Mjumbe wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariko akifungua mafunzo kwa watendaji
hao yaliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa watendaji hao yaliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, wakisaini viapo kabla ya kuanza mafunzo.
Mjumbe wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariko, akiwa kwenye picha ya pamoja na
washiriki wa mafunzo kwa watendaji hao yaliyofanyika ukumbi wa mikutano wa
Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
**************
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka Watendaji wa Uboreshaji wa Majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara kuweka utaratibu mzuri utakaoviwezesha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kushiriki katika uboreshaji katika Kata ya Ikoma.
Akifungua mafunzo kwa
watendaji hao yaliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya
Rorya, Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariko
alisema vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka mawakala katika uboreshaji huo.
Aliwataka watendaji hao
kuvishirikisha vyama vya siasa katika masuala yote ambayo wanastahili
kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yao
katika uboreshaji huo.
“Niwakumbushe kuwa, vyama vya
siasa vinaruhusiwa kuweka mawakala katika vituo vya uandikishaji. Nitumie
nafasi hii kuwasisitiza kuweka utaratibu mzuri utakaoviwezesha vyama vya siasa
na wadau wengine wa uchaguzi kushiriki kikamilifu katika zoezi hili” alisema
Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariko.
Mjumbe huyo wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi alitoa wito kwa watendaji hao wa uboreshaji wa majaribio
kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Maelekezo ya
Tume watakayopewa.
“Vilevile mhakikishe mnasimamia utunzaji wa vifaa vyote vitakavyotumika katika zoezi hili kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa” aliongeza Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariko.
Mafunzo hayo kwa watendaji wa
uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unajumuisha Mratibu
wa Uandikishaji wa Uchaguzi wa Mkoa wa Mara, Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la
Rorya, maafisa waandikishaji wasaidizi, maafisa ugavi, maafisa TEHAMA na
maafisa wanaoshughulikia masuala ya uchaguzi katika Jimbo la Rorya.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
itafanya uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika
Kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara na
Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa
Tabora, kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
“Vilevile mhakikishe mnasimamia utunzaji wa vifaa vyote vitakavyotumika katika zoezi hili kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa” aliongeza Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariko.
No comments:
Post a Comment