Dar es Salaam. Tarehe 2 Novemba 2023: Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya Visa inayoongoza katika mfumo wa malipo ya kidigitali, imezindua kampeni yake ya ‘Tisha na Tembocard Tukakiwashe AFCON’ inayohamasisha matumizi ya kazi zake za TemboCard Visa, ambapo wateja nane watakaofanya miamala mingi zaidi watapelekwa nchini Ivory Coast kushuhudia mashindano ya TotalEnergies CAF Africa Cup of Nations (AFCON) 2024.
Kampeni hiyo ambayo ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na Benki ya CRDB kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidigitali ilizinduliwa Ijumaa jioni jijini Dar es Salaam na itadumu kwa miezi mitatu mpaka Januari mwakani.
Akiongea katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ameipongeza Benki ya CRDB na kampuni ya Visa kwa kuanzisha kampeni hiyo aliyosema imekuja wakati muafaka ambapo sio tu itasaidia kupunguza matumizi ya fedha taslimu bali itahamasisha michezo miongoni mwa Watanzania.
“Mwaka huu timu yetu ya Taifa imefuzu kushiriki Fainali za AFCON 2024 zitakazofanyika nchini Ivory Coast, hivyo kampeni hii inatoa fursa kwa mashabiki kwenda kuishangilia. Nawapongeza sana Benki ya CRDB na kampuni ya Visa kwa kuja na kampeni hii madhubuti ambayo itatoa fursa adhimu ya watu kushuhudia fainali za AFCON,” amesema Msigwa.
Katibu Mkuu huyo amesema washindi wa kampeni hii watapata nafasi ya kwenda kushuhudia fainali ya michuano hiyo itakayohudhuriwa na mashabiki na viongozi wa michezo kutoka sehemu mbalimbali duniani watakaoenda kujionea vipaji vya vijana wa Kiafrika.
Msigwa aliongeza kwamba pamoja na kampeni ya “Tisha na TemboCard Visa Tukakiwashe AFCON” kuhamasisha michezo, pia inaunga mkono juhudi za serikali katika kukuza uchumi wa kidigitali.
"Uchumi wa kidigitali unahitaji njia mpya za malipo ambazo hazimlazimu mtu kutembea na fedha taslimu. TemboCard Visa inarahisisha malipo hayo kupitia majukwaa tofauti ya ndani hata kimataifa,” amesema.
Afisa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema "tunatambua upendo wa Watanzania walionao kwenye mpira wa miguu. Tunaamini kuwapa fursa hii ya kushuhudia fainali za AFCON 2024 kutawaongezea ladha isiyosahaulika.”
Raballa amesema washindi 8 watakaopata nafasi hiyo watachukuliwa miongoni mwa watumiaji wa TemboCard Visa watakaofanya miamala isiyopungua 30 kwa mwezi sawa na wastani wa muamala mmoja kila siku. Amesisitiza kuwa nafasi za kushinda zipo wazi kwa wateja wote zaidi ya milioni nne pamoja na wapya watakaojiunga na huduma za benki yao na kutumia TemboCard Visa kufanya malipo.
Salma Ingabire, Meneja mkazi wa Visa Tanzania amesema “kama mtoa huduma pekee wa huduma za malipo pekee wa TotalEnergies CAF AFCON, Visa tunafurahi kuingia ubia na Benki ya CRDB ili kuwatuza wateja watakaobahatika kwa kuwapa nafasi ya kushuhudia timu bora za Afrika zikicheza.
Washindi wa kampeni hii watalipiwa nauli ya safari yao ya kwenda Abidjan, malazi katika hoteli ya kifahari, tiketi za daraja la juu (VIP) za kushuhudia mchezo wa fainali, kuhudhuria matukio maalum na vingine vingi ambavyo bila shaka vitawaachia kumbukumbu isiyofutika.
Mbali na kushinda safari hiyo, wateja watakuwa na fursa ya kushinda zawadi nyingine ikiwemo seti ya sofa na vifaa vya kielektroniki mfano runinga na friji. Ili kushinda, amesema wateja wanaweza kutumia kadi zao kulipia bidhaa wanapozinunua dukani au sokoni, kwenye vituo vya mafuta, hotelini, wanaponunua tikiti au kulipia huduma.
0 comments:
Post a Comment