October 11, 2024

MGODI MKUBWA WA DHAHABU NYANZAGA-SENGEREMA KUANZA UJENZI MKUBWA JANUARI 2025








⚫️ Utakuwa  mgodi mpya mkubwa katika kipindi cha Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Sengerema
Mradi wa uchimbaji dhahabu wa Nyanzaga-Sengerema unatarajiwa kuanza kazi za awali za ujenzi ifikapo Januari,2025.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 11 , 2024 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde Wilayani Sengerema katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Igalula,Boma na Ibisabageni baada ya kutembelea eneo la Mgodi kwa lengo la kupokea na kutoa maelekezo juu ya kutatua changamoto mbalimbali zilizoibuliwa na wananchi. 

Akielezea kuhusu mpango wa ajira kutoka sehemu ya mgodi, Waziri Mavunde amesema kuanza kwa mradi kunatarajiwa kutoa ajira zaidi ya  1500 na hivyo, ameielekeza Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya kuweka utaratibu mzuri wa kupokea barua za maombi ya ajira kupitia wenyeviti wa vitongoji na kuwasilisha kwa Mtendaji wa Kata ili kupata orodha ya ajira iliyosahihi na uwazi.

Sambamba na hilo, Waziri Mavunde ameielekeza Kampuni ya  Sotta kutumia Mpango wa Ushirikishwaji wa Jamii inayozunguka mgodi (CSR) kama Sheria inavyoelekeza kwa kuwashirikisha wananchi katika uibuaji miradi mbalimbali ya kiuchumi inayotokana na mgodi kama kanuni zinavyoelekeza.

Vilevile, Mhe. Mavunde alibainisha kwamba Serikali ambaye ni mbia wa mgodi huo na kampuni ya Perseus kupitia kampuni ya ubia ya Sotta kwa mara ya kwanza inakwenda kunufaika  kupitia kuongezeka kwa Hisa za Serikali zisizofifishwa (Undiluted Free carried Interest) kutoka asilimia 16 hadi asilimia 20. 

Waziri Mavunde amefafanua kuwa , Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na *Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan* inatambua umuhimu wa wananchi kushiriki katika uchumi kupitia sekta ya madini na hivyo kutoa rai kwa wananchi kuchangamkia  fursa za mauzo ya bidhaa na kutoa huduma migodini kwa kuitaka Tume ya madini kuwajengea uwezo wananchi hao juu ya ushiriki wao kwenye zabuni mbalimbali.

Naye, Mbunge wa jimbo la Sengerema *Mhe.Hamis Tabasamu* amempongeza Rais, *Dkt. Samia Suluhu Hassan* kwa kupeleka kiasi cha shilingi Bilioni 137 za miradi ya maendeleo katika sekta ya Afya , elimu, maji na barabara wilayani Sengerema.  Aidha, Mhe. Tabasamu alimwomba Waziri kuhakikisha mgodi unaanza shughuli zake kwa wakati ili wananchi wa Sengerema wanufaike na kuinuka kiuchumi.

Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya mgodi Kaimu Meneja wa Mgodi wa Sotta, *Bw. Isaac Lupokela* ambaye ni Afisa Mkuu wa Fedha amesema kuwa, mgodi wa Sotta unataraji kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 500, ambao awali ulikuwa udumu kwa miaka 10, na sasa baada ya kuongeza uwekezaji utadumu kwa miaka 15  na kueleza kwamba kwasasa shughuli za uchorongaji wa kina zinaendelea na ifikapo Januari,2025 kazi za ujenzi zitakuwa zimeanza.

Kuhusu fidia kwa waguswa wa mradi, Bw. Lupokela amesema kuwa, mpaka sasa zaidi ya bilioni 20 zimelipwa na idadi ya nyumba 232 zinataraji kujengwa  na kukamilika ifikapo Mwezi Mei, 2025 ikiwa ni moja ya sehemu ya fidia kwa jamii iliyopisha eneo la mgodi.

Akifafanua kuhusu miradi mbalimbali katika Wilaya ya Sengerema, Mkuu wa Wilaya Bi. Senye Ngaga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na kueleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu Wilaya ya sengerema imekuwa ikipokea fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kwamba, ujio wa mgodi wa Sotta utakwenda kuchagiza maendeleo zaidi ya wananchi wa Wilayani kwake.

No comments:

Post a Comment