Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof.Charles Kihampa,akielezea Sera Mpya ya Elimu kwa waandishi wa habari katika banda la TCU,wakati wa uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 20214,Toleo la 2023 ,hafla iliyofanyika leo Februari 1,2025 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Kihampa, amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la mwaka 2023 ni mkombozi kwa elimu ya Tanzania na kupata vijana wanaoweza kujiajiri na kuajiri wengine na kuongeza uwezo wa ushindani kwenye soko la ajira.
Prof. Kihampa ameyasema hayo kwenye banda la TCU wakati akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 hafla inayofanyika leo Februari 1, 2025 jijini Dodoma.
Amesema kuwa uboreshaji sera na mitaala mbalimbali ya elimu itamwezesha kijana wa Kitanzania ambaye atapata elimu yenye ujuzi na anayeweza kuajirika ndani na nje ya nchi.
" Kitendo cha Rais Samia kuona umuhimu wa kuzindua Sera hiyo ni utashi wa kuboresha elimu ya Tanzania ambayo kimsingi itaweza kupatikana pia kwa njia ya kidigitali na kuwa sawa na mataifa mengine." amesema Prof. Kihampa
Aidha ameeleza kuwa elimu ambayo imeambatana na ujuzi ni elimu ambayo itafanya vijana wengi kuweza kuajirika ndani ya nchi na nje ya nchi huku kijana akitoka shuleni na ufahamu wa vitu vingi tofauti na ilivyokuwa awali.
"Elimu ya Ujuzi itamfanya kijana aliyemaliza elimu yake kuajirika haraka, kitendo hicho kitachagiza kuwepo kwa mageuzi makubwa ya kimaendeleo kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
"Pia upatikanaji wa elimu ya ujuzi ni mkombozi wa wanafunzi wote wa vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu, jambo ambalo ni mkombozi kwa vijana wengi hata kuweza kujiajiri wenyewe badala ya kutumia muda mwingi kufikilia zaidi kuajiliwa" ameeleza Prof. Kihampa.
Hata hivyo ameeleza kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kufungua milango ya majadiliano ya mazungumzo na mataifa mengine na kuweka miongozo mbalimbali ya namna wageni kutoka nje ya nchi wanavyoweza kunufaika na elimu itolewayo katika vyuo vikuu hapa nchini.
Amesema kuwa katika kutekeleza sera hiyo itasaidia vyuo vikuu nchini kudahili wanafunzi wengi zaidi kutoka nje ya Tanzania na hivyo kufanikisha dhana nzima ya umataifishaji.
Pia ameeleza kuwa zaidi ya mitaala 160 ya vyuo vikuu imeboreshwa kwa kuzingatia sera mpya ya elimu na mitaala mingine inaendelea kuboreshwa.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Kihampa,akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo,alipotembelea banda la TCU,wakati wa uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 20214,Toleo la 2023 ,hafla iliyofanyika leo Februari 1,2025 jijini Dodoma.
Picha ya pamoja
0 comments:
Post a Comment