Wajasiriamali wadogowadogo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, wameshukuru uwepo wa michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Morogoro, kwa kuwa imewaongezea vipato vyao.
Kiongozi na Mwamuzi wa zamani wa mchezo wa mpira wa netiboli, Mwajuma Kisengo aliyetokea Jijini Dar es Salaam akiwa na biashara ya nguo za michezo amesema michezo hiyo imetoa fursa ya wajasiriamali kujiongeza na kuleta bidhaa mbalimbali za kuwauzia wachezaji wanaoshiriki kwenye mchezo hiyo
Kisengo amesema mbali na kufanya biashara michezo pia inasaidia kuwaongezea maarifa maana wamekuwa wakifanya utalii wa ndani kwa kutembelea mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, ambayo imechaguliwa kuwa mwenyeji wa michezo hiyo.
“Tunashukuru uwepo wa hii michezo na tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kupenda michezo, tunaomba iendelee kuwepo hata kwa miaka ijayo,” amesema Kisengo.
Naye Hope Chinga kutoka jijini Dodoma akiwa anauza juisi za tende, matunda na lishe kwa ajili ya wenye matatizo ya kiafya, ambazo anawauzia wanamichezo wanaoshiriki SHIMIWI 2024.
Hope ameiomba serikali kuipa michezo hiyo kipaumbele na ifanyike mara kwa mara kwani inasaidia wajasiriamali wadogowadogo waweze kunufaika kwa kuongeza kipato kutokana na biashara watakazowauzia wanamichezo.
Kwa upande wake Samwel Peter kutoka Mwanza naye ameishukuru serikali kwa kufanya michezo kwa watumishi wa umma kwani inasaidia kuimarisha afya zao, na ni ajira, na pia kuwasaidia wajasiriamali wadogowadogo kuongeza kipato chao.
“Nimekuwa nikizunguka sehemu mbalimbali zenye mashindano haya ya SHIMIWI, na ninawashukuru sana wachezaji wa taasisi na wizara kwa kutuunga mkono katika kununua bidhaa zetu tunazouza na kutufanya tupate riziki, kama mimi nimekuja na nguo na raba za michezo, nawashukuru wachezaji kwa kutuunga mkono,” amesema Peter.
Naye Hadija Kihonda mkazi wa Morogoro anayeuza marashi kutoka Dubai ameshukuru maamuzi ya mkoa wa Morogoro kuwa mwenyeji wa michezo hiyo, maana kumewezesha wajasiriamali kuuza bidhaa mbalimbali.
“Mama Samia adumu kwa kuwezesha michezo kufanyika hapa mkoani kwetu, kwani imekuwa manufaa kwenu kwa kuuza bidhaa mbalimbali, tunasema asante Mhe. Rais,” amesisitiza .
Kwa upande wake Moses Mrisho mwenye biashara ya madafu mkazi wa Morogoro maeneo ya Msongeni, ameshukuru uwepo wa michezo ya SHIMIWI kutokana na kufanya biashara kubwa na kupata fedha zinazokidhi mahitaji yake, tofauti na awali, alipokuwa akiuza mtaani pekee.
Mrisho amesema dafu linafaida kubwa mwilini kwa kuwa husafisha kibofu cha mkojo na pia kuponya magonjwa mbalimbali ukiwepo wa UTI.
Naye Fortunatus Felician mjasiriamali kutoka Jiji la Dar es Salaam akiwa na bidhaa za asili na batiki, amesema michezo ya SHIMIWI imekuwa mkombozi kwake, kwani amekuwa akipata riziki kwa kuuza bidhaa zake kwa washiriki wa michezo hii.
Naye Pendo Florian mkazi wa Morogoro anayeuza uji wa ulezi, mhogo na mchele kwa wanamichezo amesema michezo hii imemuinua na kuongeza bidii kwa kuwa maisha ni magumu, na hapaswi kutegemea kuletewa na mwanaume.
No comments:
Post a Comment