Nafasi Ya Matangazo

May 01, 2025






Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi nchini, Serikali imefanya maamuzi ya kupandisha kima cha chini cha mishahara kwa watumishi wa umma kwa 35.1%.
 
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo katika viwanja vya Bombadia katika Maadhimisho ya Sherehe za Wafanyakazi Dunia (Mei Mosi) ambazo kitaifa zimefanyika mkoani Singida.
 
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema maamuzi ya Serikali kupandisha mishahara yamewezeshwa na kasi ya ukuaji wa uchumi kupanda hadi kufikia 5.5% kwa mwaka, hali iliyochangiwa na wafanyakazi kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
 
Aidha, kwa upande wa wafanyakazi wa sekta binafsi, Rais Dkt. Samia amesema Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara inaendelea na tathmini kwa lengo la kuboresha viwango vya mishahara kwa sekta binafsi.
 
Aidha, Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyakazi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili.
 
Ahadi yetu, tutaendelea kuboresha mazingira ya wafanyakazi ikiwemo maslahi ya wafanyakazi kwa kadiri hali itakavyoruhusu... Kujenga nchi yetu ni jukumu letu sote, hivyo hatuna budi kuimarisha umoja na mshikamano wetu. 

Ili tuweze kujenga vyema Taifa letu ni lazima tulinde amani na utulivu nchini. Kwa namna yoyote ile, tusitoe fursa kwa vyama vya wafanyakazi kutumika kuichafua nchi yetu. Historia ya vyama vya wafanyakazi ni vyama vilivyoleta vuguvugu la uhuru wetu, tusitumike kusaliti uhuru wetu.” amesisitiza Rais Dkt. Samia.

Rais Dkt. Samia amepongeza Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa namna kinavyolinda maslahi ya wafanyakazi kwa weledi kupitia mazungumzo ya utatu ya Serikali, mfanyakazi na mwajiri na ameitaka TUCTA kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro baina ya vyama vilivyopo kwenye shirikisho.
 
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa mwaka huu, Rais Dkt. Samia ameeleza haja ya wafanyakazi kutumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi na kuwachagua viongozi bora watakaolinda na kutetea maslahi yao.
Posted by MROKI On Thursday, May 01, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo