Nafasi Ya Matangazo

September 20, 2024

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya UjenziDkt. Charles Enock Msonde akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa TEMESA Dar es Salaam

Na Neema Macha, - TEMESA Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Enock Msonde ameitaka Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) TEMESA kutafuta mbinu mpya na za kisasa katika ukusanyaji wa mapato.
 
Aidha, amesema kuboresha mikakati ya ukusanyaji wa mapato kwenye vituo kutaifanya wakala kuongeza uwezo wa kifedha na kufanikisha miradi zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
 
Dkt. Msonde, ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea karakana ya TEMESA mkoani Dar es Salaam hivi karibuni, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa ya kumtaka kufuatilia utendaji wa Wakala na kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa viwango vya hali ya juu.
 
Naibu Katibu Mkuu huyo ameitaka  TEMESA mbali na kutafuta mbinu za ukusanyaji mapato lakini kuwa na mifumo bora itakayosaidia kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wateja ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa vivuko.
 
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa kila shilingi inayokusanywa inatumika ipasavyo kwa ajili ya maendeleo ya wakala na wananchi, hii ni fursa nzuri kwa TEMESA kuonyesha ufanisi wake na kujenga uaminifu kwa wananchi. Tunatarajia kuona mabadiliko chanya katika ukusanyaji wa mapato na huduma zinazotolewa,” alisimema Dkt Msonde.
 
Akizungumza na viongozi na wahandisi wa TEMESA, Dkt. Msonde alisisitiza umuhimu wa utekelezaji mzuri wa kazi ili kukidhi mahitaji ya jamii ambapo alitoa wito kwa viongozi wa vituo vyote nchini kujifunza kutokana na mbinu na mikakati inayotumika katika vituo vya Dar es Salaam, akisema kuwa ni fursa muhimu kwa maendeleo ya sekta ya ufundi na umeme.
 
“Nimeongea na baadhi ya madereva na taasisi mbalimbali zinazohudumiwa na TEMESA hapa Dar es Salaam, hasa katika utengenezaji wa magari na wameonyesha kuridhishwa na huduma mnazozitoa,” alisema Dkt. Msonde.
 
Aidha, Dkt. Msonde ameipongeza TEMESA na kuitaka kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa changamoto zinazoikabili, ambapo pia aliwaagiza watendaji wote kuzingatia ubora katika huduma ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuimarisha ufanisi wa shughuli zao.
Posted by MROKI On Friday, September 20, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo