Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani leo Machi 07, 2025 wanawake kutoka Tume ya Madini wamefanya ziara katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Kanda ya Kati Mkoa wa Dodoma na kulipia gharama za matibabu kwa wagonjwa wenye uhitaji maalum ikiwemo vifaa tiba, dawa, operesheni pamoja na kugawa baadhi ya vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwatia moyo wagonjwa hao.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Tume ya Madini, Mkurugenzi wa Idara ya Leseni, Eng. Aziza Swedi amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika tarehe 08, Machi 2025 ambapo imekuwa desturi kwa Tume ya Madini kuwatembelea wagonjwa wenye uhitaji, kuwapatia msaada na kuwatia moyo.
“Tunatambua kila mtu ana mahitaji mbalimbali lakini nashukuru kwa michango iliyotolewa na Tume ya Madini kufanikisha kulipia baadhi ya gharama kwa wagonjwa sita (6) ambao wamekuwa wakipatiwa matibabu lakini wamepata changamoto ya kulipia gharama za kutibiwa” amesema Eng. Swedi.
Ameendelea kusema kuwa, “ Natoa wito kwa wanawake wengine kuwa sisi kama walezi tunategemewa na tuendelee kuwasaidia watanzania wenzetu wenye mahitaji zaidi lakini wanakosa msaada, ambapo kutoa ni akiba ya baadaye pamoja na familia zetu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi ameshukuru Tume ya Madini kwa kujitoa kwa watu wenye mahitaji, “kwa niaba ya menejimenti na utumishi tunashukuru kuja kututembelea, wengine wanajifungua watoto wenye matatizo na gharama kubwa kwa hiyo tunafarijika sana, tunashukuru kwa kutuunga mkono kwa ajili ya kuwasaidia wenye uhitaji
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali watu, Sophia Tangalo ameshukuru wanawake wa Tume ya Madini kwa umoja huo na kusisitiza wanawake wengine kujitokeza ili kuondokana na matatizo yanayowakabili wagonjwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Bahati Sayi ameshukuru kwa jitihada zilizofanywa na wanawake na kusisitiza kuendelea kujitokeza katika kuwasaidia wenye mahitaji maalum na walioshindwa kupewa matibabu kama wanawake wa madini.
Mmoja kati ya wagonjwa walionufaika na msaada huo, Mariamu Mtuki ameushukuru uongozi wa Tume ya Madini kwa jambo walilofanya la kuwapatia msaada na kuongeza kuwa imewatia moyo sana na kujiona wa thamani sana katika jamii.
No comments:
Post a Comment