Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imezindua Bodi ya Ushauri ya kimataifa ya NM-AIST ambayo imeundwa mahususi kwa lengo la kushauri Baraza la Taasisi, ili kufanya elimu ya Tanzania iwe ya Kimataifa hususani katika Nyanja za Sayansi ,Teknolojia na Ubunifu.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi Naibu Katibu Mkuu Sayansi, Teknolojia na Elimu ya juu amesema, kutokana na upekee uliopo katika taasisi hiyo iliyo jikita katika Sanyansi, Teknolojia na Utafiti, wanategemea uwepo wa bodi hiyo utaifanya taasisi izidi kuongeza ufanisi na kufikia hadhi ya kimataifa na kutoa elimu bora kwa wanafunzi watakaokuja kusoma nchini Tanzania, kuzalisha wataalamu watakaoajirika popote duniani ili kukuza uchumi wa nchi.
“Uundwaji wa bodi umezingatia Kimataifa kwa kulenga wajumbe kutoka nchi na mataifa mbalimbali duniani, zilizofanikiwa zaidi katika sekta ya Teknolojia na viwanda ili kuishauri taasisi hii kwani uteuzi wa wajumbe ulizingatia uwezo na ujuzi wa wajumbe na uwezo wa nchi walizotokea katika nyanja za Teknolojia na Viwanda" amesema Prof.Mushi.
Naye Mkuu wa taasisi hiyo, Bw. Omary Issa amesema bodi iliyoundwa ni kwa ajili ya kuishauri taasisi katika kuzalisha teknolojia ambazo zitakuza uchumi wa nchi na kuweza kupandisha hadhi ya NM-AIST katika utoaji nguvu kazi na bunifu zenye tija.
Naye mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo kutoka Korea ya Kusini Prof. Park Ho Koon amesema amefurahishwa kuwa mmoja wa kamati hiyo, na kuahidi kutoa uzoefu alionao wa miaka kumi na sita vyuoni wa kuunganisha daraja lililopo kati ya wanataaluma na viwanda ili kuleta mabadiliko ya viwanda na jamii kwa taasisi, taifa na Afrika kwa ujumla.
Kamati ya Kimataifa ya NM-AIST imeundwa na wajumbe saba kutoka Korea, Itali, Amerika na wenyeji Tanzania na kikao cha kwanza kinafanyika Oktoba 4, 2024, katika kampasi Tengeru Arusha .
0 comments:
Post a Comment