Jumatano ijayo ili taratibu za utoaji wa mkopo zikamilike mapema.
Ameeleza manufaa ya mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini kuwa ni pamoja na uzalishaji kuongezeka na mchango wao kuongezeka kwenye ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali hasa ikizingatiwa kwa sasa wanachangia asilimia 40.
Wakati huohuo, Mhe. Mavunde amezitaka Taasisi za Fedha nchini kuwaamini wachimbaji wadogo wa madini kwa kuweka mazingira rafiki ya mikopo kwani wana utajiri mkubwa wa rasilimali za madini.
“Ninaomba Taasisi za Fedha kuwaamini wachimbaji wa madini kwa kuwa wenyewe kwa wenyewe wana uwezo wa kukopeshana hadi shilingi bilioni tano kwa kuaminiana, mkiweka mazingira mazuri na kuwakopesha mtapata faida kubwa sana kupitia Sekta ya Madini na kukuza mitaji yenu,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Naye Mbunge wa Songwe, Mhe. Philipo Mlugo akizungumza kwenye kikao hicho amempongeza Waziri Mavunde kwa kuwa mlezi wa wachimbaji wadogo wa madini nchini sambamba na kuwaunganisha na Taasisi za Fedha kwa lengo la kuhakikisha wanatajirika kupitia Sekta ya Madini.
“Ninampongeza sana Waziri Mavunde kwa kuwa mstari wa mbele kuwapambania wachimbaji wadogo wa madini kuanzia kwenye upatikanaji wa leseni za madini, kuwaunganisha na Taasisi za Fedha kwa ajili ya upatikanaji wa mikopo na kutatua changamoto mbalimbali,” amesema Mulugo.
Katika hatua nyingine ameitaka Benki ya CRDB kuajiri wataalam wa madini ili kuwa na uelewa wa Sekta ya Madini hali itakayowawezesha kutoa mikopo kwa urahisi zaidi na kuweka mazingira mazuri ya ukopeshaji.
Naye Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa sambamba na kupongeza Benki ya CRDB kwa nia yake ya kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini amewataka kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kuhusu masuala ya fedha ili waweze kukopa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba ameshauri Benki ya CRDB kuendelea kuweka mazingira mazuri ya utoaji wa mikopo kwa kuangalia historia ya uzalishaji kwa wachimbaji wadogo wa madini ili waweze kukopesheka.
Wakati huohuo akizungumza kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa Songwe Gold Family, Simon Ndaki ameshukuru sana kwa msaada wa Serikali kwa kuwaunganisha na Benki ya CRDB na kufanikisha hatua za awali za maombi ya mkopo huo.
“Tunamshukuru sana Waziri wa Madini na timu yake kwa kutupatia leseni ya madini na kusimamia kikamilifu hatua zote za awali za maombi ya mkopo kwenye kikundi chetu chenye wanachama 264, tunaamini kupitia uzalishaji wetu kwa kutumia vifaa vya kisasa mchango wetu unakwenda kuwa mkubwa kwenye makusanyo ya maduhuli ya Serikali,” amesema Ndaki.








No comments:
Post a Comment