July 12, 2024

SILLO ASHIRIKI MAZUNGUMZO KATI YA WAZIRI MAKAMBA NA KATIBU MTENDAJI SADC








Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo (Mb) leo Julai 12, 2024 Jijini Lusaka, Zambia ameshiriki mazungumzo yaliyofanywa kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki, Mhe. January Makamba na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Elias Mpedi Magosi.


Katika mazungumzo yao ambayo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC uliomalizika leo Jijini hapa, Mhe. Makamba amempongeza Mhe. Magosi kwa kazi kubwa inayofanywa na Sekretarieti hiyo katika kusimamia utekelezaji wa mipango, itifaki, na mikataba mbalimbali iliyopitishwa au kuridhiwa na nchi wanachama wa SADC.


Kadhalika Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Sekretarieti hiyo na matayarisho yanayoendelea wakati Tanzania ikijiandaa kuchukua Unyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama kuanzia mwezi Agosti 2024.


Viongozi wengine kutoka Tanzania walioambatana na Mhe. Makamba kwenye kikao hicho ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri.

No comments:

Post a Comment