Mkurugenzi wa Kampuni ya Rabbit Republic ambaye ni mfugaji wa sungura kutoka Kenya, Moses Mutua (kulia) akielezea mipango yake ya kuzanzisha machinjio ya kisasa ya sungura hapa nchini, wakati wa hafla ya Kampuni ya Namaingo kugawa sungura kwa vikundi 20 vya wajasiriamali, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Donald Bombo,Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo, Ubwa Ibrahim na Meneja wa Mradi wa Sungura, Amos Misinde.
********************
Na Richard Mwaikenda;Kamanda wa Matukio Blog
WAKATI Tanzania ikijielekeza katika uchumi
wa viwanda, mpango wa ujenzi wa machinjio ya kisasa ya sungura yatakayogharimu
sh. milioni 100 utaanza mapema mwakani, ukiratibiwa na Kampuni ya Rabbit Republic.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Moses Mutua
alisema hayo wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa miradi ya sungura kwa
wajasiriamali uliofanywa na Kampuni ya Namaingo Business Agency jijini Dar es
Salaam wiki iliyopita.
Mutua ambaye ni mfugaji wa sungura kutoka
nchini Kenya, alisema uamuzi wa kujenga machinjio ya sungura unatokana na kuongezeka kwa mwamko wa
wananchi kufuga sungura.
Alisema awali, mradi huo ulihusisha
kusafirisha sungura hai hadi Kenya, lakini ongezeko la watu wanaohitaji
kujishughulisha na biashara hiyo limesababisha kuwapo haja ya kujenga machinjio
hayo.
Alisema nia na uthubutu wa serikali ya Rais
JohnMagufuli kuwaondoa wananchi wanyonge katika
umasikini, ni miongoni mwa mambo yaliyomsukuma kufikia uamuzi huo.
"Machinjio hayo yatakayojengwa Dar es
Salaam yatakuwa na uwezo wa kuchinja sungura wengi
kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kutenganisha vizuri ngozi, nyama na
kucha," alisema.
Alisema bidhaa zote hizo zitakuwa
zikisafirishwa kuuzwa nje ya nchi ambako
kuna soko kubwa, wakati mkojo na mavi ya wanyama hao yatauzwa nchini kwa
matumizi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mutua, kampuni yake
inakusudia kusafirisha tani mbili za nyama ya sungura kila siku kwenda kuuzwa
nje ya nchi, hivyo kufanya kiasi kwa mwaka mmoja kufikia tani 720.
Alisema mbali na sungura, kampuni yake
inakusudia kuanzisha hoteli mahsusi kwa ajili ya uuzaji wa bidhaa zinazotokana
na sungura pekee.
Utekelezaji wa mradi wa sungura kupitia
Namaingo, utahusisha mafunzo ya kitaalamu kwa wafugaji yatakayotolewa kwa ushirikiano
na watalaamu kutoka Suma JKT na Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA).
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kaimu
Mkurugenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Donald Bombo alisema hatua iliyofikiwa na
Mkurugenzi wa Namaingo, Ubwa Ibrahim kuanzisha mradi huo ni ya ujasiri na
uthubutu unaolenga kuwanufaisha wananchi
na kuinua vipato vyao.
Bombo aliahidi kuwa, serikali itakuwa bega
kwa bega kuhakikisha mipango ya kusaidia kiuchumi wananchi inafanikiwa.
Alisema ujenzi wa machinjio ya kisasa ya
sungura unadhihirisha umoja na ushirikiano thabiti wa wafanyabiashara katika
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Katika uzinduzi huo, jumla ya sungura 600
waligawiwa kwa vikundi 20 vya
wajasiriamali wa Mkoa wa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment