Nafasi Ya Matangazo

December 31, 2023

 









Na Happiness Shayo, Handeni.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekagua mradi wa ujenzi wa nyumba katika kijiji cha Msomera Wilayani Handeni kwa ajili ya wananchi wanaohama kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda  Msomera, ikiwa ni awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba hizo.

Mhe. Kairuki amefanya ziara hiyo leo Desemba 31,2023 kwa lengo la kuangalia maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo ambapo zoezi la kuwahamishia wananchi Msomera linaendelea.

Katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoani Tanga Serikali inajenga nyumba 2500 huku nyumba nyingine 1500 zikitarajiwa kujengwa katika kijiji cha Kitwai B wilayani Simanjiro na nyumba 1000 zitajengwa katika kijiji cha Saunyi wilayani Kilindi na kufanya jumla ya nyumba 5000 kwa mradi wote.

“Tulishaendesha zoezi katika awamu ya kwanza kwa ajili ya kuhamisha wananchi kutoka katika eneo la hifadhi ya ngorongoro,tumemaliza vizuri na zaidi ya nyumba 500 ziliweza kujengwa, hivyo tumeanza awamu ya pili ya  kuhamisha wananchi kwa hiari tangu mwezi Julai 2023 lengo ikiwa ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwezi Machi mwaka 2024 tuwe tumekamilisha ujenzi wa nyumba takribani 5000 kwa hapa Msomera, Saunyi na Kitwai B.

Amefafanua kuwa hadi kufikia Desemba 31,2023 zaidi ya nyumba 347 ziko tayari na kwamba ndani ya wiki 2 au 3 ujenzi wa nyumba takribani 1000 utakuwa umekamilika katika block A,B, C na D.

“Tunatarajia ifikapo mwisho wa mwezi wa pili mwaka 2024 zaidi ya nyumba 1559 zilizobaki kwa upande wa Msomera ambazo zitafanya jumla ya nyumba 2559 ziwe zimekamilika “ amesisitiza Mhe. Kairuki.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wenye nia ya kuhama kwa hiari  kufanya hivyo kwani Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ina nia njema ya kuhakikisha inaboresha maisha ya Watanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Albert Msando amewahakikishia wanaohamia Wilayani Handeni kwamba ni sehemu salama sana, kuna huduma za jamii zote na kwamba maisha yao yatakuwa bora zaidi.

Naye, Kamishna  wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Bw. Richard Kiiza amesema Serikali  imeandaa maeneo mazuri kwa ajili ya maisha wananchi watakaohamia Msomera kwa hiari  yatakayowawezesha kufanya shughuli za kiuchumi badala ya maeneo ya Ngorogoro ambayo yanazuiwa na baadhi ya taratibu na kwamba  Serikali inawezesha upatikanaji wa  huduma zote muhimu.

Ziara hiyo  imehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi pamoja na uongozi wa Wilaya ya Handeni, Jeshi la Wananchi pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa.
Posted by MROKI On Sunday, December 31, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo