Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa katika utekelezaji wa Dira ya 2030 yenye kueleza kuwa, “Madini ni Maisha na Utajiri, Tume imejipanga kuboresha usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na kuendelea kutenga maeneo yaliyofanyiwa utafiti wa kijiolojia kwa wachimbaji wadogo ili uchimbaji wao uweze kuwa na tija pamoja na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa watanzania kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini nchini.
Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Novemba 10, 2023 kwenye kipindi cha Goodmorning kilichorushwa mubashara na kituo cha Televisheni cha Wasafi chenye lengo la kuelezea mikakati ya Taasisi za Wizara ya Madini kwenye utekelezaji wa Dira ya 2030 yenye lengo la kuimarisha Sekta ya Madini.
Amesema kuwa utekelezaji wa Dira hii katika Sekta ya Madini inawalenga zaidi wachimbaji wadogo wa madini ambao wamekuwa wakiwekeza lakini manufaa yamekuwa si ya kuridhisha kutokana na kutokuwa na taarifa za kutosha za utafiti za madini na teknolojia duni kwenye uchimbaji wa madini.
Amefafanua kuwa Tume itaendelea kuimarisha usimamizi katika shughuli za madini kwa kutenga maeneo yenye taarifa za kijiolojia yaliyofanyiwa tafiti ili kuweza kunufaika na rasilimali hizo sambamba na kuandaa Mpango Kazi utakaolenga kusimamia maeneo ya elimu za ugani; kuboresha mfumo wa utoaji wa leseni; ukaguzi migodi na mazingira; usimamizi wa masuala ya afya na usalama mahala pa kazi pamoja na kuimarisha mifumo ya makusanyo ya maduhuli.
Akielezea mikakati iliyowekwa na Tume ya Madini kwenye utekelezaji wa Dira ya 2030, hususan kwenye ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini Mhandisi Samamba amefafanua kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wamiliki wote wa migodi kuhusu kutoa kipaumbele kwa huduma na bidhaa zote zinazotolewa na watanzania pamoja na kuandaa namna bora ya kuingia ubia kati ya kampuni za watanzania na kampuni za nje na uwepo wa utekelezaji wa Sheria ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini pamoja na Urejeshaji wa Huduma kwa Jamii.
Ameendelea kufafanua mikakati mingine kuwa ni pamoja na uwepo wa mfumo wa usimamizi wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini na kutoa elimu kwa wakandarasi wote ili kuwaandaa kushiriki katika mikataba yenye thamani kubwa kwa lengo la kuchangia ajira na kuongeza uzalishaji wa bidhaa nchini.
Hata hivyo ameeleza mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuhakikisha kampuni za madini zinaboresha huduma za jamii kwenye vijiji vinavyozunguka migodi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, maji, vituo vya afya na shule.
Tume ya Madini ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Madini ambayo iliundwa kutokana na Sheria ya Madini Sura ya 123 na ilianza utekelezaji wa majukumu yake Mwezi Aprili, 2018 kwa kutekeleza majukumu 22, ambapo jukumu kubwa ni kusimamia na kudhibiti Sekta ya Madini nchini.
No comments:
Post a Comment