Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imekutana kujadili utekelezaji na mwelekeo wa Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Najma Murtaza Giga (Mb.), kilichofanyika tarehe 23 Januari, 2026 katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb.), amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha Sera ya Mambo ya Nje inatekelezwa kwa ufanisi sambamba na mabadiliko ya mazingira ya kimataifa, ili kulinda na kukuza maslahi ya Taifa.
Kikao hicho, kilichowakutanisha wajumbe wa Kamati hiyo na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kililenga kutathmini namna utekelezaji wa sera hiyo unavyoendelea kuimarisha maslahi ya Taifa katika nyanja za diplomasia, usalama, uchumi na ushirikiano wa kimataifa.
Aidha, wajumbe wa Kamati walitoa mapendekezo na maelekezo yaliyolenga kuimarisha utekelezaji wa sera hiyo, ikiwemo kuongeza jitihada za diplomasia ya uchumi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na kulinda amani na usalama wa Taifa.
Kikao hicho ni sehemu ya majukumu ya Kamati ya Bunge katika kusimamia na kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa sera, mipango na shughuli za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa lengo la kuimarisha mchango wa diplomasia katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa na Ajenda ya Maendeleo Endelevu.
Hatua hizo pia zinalenga kuimarisha taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika medani ya kimataifa, sambamba na kuendeleza maslahi ya Taifa katika mazingira yanayobadilika ya kidiplomasia na kiuchumi duniani.









No comments:
Post a Comment