Nafasi Ya Matangazo

October 22, 2023









Na Wizara ya Madini, Dar  Es Salaam.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini kwa mara nyingine imeweka Historia ya kuwa Nchi ya Kwanza Barani Afrika kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Sita (6) wa Kimataifa wa Wakandarasi waliowekeza kwenye Madini yanayopatikana Chini ya Sakafu ya Bahari Kuu ambapo nchi inapata fursa ya kujifunza kuhusu utafiti, uvunaji na uendelezaji wa rasilimali hiyo.

Hayo yamebainishwa na  Naibu  Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa  wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo wa Siku Tatu  ulioanza  leo tarehe Oktoba 22, 2023 jijini Dar es Salaam na utaendelea  hadi Oktoba 24, 2023  huku ukitarajiwa  kufungwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Kassim Majaliwa.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Kiruswa amesema umelenga kuwafahamisha washiriki kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa katika maandalizi ya kuandaa Kanuni zitakazotoa mwongozo wa namna dunia itakavyonufaika na uvunaji wa rasilimali hiyo  inayopatikana katika sakafu iliyo chini ya bahari  kuu.

Ameongeza kwamba, pamoja na mambo mengine mkutano huo unatarajia kujadili  ajenda mbalimbali kuhusu masuala ya utafiti, uchimbaji, utunzaji wa mazingira yaliyo chini ya sakafu ya bahari kuu ikiwa ni kuendelea na utekelezaji wa  Article 145 ya UNCLOS Umoja wa Mataifa na makubaliano ya mwaka 1994 kuhusu shughuli za uchimbaji wa madini kwenye sakafu ya bahari.

‘’Nchi  wanachama  wa umoja wa Mataifa zinaandaa kanuni zitakazosimamia uvunaji wa rasilimali hizo kutokana na nchi nyingi duniani kuwa na wasiwasi kuhusu madhara ya kimazingira  yanayoweza kusababishwa na shughuli za uchimbaji wa madini haya. ‘’ Kimsingi uchimbaji wa madini haya hauwezi kuharibu mazingira ya bahari bali madini haya yanachotwa kwa kutumia kifaa kiitwacho “collector”  tu na kuletwa juu ya ardhi,’’ amefafanua Dkt. Kiruswa.

Akizungumza ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama  wa umoja huo amesema ni nafasi kwa Tanzania kuendelea kujifunza  mambo mbalimbali  yanayohusu rasilimali madini iliyo chini ya sakafu ya bahari ikiwemo kutafiti, kuvuna na kuiendeleza ili kunufaika ipasavyo na rasilimali hiyo ikiwa ni moja ya maeneo muhimu wa Uchumi wa  Buluu.

Ameongeza kwamba, huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuendeleza rasilimali madini hususan madini muhimu na mkakati na kwa kuzingatia *Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri* ambayo inalenga kufanya utafiti wa kina kwa kutumia ndege angalau kufikia asilimia 50 ya eneo zima la nchi ifikapo mwaka 2030 ili hatimaye madini hayo yaweze kuongeza tija zaidi katika uchumi   na mchango wa sekta ya Madini katika maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Kimataifa ya Usimamizi wa Madini yanayopatikana chini ya Sakafu ya Bahari Kuu (International Seabed Authority – ISA) Dkt.  Marie Bourrel- MacKinnon  ameipongeza Tanzania kuonesha dhamira ya uendelezaji wa madini hayo na kusema kwamba ushiriki wake katika  mkutano huo utaisaidia  kufanya maamuzi sahihi juu ya matarajio yake ya baadaye. Pia, ameongeza kuwa, mikutano kama hiyo inatoa fursa ya muhimu ya wanachama kujadili kwa kina na kutafakari namna bora  zitakazowezesha kutoa uwiano sahihi na wa kutosha kwa maslahi ya wote.

 Amesisitiza kuwa, wakandarasi hao wa madini yaliyo chini ya sakafu ya bahari  kuu wanapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria na Kanuni zinazoongoza katika hatua mbalimbali za  utafutaji wa madini hayo.

Awali, akizungumza katika ufunguzi huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema Tanzania bado haina ujuzi na teknolojia za kutafiti na kuchimba madini yaliyochini ya sakafu ya bahari kuu hivyo, ushiriki wake na uwenyeji wake katika mkutano huo utaisaidia kujifunza, kupata ujuzi na kujengewa uelewa wa namna ya kuendeleza madini hayo.

Aidha, ameeleza kuwa, mkutano huo ni wa manufaa kwa Tanzania kwa kuwa utaiwezesha kujenga na kuimarisha mahusiano yatakayoisaidia kuendeleza rasilimali hiyo.

Kwa upande wa Tanzania,  mbali  na ushiriki wa  viongozi na wataalam kutoka Wizara, Taasisi zake, pamoja na taasisi  nyingine za umma,  pia, umehudhuriwa na Mwakilishi wa Kudumu wa  Serikali kwenye Umoja wa Tanzania , Mhe. Balozi Hussein Kattanga.

Tanzania inashiriki ikiwa ni miongoni mwa nchi 169 wanachama wa Mamlaka ya Kimataifa ya Usimamizi wa Madini hayo (ISA)  ambayo iko chini ya Umoja wa  Mataifa  yenye makao makuu yake  Kingston nchini Jamaika.

 Mkutano wa Sita umeshirikisha watu binafsi, na wawakilishi kutoka wakandarasi 15   huku wengine 16 wakishiriki kwa njia ya mtandao.

Mkutano huo hufanyika kila mwaka ili kuhakikisha usimamizi mzuri wa shughuli zote za utafiti, uchimbaji na utunzaji wa mazingira yazingatiwa. Hadi kufikia sasa kuna wakandarasi wapatao 31 wa nchi zinazodhamini kutoka Ulaya, Amerika, Asia na Karibian ambazo zinaendela kutekeleza shughuli za utafiti wa madini aina ya Polymetalic Manganese Nodules (PMN), Sulphide na madini mengine yanayopatikana chini ya sakafu ya bahari ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa teknolojia za kisasa.

Aidha, mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu isemayo *Kuimarisha mahusiano na uwajibikaji katika usimamizi warasilimali za madini yaliyopo chini ya sakafu ya bahari kuu*
Posted by MROKI On Sunday, October 22, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo