November 11, 2024

NAIBU WAZIRI LONDO AZINADI FURSA ZA KIUCHUMI NCHINI URUSI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo akikaribishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa shirikisho la Urusi, Mhe. Bogdanov Mikhail Leonidovich alipowasili kwa mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri  wa Mambo ya Nje  kutoka nchi za Afrika na Shirikisho la Urusi unaofanyika tarehe 9 hadi 10 Novemba, 2024 mjini Sochi, Urusi
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo amezinadi fursa za mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uwekezaji, biashara na utalii nchini Urusi wakati alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa shirikisho la Urusi, Mhe. Bogdanov Mikhail Leonidovich.
 
Mazungumzo ya viongozi hao yamefanyika tarehe 10 Novemba, 2024 pembezoni mwa Mkutano wa  Kwanza wa Mawaziri  wa Mambo ya Nje  kutoka nchi za Afrika na Shirikisho la Urusi unaofanyika tarehe 9 hadi 10 Novemba, 2024 mjini Sochi, Urusi
 
Pamoja na mauala mengine, wamejadili kuhusu Ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Urusi tangu enzi za Baba wa Taifa Hayati, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na  kuhaidi  kuendelea kuimarisha Ushirikiano huo kati ya nchi hizi mbili.
 
Aidha, kwa upande wake Mhe. Londo ameihakikishai Serikali ya Urusi kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kuhakikisha ushirikiano katika sekta za Utalii, Uwekezaji, Biashara, Kilimo, Afya, Viwanda una imarika na kukua kwa maendeleo endelevu ya watu wake na mataifa hayo kwa ujumla.
 
Vilevile, Mhe. Naibu Waziri Londo ameeleza kuhusu uwepo wa mazingira rafiki ya uwekezaji, fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana nchini na maeneo ya kimkakati ambayo Urusi inaweza kushirikiana na Tanzania ili kuleta tija katika ushirikiano wake. Kadhalika, ametoa rai kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Urusi kuchangamkia fursa nyingi za uwekezaji na masoko zinazopatikana nchini.
 
Naye, Mhe. Leonidovich ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kukuza ushirikiano na Urusi na kuahidi kuwa Urusi imejizatiti kuhakikisha ushirikiano wake na Tanzania unakuwa wenye manufaa makubwa kiuchumi na kidiplomasi kwa pande zote.




No comments:

Post a Comment