Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ametembelea Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Mkoani Iringa ambapo pamoja na mambo mengine amefanya kikao na baadhi ya watumishi wa kituo hicho na kupokea taarifa ya utendaji kazi.
Akizungumza katika kikao hicho, leo Oktoba 7,2024 Mhe. Chana amepongeza utendaji kazi wa kituo hicho huku akisisitiza kuendelea kujiimarisha ili kukuza soko la bidhaa za misitu wanazotengeneza.
“Wakati umefika wa chuo hiki kuwa cha mfano na nawapongeza kwa namna ambavyo mnafanya kazi zenu na ninaahidi Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kuwasaidia ili kuinua soko la bidhaa mnazotengeneza” Mhe. Chana amesisitiza
Aidha, ametoa rai kwa taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kununua bidhaa za samani zinazotengenezwa na kituo hicho ili kukiunga mkono.
Katika hatua nyingine ameilekeza menejimenti ya chuo hicho kujitangaza ili kupanua soko la bidhaa za samani zinazotengenezwa hasa kwa taasisi za Serikali.
Naye, Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu, Berthan Odelo amesema Kituo kimefanikiwa kujenga uwezo wa wajasiriamali wadogo na wa kati ambapo mafunzo ya awali kwa wajasiriamali wadogo 80 yametolewa juu ya mbinu za kuandaa mbao na kuziongezea thamani wakati wa kutengeneza samani na uanzishaji na utunzaji wa kitalu cha miche cha kisasa.
“Kituo kimetoa mafunzo juu ya kinga na udhibiti wa moto kichaa, huduma ya ukaushaji na uchakataji wa mbao, utengenezaji wa mkaa endelevu, kunoa, kunyoosha na kuunga misumeno na uzalishaji wa miche ya kisasa ya miti na kusimamia uanzishaji na utunzaji wa mashamba 15 ya mbegu bora za miti yenye eneo hekari 137 na kufanya Uwezeshaji wa mafunzo na teknolojia za uzalishaji wa nishati mbadala kwa wananchi” amesema.
Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu kilianzishwa mwaka 2016, chini ya mradi wa Panda miti kibiashara – PFP unaofadhiliwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na wizara ya mambo ya nje ya Ufini.
Kituo kinatoa mafunzo mbalimbali ya muda mfupi, ambayo yanalenga kuwaandaa na kuwajengea uwezo wataalamu/wafanyakazi katika mashamba ya miti na Viwanda vinavyochakata mazao ya misitu sambamba uzalishaji wa mbao kwa kutumia teknolojia mbalimbali, uzalishaji wa mkaa na mkaa mbadala, uzalishaji wa samani za maofisini, majumbani, hotelini, uzalishaji wa miche ya miti ya kupanda hasa spishi za mikaratusi na misindano uzalishaji wa mbegu bora za kisasa.
No comments:
Post a Comment