November 10, 2023

MRADI WA RELI YA KISASA YA UMEME (SGR ) MBIONI KUKAMILIKA JANUARI-2024







Mradi wa reli ya kisasa ya umeme (SGR)  unatarajia kukamilika Januari mwakani ambapo unahusisha kipande cha kutoka Morogoro, Dodoma na Makutupora.

Hayo yamebainishwa  hii leo Novemba 10, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ndani ya Jiji hilo ambapo ametembelea mradi wa Reli ya kisasa ya umeme (SGR ) na Mji wa Serikali Mtumba (Magufi City). Amesema  ameridhishwa na mradi huo ambao mpaka sasa kwa mujibu wa mkandarasi umefikia asilimia 95.7 kukamilika.

Amesema kupitia mradi huo utaongeza kasi ya maendeleo na fursa za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kupendezesha mandhari ya jiji la Dodoma ambapo pia ni fursa ya utalii hivyo amewataka wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi 

Aidha, amewaagiza wasimamizi wa mradi  ambao ni  Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi huo juu ya kuchukua tahadhari ikiwemo ya usalama wa mifugo na watu katika eneo la miradi kwa kuhakikisha wanapita maeneo husika ambayo yamewekwa kwa ajili ya matumizi yao  ikiwemo vivuko kwa ajili ya usalama.

Akiwa katika Mji wa Serikali Mhe.Senyamule  amekagua  maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Wizara na ameonyesha kuridhishwa na kasi ya maendeleo ya miradi hiyo.

Hata hivyo, amewaagiza wakandarasi wa miradi hiyo kuongeza kasi ya ujenzi kwa kuzingatia ubora wa majengo hayo ili kufikia Januari 2024 iwe imekamilika huku akiendelea kusisitiza suala la kupanda miti ili kutunza mazingira.

"Tumekuja leo kutembelea na kuona maendeleo ya miradi ambayo pia ni kivutio cha Utalii ndani ya Jiji letu ambayo yapo katika hatua tofauti tofauti, kuna yaliyofikia asilimia 75 hadi 78 na kuna ya asilimia 99.9, kuna ya asilimia 53 ambapo ya asilimia 75-78 yalitakiwa yawe yamekamilika .

"Nitoe wito kwa wakandarasi waliopata fursa za kujenga, hakikisheni mnatimiza wajibu wenu, punguzeni sababu nyingi kwani tuna amini Changamoto zipo ila  tatueni kwa haraka ili kukamilisha majengo haya kwa wakati husika " Ameeleza Mhe. Senyamule 

Kwa Upande Wake, Meneja wa Ujenzi (TBA ) Injinia Manasseh Shekalaghe, amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watasimamia wakandarasi kwa ukaribu zaidi ili ikifika Januari watumishi wote waweze kuhamia Mtumba .


Ziara hiyo imehusisha kutembelea maendeleo ya mradi wa Reli ya kisasa ya umeme ( SGR) ambapo ametembelea katika jengo la abiria Mkonze , karakana na kituo cha kushushia mizigo Ihumwa jijini Dodoma. Kwenye Mji wa Serikali ametembelea Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Utumishi, ziara hii imekua ni mwendeleo wa Mkuu huyo  kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment