Na. Saidina Msangi na Ramadhani Kissimba, WF- Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema Serikali itaendelea kukiwezesha kibajeti Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) ili kiweze kuwa na miundombinu na rasilimali watu inayokidhi mahitaji ya utoaji wa elimu kwa viwango bora.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema Serikali itaendelea kukiwezesha kibajeti Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) ili kiweze kuwa na miundombinu na rasilimali watu inayokidhi mahitaji ya utoaji wa elimu kwa viwango bora.
Akizungumza kwa niaba ya Mhe. Dkt. Nchemba katika Mahafali ya 38 duru ya kwanza yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya Dodoma, Kamishina wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja alisema ili kuboresha sekta ya elimu nchini Serikali inakusudia kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Dkt. Mwamwaja alisema kuwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa muda mrefu kimekuwa kikipitia kwenye mafanikio makubwa kutokana na mikakati iliyojiwekea hasa ile ya kuwainua wananchi kiuchumi kupitia program mbalimbali ikiwemo uanzishwaji wa Kituo cha Ujasiriamali na Ubunifu (Mipango Enterprenurship and Innovation Centre - (MEI)), pamoja na miradi inayoendeshwa na wabia wa maendeleo wakiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (United Nations Development Programme – UNDP).
Alitumia Mahafali hayo kuushauri Uongozi wa Chuo kupanua wigo wa miradi katika upande wa miradi ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili huduma hiyo iwafikie wananchi wengi zaidi na waweze kunufaika na fursa zinazotokana na huduma hizo.
‘’Aidha, kwa upande wa miradi ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ninawashauri kupanua wigo wa maeneo mengine ya nchi ili wananachi wengi zaidi wanufaike na huduma zenu na kwa kufanya hivyo mtawasaidia kujikwamua kiuchumi’’ aliongeza Dkt. Mwamwaja.
Dkt. Mwamwaja kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe.Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) aliwataka wahitimu na wananchi kwa ujumla kujitokeza na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba,2024,Uchaguzi ambao ni muhimu katika kuimarisha demokrasia na ushiriki wa wananchi katika utawala wa nchi yao.
Awali, akiongea katika Mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Profesa Hozen Mayaya, alisema Chuo hicho kimeendelea kutekeleza majukumu yake ya Kitaaluma kwa mafanikio makubwa ambapo inajivunia kutoa wahitimu waliopata mafunzo ya darasani na mafunzo kwa vitendo jambo ambalo litawajengea umahiri katika nyanja walizosomea.
Aidha, Profesa Mayaya, alisema kuwa pamoja na kuadhimisha Mahafali ya 38, Chuo pia kinatimiza miaka 45 tangu kuanzishwa na kwa kipindi chote hicho Chuo kimepitia mafanikio mbalimbali ikiwemo kuwajengea uwezo wahadhiri wa chuo katika kufanya utafiti, kutekeleza miradi mbalimbali ya tafiti shirikishi kwa lengo la kujenga uwezo kwa Taasisi na Wadau.
‘’Ninapenda kukutaarifu kuwa katika azma yake ya kuwajengea uwezo wahadhiri katika kufanya utafiti, Chuo kimendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya tafiti ambazo zinalenga katika kutatua changamoto za kiuchumi zinazoikabili jamii na Taifa kwa ujumla’’ alisema Pro. Mayaya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Profesa Joseph Kuzilwa alisema kuwa jukumu mojawapo la Baraza la Uongozi wa Chuo ni kuendelea kukisimamia Chuo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Profesa Kuzilwa aliongeza kuwa mafanikio makubwa yanayopatikana Chuo cha Mipango ni kutokana na kuwa na Viongozi wenye weledi mkubwa katika kusimamia na kutekeleza majukumu ya Chuo kwa kuzingatia sheria na Baraza la Chuo litaendelea kuhakikisha Chuo kinatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali.
Mahafali ya 38 duru ya kwanza ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yamejumuisha wahitimu 5,589 kutoka katika programu mbalimbali kuanzia ngazi ya Astashahada hadi shahada ya Umahiri ambapo kati yao wanaume ni 2,455 na wanawake 3,134.
No comments:
Post a Comment