Nafasi Ya Matangazo

July 06, 2024



Na Eleuteri Mangi, WANMM
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatumia mfumo wa kisasa wa kidijiti wa kutoa Taarifa za Sekta ya Ardhi (ILMIS) kurahisisha huduma ya kutoa Hati Miliki za Ardhi kwa wananchi kwa wakati.

Mfumo huo una lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kutoa huduma kwa wananchi tofauti na huduma za awali ambapo kwenye Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) mfumo huo unaendelea kutumika kutoa hati za viwanja katika jiji la Dar es salaam na Dodoma.

Wananchi wenye viwanja jiji la Dar es salaam na Dodoma wamepata fursa ya kuchukua hati zao kwenye banda la Wizara lililopo katika viwanja vya Sabasaba Temeke jijini Dar es salaam, hatua inayompunguzia adha na gharama ya kusafiri kufuata hati zao badala yake watatumia muda huo kufanya shughuli nyingine za maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.

Familia ya Bw. Martin Sintala na mke wake Juliana Lucas wakazi wa mtaa wa Akachube Makumbusho jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa wananchi walipata Hati Miliki ya pamoja ya kiwanja chao kwenye maonyesho hayo.

Wanafamilia hao wamesema wameamua kuwa na hati ya pamoja ya baba, mama na watoto wakiongozwa na msingi wa upendo miongoni mwao hatua inayompa kila mmoja wao haki ya kumiliki ardhi kama mwanafamilia.

Aidha, Rais wa Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Dkt. wa Jakaya Kikwete ametembelea banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kujionea huduma zinazotolewa na Wizara katika maonyesho hayo.

Maonyesho ya Sabasaba 2024 yamefunguliwa rasmi Julai 3, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamona na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Filipe Nyusi na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2024.
Posted by MROKI On Saturday, July 06, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo