Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza tabia
kwa baadhi ya watu wakiwemo wasanii watu wengine mmoja mmoja kutumia
mavazi yanayofanana na sare za Majeshi ya Ulinzi na usalama hapa nchini
likiwemo Jeshi la Polisi katika shughuli zao za kisanii au katika kazi
mbalimbali, Jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za
Nchi.
Kwa
mujibu wa Sheria ya kanuni za makosa ya Jinai, sura ya 16 na marejeo
yake ya mwaka 2002, kifungu cha 178 (1) na (2) kinachozungumzia makosa
dhidi ya sare za majeshi ya ulinzi na usalama, kinabainisha wazi kuwa
ni kosa kisheria kwa mtu yeyote ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya
ulinzi na usalama kuvaa mavazi yanayotumiwa au kushabihiana na sare za
majeshi hayo bila kibali kutoka kwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Kufuatia
kitendo kilichofanywa na kundi la kisanii la “ Original Comedy” kuvaa
mavazi yanayoshabihiana na sare za Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi
Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam linachukua hatua za kisheria dhidi ya
wasanii hao.
Aidha
Jeshi la Polisi nchini, linatoa onyo kali kwa mtu ama kikundi chochote
kuacha kutumia mavazi yanayofanana na sare zinazovaliwa na majeshi ya
ulinzi na usalama hapa nchini na atakayebainika hatutasita kuchukua
hatua kali za kisheria dhidi yake.
Jeshi
la Polisi linatoa rai kwa wale wote wenye mavazi yanayoshabihiana na
sare za majeshi ya ulinzi na usalama kuzisalimisha mara moja katika
vituo vya Polisi vilivyokaribu nao.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
No comments:
Post a Comment