Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga amewapongeza Mawakili wa Kujitegemea kwa ushirikiano wao, hatua iliyosaidia kuongeza kasi ya kumaliza mlundikano wa mashauri katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Dodoma.
Mhandisi Sanga ametoa pongezi hizo Juni 12, 2025 wakati akizungumza na Mawakili hao walipomtembelea Ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.
"Moja ya jambo muhimu katika kuboresha utendaji ni kupongeza pale ambapo kazi imefanyika vizuri. Ndugu zetu hawa wanastahili pongezi kwa kazi kubwa ya kuwawakilisha wananchi katika mashauri yanayohusu ardhi" amesema Mhandisi Sanga.
Aidha, Mhandisi Sanga amesema Mawakili wamekuwa tayari kufanya kazi kwa muda wa mchana baada ya kumaliza kesi katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa mbapo baada ya hapo waliendelea na ratiba ya kusikiliza mashauri katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.
Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini Bi. Stella Tullo amesema kuwa kuanzia mwezi Februari 2025 waliamua kufanya zoezi maalum la kuondosha mlundikano wa mashauri katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, Dodoma ili wananchi wapate haki zao kwa haraka na kuwawezesha kutumia ardhi zao kujiletea maendeleo
Msajili Bi. Stella amesema katika kipindi hiki kifupi kuanzia mwezi wa Februari hadi mwezi Mei wamefanikiwa kumaliza mashauri 423 kati ya mashauri 897 ambayo yalikuwa yanaendelea katika Baraza la Dodoma.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mawakili Kanda ya Dodoma Wakili Mary Munissi ameipongeza hatua ya Wizara ya kuweka mpango maalum wa kupunguza mlundikano wa kesi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba na ameahidi kuwa wataendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kazi hiyo inaendelea kutekelezwa kwa kasi.
0 comments:
Post a Comment