Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu akiongea na baadhi ya akina mama toka mkoani Tanga na Manyara waliofika kupata matibabu. Waziri Ummy aliwatembelea wakati wa uzinduzi wa kambi ya wiki moja ya matibabu ya Fistula.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu akitoa maelekezo kwa viongozi wa mkoa wa Tanga juu ya utekelezaji wa sera ya matibabu bure kwa wazee wajawazito na watoto chini ya miaka mitano baada ya kubaini kasoro katika hospitali hiyo
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu akizindua huduma ya Fistula katika Hospitali ya rufaa ya Mombo
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza na madaktari toka Canada,Pakistani,Afrika ya Kusini,Uingereza na Marekani wanaotoa huduma ya fistula hospitalini hapo
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu akiwa pamoja ya menejimenti ya hospitali pamoja na viongozi wa Taasisi ya The sunshine Muslim Volunteers ya Tanzania
***********
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu (pichani) ameziagiza Hospitali zote za Rufaa nchini ngazi
ya Mkoa, Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa Matibabu Bure kwa Wagonjwa
wa Fistula.
Ummy aliyasema hayo juzi mjini Tanga, katika uzinduzi wa kambi ya matibabu ya Wagonjwa wa Fistula itakayodumu kwa kipindi cha wiki moja kuanzia tarehe 15 hadi 19 agosti,2016 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bombo.BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
"Serikali imejikita zaidi katika kuwahudumia
Wanyonge, kwa mamlaka niliyopewa natoa msamaha wa kulipia matibabu ya Fistula
ili kuwapunguzia mateso wanawake hawa kwa kuwa wenye tatizo la Fistula ni
wanawake wa kipato cha chini na wa vijijini naziagiza Hospitali zote za Rufaa
za Mikoa na Kanda kutoa Matibabu ya Fistula Bure kwa Wagonjwa watakaofika
kutaka Huduma hizo,”alisema Ummy.
Alisema tatizo la Fistula limekuwa likiongezeka kila siku na waathirika wengi ni akina mama wa vijijini na wale wa kipato cha chini ambao wanashindwa kupata huduma sahihi za afya ikiwemo kuchelewa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakati wa kujifungua.
Takwimu zinaonesha kuwa takribani kina mama 2500 hadi 3000 hupata tatizo la ugonjwa wa Fistula kila mwaka japo idadi hii ni ndogo kuliko hali halisi ilivyo kwa kuwa wagonjwa wengi hunyanyapaliwa na familia zao na jamii kwa ujumla.
Waziri Ummy alisema ili kuhakikisha huduma hizo
zinatolewa ameziaagiza hospitali hizo kuandaa Kambi za Matibabu ya Fistula
angalau mara moja kila mwaka na apatiwe Taarifa.
Aidha ,ameeleza kuwa kina mama wengi wenye tatizo la Fistula wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli za uchumi kama biashara ndogo ndogo kwa kuwa ugonjwa huo ni wa aibu ambao hupelekea watu kunyanyapaliwa na jamii.
"Utaratibu huu wa kushirikiana na wadau wa afya, kwani unasaidia kuongeza ujuzi kwa wataalam wakiwa katika maeneo yao ya kazi. Pia,amewaomba wadau hao kuongeza wigo wa ushirikiano katika eneo la Afya ya Uzazi ikiwemo matibabu ya Saratani ya Shingo ya Kizazi"alisema Ummy.
Kuhusu uhaba wa watumishi katika hospitali hiyo ya Rufaa,Waziri Ummy ameahidi kupanga watumishi wanaohitajika katika Hospitali za Rufaa za Mikoa pindi kibali cha ajira kitakapotoka,Vile vile kutoa kipaumbele cha ufadhili wa masomo ya juu kwa madaktari watakaoomba kuchukuwa masomo yatakayowawezesha kubobea kwenye magonjwa ya akina mama na watoto.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Asha Mahita,
alieleza kuwa hospitali ya Bombo inakabiliwa na changamoto
ya kuwa na miundombinu chakavu, uhaba wa vifaa tiba na watumishi kiasi ambacho
wanashindwa kutoa huduma ya kutibu akina mama wenye tatizo la Fistula kwa kuwa
hawana wataalam waliobobea katika maeneo hayo.
Naye Mwenyekiti wa The Sunshine Muslim Volunteers (SMV) Tanzania Dkt Juma Mwimbe alisema wameguswa na tatizo la fistula kwa kuwa linawakumba wanawake maskini na wa hali ya chini. Hivyo wataendelea kujitolea kwa kufanya kambi kama hizi kadri watakavyoweza ili waweze kuwafikia kina mama wengi zaidi hasa wa vijijini.
Kambi hii ya wiki moja inatarajia kuhudumia kina mama wapatao 100 kutoka Mikoa wa Tanga na Manyara ambapo wameweza kupatikana madaktari bingwa 7 kutoka nchi za Afrika Kusini, Pakistani, Australia na Uingereza.
No comments:
Post a Comment