Mkatab wa Mradi huo ambao umeasisiwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye, ulisainiwa Stesheni ya Magufuli Jijini Dae es Salaam, Januari 29, 2025.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu nchini Burundi Mhe. Mhandisi Nijimbere Egide, alielezea kuwa ziara hiyo imefanywa katika mikoa ambayo mradi wa SGR unatarajiwa kupita ikiwemo Mkoa wa Makamba na Rutana ambapo ameihakikishia TRC kuwa wananchi wako tayari kuupokea mradi huo na kutoa maeneo yatakayo hitajika ili kuweza kurahisisha ujenzi wake.
“Nawahakikishia kwamba sheria ya Burundi, iko vizuri katika utwaaji ardhi ya wananchi na wao wako tayari kwa asilimia mia moja” alisema Mhe. Mhandisi Nijimbere Egide.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu wa Mradi wa SGR kipande cha saba na nane Ndugu Benjamin Mbimbi, alisema kuwa wananchi nchini Burundi watanufaika katika mambo mbalimbali ikiwemo miji kukua kibiashara kutokana na wageni watakao ingia na kutoka, kujengwa kwa shule, hospitali katika maeneo yaliyopitiwa na mradi pamoja na fursa mbalimbali za ajira katika maeneo hayo.
“Mradi unapokuja katika nchi, ni jukumu la wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji ikiwemo sekta ya hoteli na huduma zingine za kijamii ” alieleza Ndugu Mbimbi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa miundombinu kutoka TRC Mhandisi Machibya Masanja, akizungumza katika ziara hiyo ua hivi karibuni alisema, mantiki ya mradi huo ni kuunganisha mgodi wa Msongati na Bandari ya Dar es Salaam na pia kuweka mtangamano wa kibiashara kati ya nchi ya Burundi na Tanzania.
“Tanzania tunawapa huduma wenzetu ambao hawana bahari waweze kutoa bidhaa kutoka kwenye masoko yao kama mgodi wa msongati kuelekea masoko ya nchi za ulaya na nchi zingine” alisema Mhandisi Machibya.
Mhandisi Machibya, aligusia pia gharama za uwekezaji wa mradi huo ambao unagharimu dola za kimarekani bilioni 2.154 ambapo utekelezaji wa mradi huo utachukua miezi 72, miezi 60 ya ujenzi wa reli ikijumuisha miezi 12 ya uangalizi.
“Kipande ni kifupi lakini kutokana na sababu za kijografia nchi ya Burundi kuwa na milima mingi hivyo inahitaji mahandaki na madaraja makubwa” aliongezea Mhandisi Machibya.
Shirika la Reli Tanzania (TRC) litaendelea kutoa elimu na uelewa kwa wananchi wa Burundi wakishirikiana na viongozi wa nchini humo pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu kutoka nchini humo.
No comments:
Post a Comment