Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID) limetoa msaada wa Sh 229,592 176, kwa Taasisi ya Wanyamapori Afrika (AWF) kwa ajili ya mradi wa ‘Tuhifadhi Maliasili’ wenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi kuzunguka ushoroba wa Manyara Ranchi wilaya Monduli mkoani Arusha.
Vilevile, mradi huo unatasidia kuwaongezea wananchi hao uwezo na utalaamu wa kushiriki shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na mazingira katika eneo hilo.
USAID imetoa fedha hizo kupitia Taasisi ya Utafiti (RTI) ambayo itakuwa msimamizi mkuu kufadhili mradi huo ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Julai 8, 2022.
Mratibu wa AWF Tanzania, Pastor Magingi anasema msaada huo wa fedha utaongeza idadi ya vijiji vitakavyonufaika na mradi wa Tuhifadhi Maliasili ulipo katika ushoroba unaounganisha hifadhi za wanyamapori za Manyara na Tarangire (Kwa Kuchinja Wildlife Corridor) kutoka viwili hadi vitano.
Anasema vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni Esilalei, Naitolia, Mswakini Juu, Makuyuni na Oltukai vyote vikiwa wilaya ya Monduli mkoani Arusha. Kabla ya ufadhili huo vijiji vilivyokuwa vikinufaika ni Esilalei na Oltukai.
Magingi anasema mradi wa Tuhifadhi Maliasili una lengo la kuwainua kiuchumi wananchi wa vijiji hivyo ambao ni wafugaji wa mifugo ili washiriki kikamlifu katika uhifadhi endelevu wa wanyamapori na mazingira katika eneo hilo.
Mradi utaendeleza kazi ambayo imekuwa ikifanywa na AWF eneo la Manyara Ranch kupitia mradi wake wa Kuboresha Ufugaji ukiwa na lengo la kuongeza thamani ya mifugo yao na kuwapatia masoko ya maziwa.
Mradi utahakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo hususan wanawake, vijana na makundi maalumu wanafaidi matunda na fursa zitakazopatikana kwenye maliasili yao.
Magingi anasema kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili wananchi wa vijijini wanufaika watatafutiwa masoko ya maziwa Arusha mjini na kuikaribisha sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji katika uzalishaji wa maziwa kama shughuli kuu ya kiuchumi.
Taasisi ya Wanyamapori Afrika yenye makao makuu yake nchini Marekani imekuwa ikifanya kazi nyingi nchini ikiwamo kudhibiti ujangili wa wanyamapori, kufanya kazi na wananchi na serikali kulinda vyanzo vya maji na kulinda shoroba za wanyara.

No comments:
Post a Comment