Meneja wa Shirika la Umeme mkoani Kigoma, Masigija Lugata (katikati) akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madidi, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) wakati wa ziara yake Wilayani Kankonko mkoani Kigoma. Wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala.
Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya State Grid Company
anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (REA II) wilayani Kakonko mkoani Kigoma
kuhakikisha anarekebisha kasoro zote zilizo bainika katika mradi huo kabla ya
kuukabidhi hapo tarehe 30 mwezi huu.
Wito huo umetolewa jana
wilayani humo wakati alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme
Vijijini Awamu ya Pili Mkoani Kigoma ambapo alibaini changamoto mbalimbali
ikiwemo ya nguzo za umeme kusimikwa vibaya bila kuzingatia utaalamu hasa
ikizingatiwa kuwa maeneo hayo hua na upepo mkali unaoweza kusababisha nguzo
hizo kuanguka.
Katika ziara hiyo, Profesa
Muhongo alipatiwa taarifa na Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Col. Hosea Ndagala
ambaye alimueleza kutoridhishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa ikiwemo
uduni katika usimikaji wa nguzo za umeme.
Alisema baadhi ya nguzo hizo
zimeanza kuinama kutokana na upepo na kutokana na nguzo hizo kusimikwa bila
ubora hali inayoweza kusababisha madhara kwa Wananchi wa eneo hilo endapo nguzo
hizo zitadondoka.
Kufuatia taarifa hiyo na
ukaguzi alioufanya kwenye eneo la mradi, Waziri Muhongo aliagiza hadi kufikia
mwisho wa Mwezi huu Mradi huo uwe umekabidhiwa kwa Meneja wa TANESCO Kigoma na
kwamba kabla ya kupokelewa Mkuu wa Wilaya naye athibitishe kuridhishwa
utekelezaji wake ikiwemo kurekebisha kasoro zilizobainika ili wananchi
wanufaike na mradi ulio katika ubora unaotakiwa.
Profesa Muhongo alisema endapo
Mkandarasi atashindwa kutatua changamoto hizo na kasoro zilizo jitokeza katika
mradi huo hatoruhusiwa kushiriki katika utekelezaji wa Mradi wa REA III ambao
unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya
Awamu hii ya pili kukamilika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Kampuni ya State Grid, Wilboad Mutabuzi alisema mradi huo wa Kakonko
anaoutekeleza umekamilika kwa asilimia 98 na huku akiahidi kuhakikisha
anashughulikia kasoro zilizobainika ili akamilishe mradi kwa wakati na wenye
ubora unaokubalika.
Mutabuzi alisema gharama za
mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) kwa mkoa wa Kigoma ni shilingi
bilioni 23 na kwamba katika Wilaya ya Kakonko vijiji saba vimefaidika na mradi
huo.
Alisema changamoto kubwa iliyojitokeza ni muitikio
mdogo wa Wananchi kuunganishiwa huduma ya nishati ya umeme kutokana na sababu
mbalimbali.
Alisema kutokana na muitikio
wa wananchi kuwa mdogo imesababisha kushindwa kufikia lengo ambapo kwa Mkoa
mzima wa Kigoma lengo lilikuwa ni kuwaunganishia huduma ya umeme wateja wapatao
11,000 lakini hadi sasa ni wateja 7,000
tu ndio waliopatiwa huduma husika.
No comments:
Post a Comment