August 05, 2016

TRA YAKUSANYA TRILIONI 1.055 YA KODI MWEZI JULAI 2016

Mamlaka ya Mapato Tanzania imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Trilioni 1.055 sawa na asilimia 95.6 ya lengo la kukusanya shilingi Trilioni 1.103 iliyopangiwa na Serikali kwa mwezi Julai 2016.

Ikilinganishwa na kipindi kama hiki Mwezi Julai 2015 ambapo TRA ilikusanya kiasi cha shilingi Bilioni 914 kuna ongezeko la asilimia 15.43 ya makusanyo kwa mwezi huu wa Julai 2016 .

Katika mwaka huu wa Fedha 2016/2017 TRA imepewa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 15.1 ikilinganishwa na lengo la shilingi Trilioni 13.32 la mwaka 2015/16.

Mamlaka imejiwekea mikakati thabiti ambayo itaiwezesha kufikia au kuvuka lengo hilo lililopangwa na serikali.

Moja ya mikakati hiyo ni kuhakikisha kuwa walipakodi wapya wanasajiliwa zaidi pamoja na kuhuisha taarifa za walipakodi kwa kuhakikisha kwamba Namba za Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) zisizotumika zinafutwa katika mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. 

Bwana Kayombo amesema Maandalizi ya kuhuisha taarifa za walipakodi yako katika hatua za mwisho yakihusisha kupigaji picha, kuchukua alama za vidole pamoja na vielelezo muhimu vya mlipakodi ili kuhakisha kuwa kila biashara inakuwa na TIN moja tu na taarifa sahihi na za uhakika.

Aidha mkakati mwingine ni kutembelea walipakodi katika maeneo yao ya Biashara ili kuwaelimisha na kuhakikisha wanatekeleza mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi ambazo zimelenga kuiwezesha Mamlaka kufikia lengo la makusanyo lililowekwa na Serikali katika mwaka huu wa Fedha. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.


Kwa upande wa wenye majengo ya kupangisha, TRA itafanya zoezi la kutembelea nyumba hadi nyumba kuhakiki gharama za upangishaji ili kukokotoa na kukusanya kodi sahihi ambayo ilikuwa haifiki serikalini; hivyo wananchi wanaombwa kutunza kumbukumbu za mikataba ya pango ili itakapohitajika na maafisa wa Mamlaka iweze kupatikana mara moja. 

“Natoa wito kwa wapangaji na wapangishaji kujiepusha na aina yoyote ya udanganyifu katika suala zima la kodi halisi ya pango kwa kuwa inaweza kuwasababishia kushitakiwa endapo udanganyifu huo utabainika”

Kwa upande wa kodi za ajira TRA itatembelea waajiri maeneo mbali mbali kuhakiki na kukagua usahihi wa orodha na malipo ya ajira ili kujiridhisha kama kodi za ajira zinakokotolewa na kulipwa serikalini inavyostahili.

Katika kuhakikisha kwamba makusanyo yote yanakusanywa kwa wakati na kwa usahihi, TRA imeboresha zaidi mifumo yake ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto za kutopatikana kwa mtandao ambayo mara nyingi huathiri makusanyo. Hii ni pamoja na kuunganisha mifumo ya TRA pamoja na ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili kuhakisha kwamba Mapato yote ya serikali yanakusanywa kwa usahihi na kwa wakati.

Sambamba na mikakati hiyo TRA inaendelea kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kuhakikisha wafanyabiashara wote wanaostahili kutumia mashine za Kielektroniki za kodi (EFDs) wanazitumia ipasavyo pamoja na ukaguzi wa wateja wanapotoka madukani ili kuhakikisha kwamba wanazo risiti halali na sahihi kwa manunuzi yao.

TRA inawaasa wananchi kuhakikisha wanazikagua risiti zao za manunuzi na kuangalia usahihi wa pesa walizolipa na uhalali wa risriti yenewe. 

Mbali na kusisitiza matumizi ya mashine za kielektroniki za kodi, TRA inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kufuatilia madeni pamoja na kupambana na kudhibiti wa biashara za magendo katika vituo mbalimbali vya mipakani vilivyoshamiri vitendo hivyo.

“Tunatoa wito kwa umma kutoa risiti wakati wa kuuza na kudai risiti wakati wa manunuzi ya bidhaa au huduma kwani Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 imerekebisha sheria ya usimamizi wa kodi ya mwaka 2015 kwamba kutodai risiti kwa manunuzi yoyote kuna adhabu kati ya Shillingi 30,000 na 1,500,000/-

Hivyo kutotoa risiti na kutokudai risiti ni makosa kwa mujibu wa sheria na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kutotoa risiti au kutodai risiti wakati wa mauzo na manunuzi.

TRA itaendelea kukusanya mapato kwa weledi na uadilifu pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hasa katika vipengele vya mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi kama ilivyoainishwa na sheria ya Fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa hivi karibuni ili kujenga uelewa na kukuza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari.

Watanzania wote wanahimizwa kuendelea kuwa wazalendo kwa kulipa kodi kwa hiari na kujenga utamaduni wa kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa au huduma yoyote ili kwa pamoja tuweze kufikia lengo la mwaka huu wa fedha wa 2016/17 na kuiwezesha Serikali kutimiza malengo iliyojiwekea.

Pamoja Tunajenga Taifa Letu
Richard Kayombo
MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI

No comments:

Post a Comment