Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bi. Giveness Aswile akielekeza jambo kwa BVR Kit Operator Viola Ginithone Swai na David Enock katikati namna ya kukwepa mwanga wa jua kwa vifaa vinavyotumika kwenye zoezi hilo wakati alipotembelea kituo cha Mtaa wa Kalingonji kata ya Ng'ambo.
Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bi. Giveness Aswile akielekeza jambo kwa Adam Mkina Mkurugenzi wa Tume ya ya Taifa ya Uchaguzi Ofisi ya Zanzibar wakati walipotembelea katika moja ya vituo vya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwenye kata ya Ng'ambo mkoani Tabora.
Bi. Leila Muhaji Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Habari kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi akifurahia jambo huku akiwa na mtoto wa mmoja wa wapiga kura waliofika kwenye kituo cha Tuktuk kata ya Ng'ambo ili kujiandikisha.
Baadhi ya wananchi waliofika kwenye kituo cha Tuktuk kwa ajili ya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura katika kituo cha Tuktuk kata ya Ng'ambo mkoani Tabora.
***************
Zoezi la Uboreshaji wa Majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura lililoanza tarehe 24, Novemba , 2023 katika Kata za Ng'ambo, halmashauri ya manispaa ya Tabora , mkoani Tabora na Kata ya Ikoma , halmashauri ya wilaya ya Rorya mkoani Mara, kesho tarehe 30, Novemba 2023 linakamilika.
Akizungumzia kuhusu zoezi hilo, Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bi. Giveness Aswile ametoa wito kwa wananchi wanaotaka kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na wanaotaka kujiandikisha upya na wale wenye taarifa za kuondoa kwenye daftari watu waliokosa sifa au kufariki kuitumia siku ya kesho ya tarehe 30 Novemba ili kujiandikisha ama kuboresha taarifa zao.
"Hii ni nafasi ya pekee kwenu kushiriki katika zaezi hili muhimu na pengine nitumie nafasi hii kuwashukuru wadau wote vikiwemo vyombo vya habari, vyama vya siasa ambavyo vimefanikiwa kuweka mawakala katika vituo vya kujiandikisha na kuwahamasisha wananchi ama wafuasi wao kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kujiandikisha".Amesema Aswile
Pia, amevishukuru vyombo vya habari ambavyo vimekuwa bega kwa bega na Tume ya Uchaguzi kuanzia mwanzo wa zoezi hili wakati wa mafunzo, na mikutano ya wadau Dar es Salaam, " Tunawashukuru sana kesho wasisahau kujitokeza kwenye vituo, hii ni nafasi yao haitajirudia tena baada ya kesho.
Zoezi la uboreshaji wa majaribio wa Daftari la kudumu la wapiga kura katika kata za Ng'ambo, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Ikoma Manispaa ya Wilaya ya Rorya linatarajiwa kukamilika kesho alhamisi Novemba 30, 2023 saa 12.00 jioni baada ya kufanyika kwa takriban wiki moja.
No comments:
Post a Comment