Serikali imekipongeza Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi Tanzania (TSIA) kwa kutimiza miaka 20 na kutoa ajira kwa vijana wapatao elfu tatu (3,000) na kuchangia kupunguza wimbi kubwa la vijana wanaojiingiza katika shughuli zisizo rasmi zikiwemo za kiuhalifu.
Hayo yamebainishwa katika Hotuba ya Mgeni Rasmi Mhe. Kassim Majaliwa iliyosomwa kwa niaba na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo (Mb) katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kazi wa 16 wa Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Midland Jijini Dodoma. Tarehe Juni 19, 2023.
"Mmefanya kazi nzuri ya uwekezaji wa ndani katika Sekta ya Ulinzi wa watu na mali zao, nawapongeza kwa kuwa na mahusiano mazuri na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama nimesikia hapa kuwa mnashirikiana vizuri na Jeshi letu la Polisi sanjari na Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji pamoja na changamoto mbalimbali ambazo mmezieleza katika risala yenu niwape hongera kwani bado Chama kinaonekana imara ninaamini hii ni kutokana na uongozi imara wa Chama chenu"
"Wananchi mnaowahudumia, wameweza kuwatumia walinzi wenu kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu wenyewe, hivyo suala la uaminifu na utunzaji wa siri ni jambo muhimu sana na katika kupambana na uhalifu ninaomba tuzingatie Sheria za Nchi hususani sheria za haki za binadamu, kunamazoea ya watu kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaadhibu wahalifu kwa kisingizio cha hasira kali, vitendo hivi vinapingana na dhana nzima ya utawala bora wa sheria" Alisema Mhe. Sillo
Ameeleza kuwa Chama hiko kina dhamana kubwa kwa wateja wao na kinahitaji nidhamu na uvumilivu wa hali ya juu kwa kuangalia namna ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi ili kuleta tija katika utendaji kazi wa kila siku kwani bila kuwa na maslahi mazuri, watendaji wengi hujikuta wakifanya kazi wakiwa wamekata tamaa na hivyo ni rahisi kwao kurubuniwa na kujiingiza katika vitendo vya kiuhalifu pia kumekuwepo na taarifa ya baadhi ya walinzi wa kampuni kujihusisha katika njama za uhalifu wengine wakidiriki kuazimisha silaha kwa kisingizio cha kuporwa.
0 comments:
Post a Comment