Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kumwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika tarehe 20 Novemba 2024, jijini Harare, Zimbabwe.
Pamoja na ushiriki huo, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ataongoza pia Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaotarajiwa kufanyika siku hiyo hiyo ya tarehe 20 Novemba, 2024.
Mkutano huo, utatanguliwa na Mkutano wa Utatu wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi hiyo utakaofanyika tarehe 19 Novemba 2024, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) atauongoza.
Aidha, Mkutano huo wa Mawaziri utatanguliwa na Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi hiyo ya Siasa (Organ Troika) kitakachofanyika tarehe 19 Novemba 2024 na kuongozwa na Balozi Dkt. Samwel W. Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Kimsingi, Mkutano huo unatarajia kujadili kuhusu masuala ya amani na usalama katika Ukanda wa SADC, na Masuala mengine ya kuimarisha Mtangamano.
0 comments:
Post a Comment