September 26, 2024

ALAF YAJA NA TEKNOLOJIA MPYA YA KUJENGA MAGHALA RUVUMA


KAMPUNI ya ALAF Limited Tanzania imewahakikishia wakazi wa Ruvuma kuwa mradi wa maghala 28 ya nafaka yanayojengwa na Wizara ya Kilimo katika Mkoa huo ni wa aina yake na wenye viwango vya kudumu muda mrefu ambao utamaliza kabisa tatizo la maghala katika mkoa huo.

Akizungumza mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maghala hayo katika eneo la Luhimba- Madaba Songea, Meneja Miradi wa Alaf Limited, Julius Nalitolela aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa hatua hiyo huku akisema kampuni hiyo ambayo inatekeleza mradi huo ambao imekuwa na teknolojia ya kisasa kabisa katika ujenzi huo.

Rais Samia aliongozana na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe na viongozi wengine wa Mkoa wa Ruvuma wakati wa uwekaji wa jiwe hilo la msingi.

“Teknolojia hii inatumika kwa mara ya kwanza kabisa na sisi kama kampuni inayotekeleza mradi huu chini ya Wizara ya Kilimo tuna uhakika hili ni suluhisho la kudumu kwa sababu tumezingatia ubora wa hali ya juu,” alisema.

Alieleza kuwa paa za maghala hayo zinajengwa kwa kutumia bidhaa ya saflock ambayo haivujishi kabisa hasa nyakatia za mvua.

Bidhaa nyingine inayotumika katika mradi huu ni chuma aina ya light gauge ambayo itatumika kujenga ofisi na vyoo. “Ni nyepesi, rahisi kusafirisha, imetengenezwa kwa mfumo wa kompyuta, hakuna mabaki katika eneo la kazi, sio rafiki kwa mchwa, haipati kutu, ni salama kutokana na muundo wake na ujenzi wake ni wa muda mfupi,” alisisitiza.

Naye Meneja Mradi kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Injinia Iman Nzobonaliba, alisema mradi huo ukikamilika utaweza kuhifadhi nafaka zaidi ya tani 28,000.

“Baada ya kukamilika kwa mradi huu ambao una ubora wa hali ya juu suala la uhaba wa maghala ya kuhifadhi nafaka katika Mkoa wa Ruvuma utakuwa historia, “alisema.

Alieleza kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 90 hadi sasa na unatarajiwa kukamilika kabisa ifikapo Novemba mwaka huu.

ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania kwa kutengeneza mabati ya kuezekea nyumba. Ni kampuni iliyoanzishwa mwaka 1960, na inaendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

No comments:

Post a Comment