Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) inaendelea kufanya tafiti zaidi juu ya madhara na matibabu ya ugonjwa wa ngozi wa Twiga ambao matokeo ya awali yameonyesha maeneo yanayoathirika ya viungio kwenye miguu (magoti) hususan miguu ya mbele, kuna vimelea vya bakteria, virusi na fangasi.
Akizungumza wakati wa ufuatiliaji wa matibabu ya ugonjwa huo katika hifadhi ya Taifa Ruaha, Dkt. Julius Keyyu ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti TAWIRI, amesema ugonjwa wa ngozi wa Twiga uliogundulika katika hifadhi ya Taifa Ruaha mwaka 2000 ni tofauti na ugonjwa wa ngozi wa Twiga katika nchi nyingine duniani " tumefuatilia ugonjwa huu kwa nchi nyingine duniani na kubaini upo tofauti na hapa nchini" amebainisha Dkt. Keyyu
Dkt.Keyyu amesema asilimia 62% ya Twiga waliopo hifadhi ya Taifa Ruaha wana ugonjwa wa ngozi ambao pia, umeonekana kwa kiwango kidogo katika hifadhi za Taifa za Tarangire na Serengeti, na tafiti za awali zimeonesha madhara ya ugonjwa huo ni pamoja na Twiga wenye ugonjwa kutembea kwa kuchechemea, hivyo kushindwa kukimbia wanapofukuzwa na wanyama wawindao pia hutembea umbali mdogo kwa siku, kwa wiki na kwa mwezi ukilinganisha na Twiga wasio na ugonjwa.
Dkt. Keyyu amesema kwa sasa TAWIRI inaendelea na ufuatiliaji wa matibabu ya ugonjwa huo ili kubaini kisababishi asili cha ugonjwa (_primary agent_) na kupata matokeo ya kushauri nini kifanyike ili kudhibiti ugonjwa huu wa ngozi wa Twiga na kuhakikisha mnyama huyu ambaye ni nembo ya taifa anazidi kuwepo.
Ikumbukwe utafiti wa ugonjwa huu wa ngozi wa twiga unatekelezwa chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) uliopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na jukumuu la TAWIRI ni kufanya tafiti .
0 comments:
Post a Comment