Afisa TEHAMA Mkuu kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) Bw. Lazaro Madembwe (kushoto) akijadiliana jambo na Luphingo Jafari Mwasalujoja Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Tehama NEC wakati alipotembelea vituo vya kuboresha daftari la wapiga kura katika kata ya Ng'ambo mkoani Tabora na kukagua mifumo ya tehama namna inavyofanya kazi katika zoezi hilo leo Novemba 26,2023.
BVR Kit Operator Bw. Mohammed Ally Chilongani akimpiga picha kwa kutumia Kishikwambi Mpiga kura Salvatory Rwakajende mkazi wa kata ya Ng'ambo ili kukamilisha zoezi la kujiandikisha katika kituo cha Kaze Hill Sekondari kata ya Ng'ambo mkoani Tabora.
BVR Kit Operator Bw. Mohammed Ally Chilongani akimchukua alama za vidole kwa kutumia Kishikwambi Mpiga kura Salvatory Rwakajende mkazi wa kata ya Ng'ambo ili kukamilisha zoezi la kujiandikisha katika kituo cha Kaze Hill Sekondari kata ya Ng'ambo mkoani Tabora.
Said Yusuf Shango BCR Kit Operator kituo cha Shule ya Sekondari Tabora Girls akichukua taarifa za Jenifa Samwel Mwanafunzi wa shule hiyo ambaye amefikisha umri wa miaka 18 wakati alipojiandikisha kuwa mpiga kura mpya wa kituo hicho.
Wanafunzi wa Tabora Girls ambao wametimiza miaka 18 wakisubiri kujiandikisha kama wapiga kura wapya katika kituo cha kuboresha daftari la wapiga kura cha Sekondari ya Tabora Girls.
**************
Na Mwandishi wetu,Tabora.
Tume ya Taifa ya uchaguzi(NEC) imeboresha vifaa vya uandikishaji na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kutoka kwenye BVR kubwa iliyokuwa na kompyuta ambayo ilikuwa inabeba taarifa za wapiga kura pekee hadi kwenye Kishikwambi ambacho kinabeba taarifa zote za wapiga kura ikijumuisha vifaa vingine kama kamera na (Document Scana).
Hayo yamebainishwa na Afisa TEHAMA Mkuu kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) Bw. Lazaro Madembwe, wakati alipokuwa akielezea mifumo ya tehama ya BVR na OVRS katika Kituo cha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Shule ya Sekondari ya wasichana Tabora iliyopo Kata ya Ng'ambo Mkoani Tabora.
Amesema katika uboreshaji wa majaribio Tume inatumia teknolojia ya (Biometric) kuandikisha wapiga kura,ambapo huchukua alama za vidole ili kuweza kuwatambua wapiga kura walioandikishwa zaidi ya mara moja na kuondoa taarifa za waliojirudia ambazo ziko kwenye daftari.
"Teknolojia hii ilitumika kwa mara ya kwanza kwa uandikishaji mwaka 2015 na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2019 na 2020 na vifaa vilivyotumika ilikuwa ni BVR ambayo ilikuwa na Laptop na Camera ambavyo vilikuwa vinakaa tofauti tofauti lakini kuelekea uboreshaji unaofanyika sasa vifaa vyote vinakaa kwenye Kishikwambi ambapo unaskani Nyaraka na kupiga picha kwa kutumia kishikwambi", amesema Madembwe.
Amesema Tume imejitahidi sana kupanua wigo wa huduma hapo awali mpiga kura ilikuwa ni lazima afike kituoni kwa ajili ya kuboresha taarifa zake, lakini hivi sasa mpiga kura anaweza kuanzisha mchakato wa awali wa kuboresha taarifa zake kupitia kwenye simu janja au kopyuta iliyounganishwa na intaneti na baada ya hapo atapokea ujumbe mfupi wenye kumbukumbu namba ukimtaka kufika kituoni kwa ajili ya kukamilisha taarifa zake.
Mfumo huu unaendeshwa kwenye programu wezeshi ambayo ni (Android) ukilinganisha na mwaka 2015,2019 na 2020 ilikuwa inaendeshwa na (Windows) , programu ya Sasa ni nyepesi na ina uwezo wa kuchakata taarifa za wapiga kura kwa haraka zaidi.
Ameeleza kuwa vifaa vipya vinamanufaa yafuatayo vina uzito mdogo wa kilo 15 ukilinganisha na vya awali ambavyo vilikuwa na uzito wa kilo 35, hivyo vinabebeka kwa urahisi na vinarahisisha shughuli za usafilishaji.
"Walengwa wa zoezi hili ni watanzania wote walioandikishwa hapo awali ambao wamehama kata, waliopoteza au kadi zao kuharibika na wale wote wanaotaka kuboresha taarifa zao, Watanzania wote wenye sifa ya kuandikishwa ya kuwa wapiga kura na ambao hawakuandikishwa hapo awali, ni watanzania wote ambao wametimiza miaka 18 ifikapo siku ya uchaguzi mkuu 2025", amesema Madembwe
ambapo ameongeza kuwa mfumo huo umeboreshwa na una uwezo wa kudhibiti waombaji wote ambao watataka kuandikishwa wakati hawajafikisha umri wa miaka 18.
Aidha, ameeleza kuwa katika uboreshaji huu tume imekuja na njia mpya ya uboreshaji kwa mtandao mfumo huo unawawezesha wapiga kura kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zao kwenye mtandao hivyo wanatakiwa waingie kwenye tovuti ya Tume www.nec.go.tz na kubonyeza kitufe kilicho andikwa boresha taarifa za mpiga kura au atabonyeshwa anwani ya ovrs.nec.go.tz na dilisha lenye vipengele vitatu litatokea na kufuatia na utaratibu unaofuata.
Naye Msimamizi wa BVR Kata ya Ng'ambo Kituo cha Masempele, Mwatano Gervas, amesema kuwa zoezi linaendelea vizuri kwani wapiga kura wote wanaofika katika Kituo hicho wanafuata taratibu zote za uandikishaji.
"Mpiga kura akifika katika Kituo hiki kwanza naangalia taarifa zake ili kujua amekuja kwa ajili ya nini, kama kujiandikisha upya katika daftari la wapiga kura au kumfuta mpiga kura ambaye hana sifa ikiwemo aliyefariki"
Amesema kuwa kama mtu amekuja kujiandikisha upya utaratibu huwa wanamuuliza kama ana namba ya NIDA, kama anayo anaingiza namba ya NIDA katika mfumo kwa ajili kupata taarifa zote ambazo zinampa fursa ya kuendelea katika hatua nyengine.
"Kama hana namba ya NIDA anachukua taarifa zake binafsi ikiwemo majina yote, uraia, umri, jinsia, kazi yake, sehemu anapoishi, kupiga picha, kuweka alama ya vidole,
baada ya kupata taarifa zote tunachapisha na kumpatia kitambulisho chake cha mpiga kura ili aendelee na shughuli zake" amesema Mwatano.
No comments:
Post a Comment