September 17, 2016

DC BUHIGWE ALITAKA BARAZA LA MADIWANI KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO




Na Mwandishi wetu, Kigoma
MKUU wa Wilaya ya Buhigwe, Mkoani Kigoma, Col Marco Gaguti (pichani juu) ameeleza kutoridhishwa kwake na kasi ya Ukusanyaji mapato na uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato wilayani Buhigwe.

Kanali Gaguti alisema hayo baada ya Halmashauri hiyo kushindwa kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani ya takribani  shilingi milioni 600 yaliyokusudiwa kukusanywa na badala yake kukusanya asilimia 41 tu kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 licha ya kuwa na vyanzo vingi  vya mapato vilivyopo katika  Halmashauri hiyo.

Aliwataka madiwani kwa kushirikiana na watendaji kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuvuka lengo hilo kwa mwaka huu wa 2016/17.

Kanali Gaguti aliyasema hayo jana katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo wakati wakijadili Malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha mwaka 2016/17 iliyo wasilishwa katika kikao hicho ikiwa na lengo la kukusanya kiasi cha shilingi milioni 600 na kujadili kwanini halmashauri hiyo ilishindwa kufikia malengo ya mwaka wa fedha 2015/16.

Gaguti alisema hayupo tayari kuona halmashauri hiyo inakusanya mapato chini ya kiwango kwasababu za  uzembe wa kubuni mbinu za  ukusanyaji wa mapato kwa halmashauri iliyo mpakani na nchi jirani ya Burundi haiwezi kukusanya sh milioni 600 ni ndogo Sana waongeze ifikie hata bilioni moja.

Aliwataka  madiwani washirikiane na Watendaji kuibua vyanzo vipya  vya mapato na kuweka mikakatii na muda wa kukamilisha mikakati hiyo ili kuhakikisha Halmashauri hiyo inafikia malengo ya ukusanyaji mapato kwa mwaka 2016/17 kuepukana na changamoto ya halmashauri hiyo kukosa fedha za kuiendesha.

 “Ningependa tuanze kuainisha makosa na uzembe tulio ufanya  katika ukusanyaji wa mapato  ya ndani uliyo pelekea ukosefu wa fedha za halmashauri  na tuandae mkakati wa kukabiliana na uzembe huo ambao hauvumiliki. Serikali ya Wilaya itasimama imara kushirikiana na wadau wote kuhakikisha lengo linafikiwa kwa wakati," alisema Kanali Gaguti.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Elisha Bagwenya alisema Baraza lake linaunga mkono hoja ya Mkuu wa wilaya na kusema kuwa Halmashauri inavyanzo vingi vya mapato hivyo uandaliwe utaratibu wa Mkurugenzi na watendaji na madiwani kuunda kamati itakayo kwenda kusimamia mapato ya halmashauri yanayo potea bila sababu kutokana na vyanzo vingi kuwa chini ya usimamizi wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA na Askari wa mipakani.

Alisema Halmashauri iunde vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni pamoja na kuuza vibanda na viwanja kwa wafanya biashara wa Mnanira, Nyamugali,  Kilelema na Muyama ambako kuna masoko ya ujirani mwema, na  kujenga kituo cha magari Manyovu vyanzo hivyo vita saidia kuongeza mapato ya Halmashauri.

Aidha alimuomba Mkurugenzi  wa Halmashauri  hiyo  kuurudisha mnada wa Ng’ombe katika kijiji cha Buhigwe ili wafugaji kutoka Burundi na Tanzania Waweze kuja kuuza na kununua Ng’ombe na mbuzi katika mnada huo na Halmashauri iweze kuingiza mapato kupitia mnada huo.

Nae Diwani wa kata ya Janda Pasco Nkeyemba  alisema tatizo linalo pelekea Halmashauri kushindwa kukusanya mapato ni uzembe wa watendaji Kwani kuna baadhi ya masoko hayana madaftari ya kukusanyia mapato katika masoko na watu wanaingia sokoni kufanya biashara bila kulipia ushuru wa Halmashauri.

Alisema Afisa mipango wa Halmashauri hiyo Kama ameshindwa kazi aachie nafasi hiyo maana amekuwa akiwaachia watendaji wa kijiji kukusanya Mapato hali hiyo imepelekea kushindwa kufikia lengo la mwaka wa fedha uliopita kutokana na watendaji kuzuiliwa na Askari kukusanya mapato na polisi kuchukua fedha hizo na kuziingiza  mifukoni mwao hali inayo pelekea mapato kupotea.

No comments:

Post a Comment